Matangazo ya mtandaoni kukatwa kodi

Muktasari:

  • Serikali inatarajia kuja na mfumo wa kidijitali wa kufuatilia na kuhakikisha kodi kupitia matangazo yanayowekwa katika mitandao ya kijamii zinalipwa kwa wakati.

Dar es Salaam.  Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inatarajia inatarajia kuanzisha mfumo wa kidijitali wa kufuatilia na kuhakikisha kodi husika za Serikali kupitia matangazo yanayowekwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kama vile Instagram, Facebook, Twitter na Blogs zinalipwa kwa wakati.

Hayo yameelezwa leo Juni 15 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 bungeni jijini Dodoma.

Mwigulu amesema uamuzi huo unatokana na ukuaji wa teknolojia ambao umeleta mabadiliko pia katika tasnia ya matangazo ya kibiashara (Advertisment).

“Dunia inashuhudia mabadiliko makubwa katika tasnia ya matangazo ya kibiashara  ambapo sasa matangazo mengi yamekua yakifanyika kupitia mitandao (online advertisement) hasa mitandao ya kijamii” amesema.

Pia amesisitiza kuwa utaratibu huo utajumuisha matangazo ya biashara ambayo huwekwa na watu maarufu.