Masta wa Miamala itakavyochochea malipo kidigitali
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi, Benki ya Stanbic, Emmanuel Mahodanga, akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Masta wa Miamala. Wengine kutoka kushoto ni Avin Ngoo, Meneja Idara ya Mawakala, Irene Mutahibirwa, Meneja wa Uimarishaji wa Mahusiano ya Wateja na Shabani Mwenda, Kaimu Mkuu wa Uboreshaji wa Huduma Binafsi.
Muktasari:
- Kufanya malipo kidigitali hurahisisha maisha kwa kuwa yanaweza kufanyika popote na muda wowote bila kulazimika kwenda benki au ofisini.
Dar es Salaam. Wewe ni mmoja wa wanaoenda kulipa ada za shule, kununua mafuta, au hata kununua vocha za simu kutoka benki, basi habari njema ni kuwa Benki ya Stanbic Tanzania imekuja na zawadi kwa ajili yako.
Benki ya Stanbic imetangaza ujio wa kampeni mpya ya miezi mitatu iitwayo Masta wa Miamala, ikiwa sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 tangu ianze kufanya kazi nchini.
Kampeni hiyo inalenga kuwazawadia wateja wanaofanya malipo ya kila siku kwa njia za kidijitali kama kulipa ada za shule, manunuzi ya bidhaa, mafuta na vocha za simu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na benki hiyo, imesema wateja watakuwa na nafasi ya kushinda zawadi za fedha taslimu hadi Sh100,000 kila wiki mbili, pamoja na bonasi za papo hapo na matukio maalumu kwenye maduka makubwa na vituo vya mafuta.
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Stanbic, Emmanuel Mahodanga, amesema kampeni hiyo ni uthibitisho wa dhamira ya benki katika kuhamasisha matumizi ya huduma za kidijitali.
“Masta wa Miamala ni njia yetu ya kuonyesha kuwa huduma za kidijitali sio tu rahisi na salama, bali pia zenye manufaa kwa wateja wetu. Tukiadhimisha miaka 30 Tanzania, tunataka kila muamala uwe na thamani na uwe sehemu ya safari ya ukuaji wa taifa,” amesema Mahodanga.
Meneja wa Idara ya Mawakala, Avin Ngoo, amesema mtandao wa zaidi ya mawakala 600 wa Stanbic unasaidia kusogeza huduma karibu na jamii.
“Kila muamala, hata mdogo, ni ushahidi kuwa wateja ni sehemu ya familia ya Stanbic,” amesema.
Stanbic imeeleza kuwa washindi wa zawadi wataibuliwa kupitia miamala ya kawaida, huku taarifa zao zikishirikishwa kwenye majukwaa ya kidijitali ili kuonyesha namna huduma za kifedha zinavyoweza kubadilisha maisha ya kila siku.
Hata hivyo, matumizi ya njia za malipo ya kidijitali yamekuwa na manufaa makubwa, hususan katika urahisi, usalama na uwazi wa matumizi ya fedha.
Moja ya faida kubwa ni kupunguza hatari za kupoteza au kuibiwa fedha, kwani miamala yote inarekodiwa na mteja hupata uthibitisho papo hapo.