Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Masauni acharuka mfululizo ajali za barabarani

Muktasari:

  • Siku 12 za Desemba,2023 watu 46 wamefariki dunia, Jeshi la Polisi laonya madereva.

Dar es Salaam. Ajali 46 zimeripotiwa kutokea kati ya Desemba mosi na 12, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 46, huku 59 wakijeruhiwa.

Kwa takwimu hizo za Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, takribani watu wanne walifariki dunia kila siku kutokana na ajali za barabarani.

Hii inamaana kila ajali ilisababisha kifo kimoja na majeruhi angalau mmoja.

Kutokana na hali hiyo, Serikali imetangaza hali ya hatari kwa madereva wazembe na wasiozingatia sheria za usalama barabarani.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni leo Desemba 13,2023 ameliagiza Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kutowavumilia madereva wachache wanaogharimu maisha ya Watanzania wengi kwa kuwasababishia vifo na ulemavu.

“Hatuwezi kuruhusu watu wachache waendelee kusababisha upotevu wa roho za Watanzania wenzetu na kuwasababishia ulemavu. Katika hili nasisitiza Jeshi la Polisi kuwa wakali, wasimuonee huruma wala kumuonea mtu,” ameagiza.

Waziri Masauni amesema, “Jeshi la Polisi liongeze doria, hasa katika barabara kubwa na kuongeza ukaguzi kwa magari yote ili yasiwepo yanayoingia barabarani katika hali ya ubovu; madereva walevi, wazembe na wote wanaovunja sheria wachukuliwe hatua.”

Maagizo hayo ameyatoa mbele ya waandishi wa habari baada ya kikao chake na wajumbe wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani.

Pamoja na mambo mengine, kikao hicho kimejadili mipango ya kudhibiti ajali kuelekea kipindi cha mwisho wa mwaka.

Takwimu zinaonyesha kuanzia Januari hadi Desemba 12,2023 zimetokea ajali 1,641 na kusababisha vifo vya watu 1,550. Kati ya hao wanaume ni 1,189 na wanawake 391.

Ajali hizo pia zimesababisha majeruhi  2,562 kati yao wanaume ni 1,721 na wanawake ni 841.

Akizungumza baada ya kupokea maelekezo, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhan Ng’anzi  amesema wamejipanga kikamilifu kuwakabili madereva wakorofi, walevi, wenye magari mabovu na wote wanaovunja sheria za usalama barabarani.

Amesema Jeshi la Polisi kwa kutumia taarifa za Mfumo wa Ufuatiliaji Mwenendo wa Mabasi (VTS), Oktoba na Novemba lilichukua hatua kwa madereva 1,260 waliokiuka ukomo wa mwendo au kuchezea mfumo.

“Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na madereva 1,035 kuandikiwa faini, madereva 37 kufikishwa mahakamani, 31 kufungiwa leseni za udereva na madereva 157 kuonywa,” amesema.

Amsema, “Ufuatiliaji huu utaendelea na hakuna tutakayemuonea huruma endapo atavunja sheria, lengo ni kufanya huduma za usafiri wa mabasi kuendelea kuwa salama.”