Mastaa walioongeza familia zao 2020

Friday December 11 2020
New Content Item (2)

Watoto ni baraka! Ndani ya mwaka 2020 kuna familia za mastaa zilishukiwa na baraka hiyo kwa kupata watoto wapya. Hata hivyo, idadi ya mastaa waliopata watoto kwa mwaka huu haikuwa kubwa ukilinganisha na miaka miwili iliyopa ambayo takribani wasanii 9 walipata watoto.

Kwa mwa huu ni mastaa watano tu waliobahatika kuongeza memba wa familia zao kwa maana ya kupata watoto, huku wanne kati yao wakiwa ni wanawake, na mmoja mwanaume. Lakini sio tu kupata watoto, bali pia mwaka 2020 umeweka historia ya kuwaunganisha baadhi ya mastaa na watoto wao waliopotezana muda mrefu.

Sasa tukiwa tunaelekea kwenye kumaliza mwaka, tunakupa list ya mastaa waliopata watoto ndani ya 2020.

AUNTY EZEKIEL

Black Beauty huyu wa Bongo Movie alipokea baraka zake Novemba 27 ambapo alijifungua mtoto wa kiume na kumpachika jina la Noman.

Ujio wa Noman umefanya Aunty Ezekiel kuwa mama wawili kwani kabla ya mtoto huyo kuzaliwa, Aunty alikuwa mama wa mtoto mmoja wa kike anayeitwa, Cookie ambaye ni zao la mahusiano yake na dansa wa WCB, Mose Iyobo.

Advertisement

Yote kwa yote, swali la nani ni baba wa mtoto huyu limebaki kuwa kitendawili kikubwa, kwani mama yake hajaweka wazi na mara zote anapoulizwa swali hilo huwa mbogo ile mbaya. Kwa mfano, Desemba 3 kupitia akaunti yake ya Instagram, Aunty alishusha mkeka mfupi wa kuwachamba watu wanaotungatunga maneno kuhusu ni nani baba wa mtoto huyo.

Hata hivyo tetesi zinasema kwamba mtoto huyo ni wa mwandishi wa nyimbo, jamaa anayefahamika kwa jina la Kusah ambaye pia alikuwa ni mpenzi wa mwanamuziki Ruby na walizaa naye mtoto mmoja mwaka jana.

New Content Item (2)

STAMINA

Mwaka ulifunguka vibaya sana kwa rapa kutoka Morogoro, Boniventure Kabogo A.K.A Stamina kwani ile Januari inaanza tu jamaa aliibuka na kutangaza kuwa amesalitiwa na mkewe na mbaya zaidi mkewe amekimbia nyumbani kabisa. Na hiyo ilimchoma mwana mpaka akaandika wimbo kabisa.

Lakini kabla ya mwaka kuisha, mtoto aliyezaliwa na kupewa jina la Lionel alikuja kumfuta machozi dingi yake.

Stamina alitumia siku ya Desemba 7 kutangaza kuwa amepata mtoto kupitia akaunti yake ya Instagram, lakini pia alitumia siku hiyo kuelezea kwamba ameamua kumpa mwanae jina la Lionel kutokana na ushabiki wake wa soka na mapenzi makubwa aliyonayo kwa mchezaji Lionel Messi wa Barcelona na timu ya taifa ya Argentina. Nyongeza ni kwamba, mtoto huyo alizaliwa Oktoba lakini baba yake aliamua kutangaza Desemba.

QUEEN DARLEEN

Baada ya miezi tisa tu ya ndoa yao, dada wa staa wa muziki kizazi kipya nchini, Diamond Platnumz, Queen Darleen na mume wake Isihaka walibahatika kupata mtoto wao wa kwanza wa kike. Na kwa taarifa yako tu, mtoto huyo aliyepewa jina la Balqis ni wa pili kwa Queen na wa kwanza kwa Isihaka. Dogo alizaliwa Oktoba 10.

ROSE NDAUKA

Muigizaji huyu wa Bongo Movie aliongeza familia baada ya yeye na mume wake anayefahamika kwa jina la Haffiy Mkongwa kupata mtoto wao wa pili Oktoba 9. Mtoto huyo wa kiume aliyepewa jina la Haleem alikuja na baraka zaidi kwani alipozaliwa tu alinasa dili la matangazo la duka la nguo nguo za watoto la Awesome Kids.

New Content Item (2)

TAUSI MDEGELA

Mchekeshaji Tausi Mdegela na mpenzi wake anayefahamika kwa jina la Chriss walifungua mwaka kwa baraka ya kupata mtoto wa kike wanayemuita Patrivah. Kwa mujibu wa Tausi, kupata mtoto ilikuwa ni ndoto yake kubwa maishani ambayo kwa kipindi alichoishi duniani alifanikiwa kuitimza kwa mara ya kwanza kwenye mwaka huu unaiosha ‘kesho kutwa’

MASTAA WENGINE

Mbali na watoto wa mastaa kuzaliwa, pia mwaka 2020 ulibamba kwa matukio yalihusisha mastaa na watoto wao. Tukio kubwa zaidi lilitokea mwezi Novemba ambapo bosi wa WCB, Diamond Platnumz alikutana na watoto wake kwa mara ya kwanza 2018.

Diamond alikutana na watoto wake Tiffah na Nilan aliozaa na mfanyabiashara wa Kiganda anayeishi Afrika ya Kusini, Zarina Hassan ambapo watoto hao walikuja hapa Bongo na kukaa kwa takribani siku 10.

Kwa upande mwingine, 2020 ilituzawadia mshangao mkubwa baada ya bosi wa lebo ya Konde Gang, Harmonize kutangaza alikuwa na mtoto ambaye siku zote alificha akihofia kuachwa na mpenzi wake, muitaliano Sarah Michelotti kwa sababu mtoto huyo alizaa nje ya ndoa.

Advertisement