Mateso ya saa 8 bila umeme, Tanesco yatoa tamko

Evelyne Staphord muuza Samaki wa Soko Kuu la Chifu Kingalu lililopo Manispaa ya Morogoro, akipanga samaki kwenye jokofu, hata hivyo jokofu hilo halikuwa na barafu ya kutosha kutokana na umeme kukatika katika maeneo mengi ya manispaa hiyo. Picha na Johnson James

Muktasari:

  • Umeme uliokatika usiku wa kuamkia leo kwa takriban saa nane umeleta adha katika maeneo mengi ya nchi.

Dar/Mikoani. Wananchi katika mikoa mbalimbali nchini wameeleza adha waliyoipitia kuanzia saa nane ya usiku wa kuamkia leo Jumatatu Aprili mosi, 2024 baada ya umeme kukatika karibu mikoa yote nchini.

Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limeeleza kuwa imetokea hitilafu kwenye mfumo wa njia ya kusafirishia umeme ya gridi ya Taifa.

Taarifa ya Tanesco imeeleza kwamba hitilafu hiyo iliyotokea kuanzia saa 8:22 usiku imesababisha baadhi ya maeneo nchini kukosa umeme.

“Shirika linawaomba uvumilivu wateja wake katika kipindi hiki ambacho umeme unakosekana, wataalamu wetu wanaendelea na jitihada za kurejesha huduma,” imesema taarifa hiyo.

Hata hivyo, wananchi katika maeneo mbalimbali nchini wameeleza changamoto na mateso waliyopitia kwa saa zaidi ya nane kwa kukosekana kwa nishati hiyo ambayo hivi karibuni makali ya mgao wake uliodumu kwa zaidi ya miezi mitatu, yalikuwa  yamepungua baada ya kuwashwa kwa mtambo mmoja kwenye bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere.

Hadi kufikia saa 4:00 asubuhi, maeneo mengi yaliendelea kuwa gizani huku machache yakianza kupata umeme.

Na baadhi ya wafanyabiashara wanaotegemea umeme kufanya kazi wakieleza mateso waliyopitia ikiwamo biashara zao kuathirika huku badhi yao wakilazimika kutumia jenereta.

Katika Jijini Dar es Salaam, maeneo mengi yamekosa umeme tangu Saa 8:22 alfajiri ya kuamkia leo huku uzalishaji kwa wanaotumia nishati hiyo ukikwama, wakati wazalishaji wakubwa wakieleza namna wanavyoathirika na kulazimika kutumia dizeli.

Wamesema, suala la umeme linatakiwa lipewe kipaumbele kama nchi inataka kuinua uchumi kwa kuwa gharama za kutumia dizeli ni kubwa kulinganisha na za umeme.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Coca cola Kwanza Ltd, Unguu Sulay amesema umeme unapokatika mara kwa mara ukirudi unakuwa na nguvu kubwa, tofauti na wakati mwingine husababisha kuungua kwa vifaa vya kuendeshea mashine.

“Inatuongezea gharama ya kununua vipuri kwa fedha ambazo hujazipangia na wakati mwingine vipuri havipatikani , inatulazimu kuviagiza nje ya nchi na hadi vifike ni wiki tatu hadi mwezi mmoja.

“Mzunguko huo unaathiri mwenendo wa uzalishaji na kutokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji zinazosababishwa na kukatika katika kwa umeme, kuna uwezekano mkubwa bei za bidhaa zikapanda na kumuathiri mlaji moja kwa moja.

Baadhi ya vituo vya mafuta ambavyo havina jenereta leo havikuwa na huduma hivyo vyombo vya moto kulazimika kutafuta vingine vyenye huduma. Hata taa za kuongoza magari zilikuwa zimezima katika maeneo mengine.

Mjini Morogoro, katika maeneo mengi ikiwamo Hospitali ya rufaa ya mkoa, Soko kuu la Chifu Kingalu, Kituo cha Mabasi Msamvu na kwenye vituo vingi vya mafuta wamelazimika kutumia jenereta huku shughuli nyingi za saluni na steshenari zikisimama kwa muda.

