Marwa aanzishiwa matibabu, alazwa MOI

Marwa Msyomi

Muktasari:

Kijana Marwa Msyomi (30) aliyesotea rufaa ya kufika Muhimbili kwa miaka mitano kutokana na changamoto za kiuchumi, ameanzishiwa matibabu na kulazwa katika Taasisi ya Mifupa (MOI).

Dar es Salaam. Kijana Marwa Msyomi (30) aliyesotea rufaa ya kufika Muhimbili kwa miaka mitano kutokana na changamoto za kiuchumi, ameanzishiwa matibabu na kulazwa katika Taasisi ya Mifupa (MOI).

Marwa aliyeishi zaidi ya miaka minane ubongo ukiwa nje ya fuvu baada ya kujeruhiwa vibaya wakati akiamulia ugomvi Desemba mwaka 2014, amepokelewa leo saa 2 asubuhi katika Kitengo cha Dharura, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kabla ya kupelekwa MOI.

Kijana huyo aliyefika hospitalini hapo akitokea Tarime Mara, alipewa rufaa ya kufika Muhimbili mwaka 2017 baada ya matibabu yake ya mwisho aliyofanyiwa katika Hospitali ya Kanda ya Kaskazini KCMC.

Akizungumza leo Februari 28, 2022 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano MOI, Patrick Mvungi amesema wamempokea Marwa na tayari ameshaanzishiwa matibabu ya awali.

“Tumempokea Marwa Msyomi na tayari wataalamu wetu wapo kwenye uchunguzi kuhusu hali yake na matibabu gani yatakayomfaa kwa sasa kwakuwa alishafanyiwa matibabu hapo awali.

“Kwahiyo nasi madaktari wetu wataendeleza pale ambapo wenzetu waliishia na wataueleza umma kwamba changamoto yake ni nini na kwa sasa wanafanya uchunguzi wa kina kujua tatizo lake ni nini,” amesema Mvungi.

Kutokana na kukatwa katwa mapanga kichwani, fuvu lake lilipasuliwa vibaya, kiasi cha madaktari katika Hospitali ya Rufaa Bugando kufanya maamuzi ya kuondoa eneo la fuvu ikiwa ni sehemu ya matibabu.

Baada ya matibabu ya muda mrefu, tangu Agosti 14, 2017 alipopewa rufaa Hospitali ya Kanda KCMC kwenda katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Marwa Misumi hakufanikiwa kupata nauli ya kumwezesha kuyafikia matibabu, mpaka kanisa lilipomchangia na kufanikiwa kusafiri Februari 21.

Hata hivyo safari ya kutoka Mara kisha Mwanza kuja jijini Dar es Salaam ilikuwa ni yenye misukosuko, iliyojaa unyanyapaa kutokana na hali ya harufu kali inayotoka katika jeraha alilonalo kichwani.