Masauni atangaza mambo manne kudhibiti ajali mfululizo
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni.
Muktasari:
- Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni ametangaza kufanya mapitio katika maeneo manne kwamba yatasaidia kupunguza ajali ikiwemo utoaji wa leseni.
Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni ametangaza kufanya mapitio katika maeneo manne kwamba yatasaidia kupunguza ajali.
Maeneo aliyoyataja Waziri Masauni ni eneo la utoaji leseni za madereva TRA, vyuo vya ufundishaji udereva, Wakala wa utoaji leseni kwa vyombo vya Usafiri na kitengo cha ukaguzi wa magari.
Waziri Masauni ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Februari 10, 2023 wakati alizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu matukio ya ajali za mfululizo.
Katika Siku za hivi karibuni kumekuwa na ajali za mfululizo zinazosababishwa na vyombo vya moto lakini matukio ya hivi karibu ni lililosababisha vifo vya watu 20 mkoani Tanga na tukio la jana ambalo lilisababisha vifo vya watu 12 Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.
Leo Masauni akiwa ameambatana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini na maofisa wengine, amesema matatizo ya ajali sasa hayavumiliki na itakuwa aibu Serikali inashuhudia vifo vya Watanzania wasio na hatia.
"Tunafanya mapitio katika maeneo hayo ili tuone na kujiridhisha kama leseni zinazotolewa zinatolewa kihalali au Sheria zinafuatwa, na kwa wenzetu TRA tunaangalia kama wanatoa leseni kwa darasa la mtu aliyependekezwa," amesema Masauni.
Kwa mujibu wa Waziri, lazima kutakuwa na mahali pameteleza katika utekekelezaji wake na hivyo kuna kila sababu kujiimarisha zaidi.
Katika hatua nyingine Waziri amesema hawezi kujibu maswali kwani asingetamani kuwa na mchanganyo wa habari na hiyo ilitokana waandishi kutaka kujua hatima ya gari la Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu ambalo wakati akishambuliwa na risasi 2017 alikuwa akilitumia.