Serikali kuipatia mtaji MSD

Muktasari:

  • Kufuatia kusuasua kwa Bohari ya Dawa (MSD) Serikali imesema inakusudia kuipatia mtaji taasisi hiyo ili iweze kufanya kazi kwa kujitegemea na si kutegemea fedha serikalini ili kujiendesha.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amependekeza kutenga fedha kwa ajili ya kuipatia mtaji MSD ili ifanye kazi kama bohari ya dawa na siyo kama Kitengo cha Ununuzi wa Dawa Serikali.

#LIVE: Uwasilishwaji wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024

Dk Mwigulu amependekeza hayo leo Alhamisi Juni 15, 2023 wakati akiwasilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2023/24 bungeni jijini Dodoma.

“Serikali imeendelea kuboresha ununuzi wa dawa, vifaa na vifaa tiba ambapo mpaka sasa kiasi cha Sh485 bilioni zimetolewa kupitia Bohari ya Dawa MSD, hii ni njia ya kuona huduma za afya zinaendelea kuimarishwa hivyo kufikia mwaka 2023/2024 Serikali itaendelea kutenga fedha zaidi,” amesema Mwigulu na kuongeza;

“Serikali itaendelea kutenga fedha kwa kuipatia mtaji MSD ili ifanye kazi kama bohari ya dawa na si kitengo cha ununuzi wa dawa Serikali,” amesisitiza.

Amesema Serikali imepanga kulipa madeni ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili kuiwezesha kuendelea kutoa huduma hapa nchini.

Ametaja mipango mingine kuwa ni pamoja na ukamilishaji hospitali tano za rufaa za mikoa mipya ikiwemo Hospitali ya Katavi ambayo mpaka sasa tayari Sh15.3 bilioni zimetolewa.