Evelyne Staphord, mmoja wa wauza samaki wabichi aina ya sato na sangara katika soko kuu la Kingalu amesema biashara hiyo inategemea uwepo wa umeme kwa kuwa samaki wanahifadhiwa kwenye jokofu ili wasiharibike.

“Tunapokosa umeme kwa muda mrefu ni hatari na tunapata hasara ambayo inakwenda kuyumbisha mitaji yetu,” amesema.

Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro wamelazimika kutumia jenereta kwa kipindi chote ambacho umeme haukuwepo.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Kusirye Ukio amesema jenereta hiyo imekuwa ikitoa huduma kwenye wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu ICU, wodi ya watoto wadogo waliozaliwa na uzito mdogo (njiti) na maeneo yote muhimu yanayohitaji mwanga.

Kwenye vituo vya mafuta vinavyotumia jenereta, kumekuwa na foleni za magari, bodaboda na vyombo vingine vya moto vikisubiri kupata huduma.


Maji shida

Mjini Dodoma, wilaya tano za Dodoma , Chamwino, Kongwa, Kibaigwa na Bahi zimekosa huduma ya maji kutokana na hitilafu hiyo ya umeme.

Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha mawasiliano cha Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Dodoma (Duwasa), uzalishaji na usambazaji wa maji ungeendelea baada ya umeme kurejea.

Mbali na kukosekana kwa huduma ya maji, pia shughuli nyingi kwenye migahawa, steshenari, vituo vya mafuta nazo zilikwama huku baadhi wakitumia jenereta.

Mmiliki wa kiwanda cha kuoka mikate jijini hapa, Sheila Hamza amesema amelazimika kusimamisha uzalishaji kutokana na kukosekana umeme hivyo wafanyakazi kiwandani hapo hawana kazi ya kufanya hadi umeme utakaporejea.

Wilayani Handeni baadhi ya wananchi wameishauri Tanesco kutafuta njia mbadala ya kuzalisha nishati hiyo ili kukabiliana na tatizo kama hilo kutokea.

Wamesema si mara ya kwanza kutokea hitilafu kwenye gridi ya Taifa. “Umeme unapokatika, sisi wafanyabiashara wadogo tunaathirika zaidi, wengi hatuna jenereta, mfano mimi nafanya biashara ya samaki wabichi, majokofu niliyonayo hayamudu kuweka barafu muda mrefu, kukatika kwa umeme kwa zaidi ya saa nane kwangu ni hasara,” amesema Haruna Yusuph.

Joshua Kimario mfanyabiashara wa nyumba ya kulala wageni anasema umeme unapokatika kuna baadhi ya wateja hufoka na wengine hufikia hatua ya kuhama kutokana na karaha ya joto na giza.

Jijini Mwanza, mfanyabiashara wa saluni ya kunyoa iliyopo Buhongwa, John Mwakyuse anasema kukosekana kwa umeme leo kumempa wakati mgumu kupata kipato cha kujiku na familia yake.

“Tangu saa 10 alfajiri hadi sasa (5:30 asubuhi) hatuna umeme, nikija kijiweni (saluni) ndipo Napata pesa ya kula na familia, hivyo hitilafu hiyo imehatarisha hata ustawi wa familia yangu.

"Nina wazazi wanaonitegemea, nikifanya kazi siku nzima sikosi Sh5,000 kama faida, naigawa kwa wanangu na wazazi, leo ndiyo hivyo hakuna umeme, Tanesco ingetufikiria na sisi tunaotegemea nishati hiyo ili kuendesha familia zetu,” amesema John.

Fundi Simu katika Mtaa wa Kaluta, Mohammed Jamal amesema kukosekana kwa umeme kumesababisha apoteze wateja waliofika hapo kwa ajili ya kupata huduma ya kutengenezewa simu mapema leo asubuhi.

"Sisi mafundi simu tunatumia umeme saa 24 bila umeme huwezi kufanya chochote na mpaka sasa tayari nimepoteza fedha kwa sababu kuna wateja wengi tu wamekuja na kuondoka, nawaomba mafundi wanaofanya matengenezo katika gridi ya Taifa wajitahidi kufanya haraka umeme urudi, wengi tunakwama,”.

