Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Masheikh waonya mmomonyoko wa maadili, mifarakano katika jamii

Shekh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke akitoa mawaidha wakati wa ibada ya Sikukuu ya Eid al Adh’haa iliyofanyika katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

Viongozi wa dini katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga wameiasa jamii kulinda na kusimamia maadili huku ikikwepa migogoro na mifarakano inayoweza kusambaratisha ndoa na familia.

Mwanza. Viongozi wa dini katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga wameiasa jamii kulinda na kusimamia maadili huku ikikwepa migogoro na mifarakano inayoweza kusambaratisha ndoa na familia.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ibada ya Eid al Adh’haa zilizofanyika jijini Mwanza na mjini Shinyanga, viongozi wa dini katika mikoa hiyo ambayo kwa kushirikiana na Simiyu, Mara, Geita na Kagera inaunda Kanda ya Ziwa wamewataka wazazi na walezi kila mmoja katika nafasi yake kutimiza wajibu wa malezi na makuzi ya watoto katika maadili mema.

Akizungumza na waumini wakati wa ibada ya Eid al Adh’haa iliyofanyika katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza leo Alhamisi Juni 29, 2023, Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke ametaja migogoro ya wanandoa inayotokana na kukosa au kuchelewa kupata watoto kuwa miongoni mwa mambo yasiyofaa inayotakiwa kuepukwa kwa sababu inaweza kusambaratisha familia na jamii.

“Mwenyezi Mungu ndiye hutujaalia watoto kadri apendavyo…awe mtoto wa kike au wa kiume; hivyo ni jambo lisilofaa wanandoa kufarakana kwa sababu ya kuchelewa au kutopata mtoto,’’ amesema Sheikh Kabeke

Kiongozi huyo wa dini amewaasa Watanzania kila mtu kwa Imani na dini yake kuishi kwa kuzingatia mafundishi ya kiimani, malezi na makuzi mema yanayolinda mila, desturi na tamaduni za Kitanzania.

‘’Wazazi na walezi tuwafunze tabia njema watoto na vijana wetu huku tukiwaonya dhidi ya kuiga mila, desturi na tamaduni za nje zisizofaa,’’ amesema na kuasa Sheikh Kabeke

Khadija Khery, mmoja wa waumini waliohudhuria swala la Eid al Adh’haa amewaomba wazazi, walezi na viongozi wa dini kuwafundisha vijana tabia ya uvumilivu katika maisha yote yakiwemo ya ndoa akisema huo ndio msingi wa kulinda na kudumisha uhusiano.

‘’Mifarakano ndani ya jamii ikiwemo ya kwenye ndoa ni matokeo ya vijana wengi kukosa mafundisho ya kiimani kuhusu uvumilivu…vijana wengi hawana hofu ya Mungu ndio maana wanashiriki na kufanya mambo yanayokiuka mila, desturi na tamaduni za Kiafrika,’’ anasema Khadija

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Amani na Maridhiano Mkoa wa Shinyanga, Shekhe Hamis Balilusa amewataka Watanzania kukemea vitendo vya mmomonyoko wa maadili ikiwemo ukatili wa kijinsia, ndoa za utotoni na mapenzi ya jinsia akisema siyo tu ni kinyume cha maadili ya Kitanzania, bali pia vinakinzana na mfundisho ya dini zote.

Akizungumza wakati wa Swala ya Eid al Adh’haa iliyofanyika mjini Shinyanga Juni 29, 2023, Sheikh Balilusa amewaomba wote wenye mapenzi mema kushirikiana na Serikali kupitia vyombo na taasisi zake kukemea na kupiga vita vitendo viovu na vya kihalifu ndani ya jamii.

Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga, Ismail Makusanya amewasihi waumini wa dini ya Kiislam kuwatendea mema waumini wenzao na wote wasio wa Imani yao kwa sababu hiyo siyo tu ni miongoni mwa mafundisho, bali pia ni msingi wa Imani.