Kutoka jijini Arusha, John Raphael mmiliki wa bucha la samaki na kuku eneo la Moshono amesema baada ya huduma hiyo kukatika tangu jana anahofia bidhaa zake kuharibika.

"Kiukweli naona nitapata hasara kubwa kwani nina mzigo mwingi bado na tangu jana umeme ulivyokatika hadi asubuhi hii naona kabisa vitaanza kuharibika, sina jenereta, tunaomba Tanesco waharakishe marekebisho," amesema.


Mkoani Mbeya

Baadhi ya wafanyabiashara wa mashine za kusaga nafaka wamesema huwa wanalazimika kukesha kukoboa na kusaga nafaka, lakini leo imeshindikana kutokana na kukatika kwa umeme usiku wa manane.

Inaelezwa, tangu jana Machi 31, 2024 kuanzia saa 5 usiku maeneo mengi jijini humo hayakuwa na umeme ilipofika saa 4:45 ukarejea kisha ukakatika tena.

Christopher Joseph anasema “hatujui wanarudisha saa ngapi, foleni ya kusaga na kukoboa nafaka ndiyo kama hii unayoiona.”

Wakati Joseph akilalamikia hali hiyo, mfanyabishara wa barafu, Catherine Joel amesema amepata hasara kwa kuwa alifunga zaidi ya paketi 150 alizotarajia kuziingiza sokoni asubuhi, zote zimeyeyuka.

Hali hiyo imeendelea mjini Moshi ambako kumekuwa na giza totoro tangu umeme ulipokatika saa 8:20 alfajiri huku baadhi ya wanachi wakibainisha kwamba hali hiyo inatishia usalama na kuwafanya walale macho kwa kuhofia wezi na vibaka.

Mfanyabiashara Nasra Himid alisema kifaa cha kutunzia data (BVR) cha mfumo wake wa kamera za usalama (CCTV) kinatumia umeme, hivyo kitendo cha umeme kukatika kuanzia saa 8 usiku kilimfanya alale usingizi wa mang'amng'am kwa kuwa hawezi kuona nini kinaendelea nje ya nyumba yake.

Unguja nako umeme ulikatika kuanzia saa 8:30 alfajiri na kusababisha baadhi ya shughuli zinazotegemea nishati hiyo nyingi  kudorora.

Wasiwasi zaidi ulikuwa kwa wafabiashara wa samaki wabichi kwenye Soko la Darajani kama ilivyo kwenye mikoa mingine wamelalamikia kukosekana kwa nishati hiyo wakihofu samaki wao kuoza.

Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco), limesema bado halijajua ni wakati gani umeme ungerejea kwa sababu wanaendelea kuwasiliana na wenzao wa Tanesco.

Katika wilaya za Geita na Sengerema baadhi ya wafanyabaishara ikiwamo vinyozi wamelazimika kufunga biashara zao kutokana na changamoto hiyo huku kwenye maduka makubwa wakitumia jenereta.

Mkazi wa Bomani mkoani Geita, Ruben Charles amesema hawezi kuwasha jenereta kunyoa kwas ababu wateja wake hawatamudu gharama Sh3,000.

"Kichwa kukiwa na umeme nanyoa kwa buku au buku mbili (Sh1,000 hadi 2,000), sasa kwa jenereta ukimwambia mteja Sh3,000 hakubali, inabidi tusubiri tu umeme urudi" amesema Charles.

Lilian Kavishe anaefanya biashara ya Saluni ya kike amesema licha ya kuwa ni sikukuu hawezi kufanya kazi kwa jenereta kwa kuwa wateja hawamudu gharama.

Hali hiyo haitofautiani na wilayani Sengerema mkoani Mwanza ambapo mfanyabiashara wa vinywaji, Amos Kone ameeleza kuhofia biashara yake kudorora huku akiiomba Tanesco kurejesha nishati hiyo.

Imeandikwa na Florah Temba, Hawa Mathias, Janeth Mushi, Mgongo Kaitira, Anania Kajuni, Johnson James, Juma Isihaka , Rachel Chibwete, Jesse Mikofu, Muhammed Said, Rehema Matowo, Daniel Makaka na Imani Makongoro