Tanesco yafafanua changamoto ya umeme kipindi cha mvua

Muktasari:

  • Tanesco imebainisha kwamba mvua zinazoendelea kunyesha kwenye maeneo mbalimbali nchini zimeathiri miundombinu ya umeme, jambo lililosababisha upatikanaji wa nishati hiyo kuwa hafifu.

Dar es Salaam. Wakati kero ya mgao wa umeme ikiwa haijapoa katika maeneo mbalimbali nchini, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limeeleza kuwepo na hali duni ya upatikanaji wa umeme katika kipindi hiki cha mvua.

Tanesco imebainisha kwamba mvua zinazoendelea kunyesha kwenye maeneo mbalimbali nchini zimeathiri miundombinu ya umeme, jambo lililosababisha upatikanaji wa nishati hiyo kuwa hafifu.

Vilevile, imetahadharisha watu kukaa mbali na ilipo miundombinu ya umeme hasa kipindi hiki cha mvua kwa kuwa ni hatari kwa usalama.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirika hilo leo Januari 21, 2024, baadhi ya nguzo na transfoma zimeanguka kutokana na mvua hizo.

“Baadhi ya transfoma zimeangushwa na maji na nguzo kuanguka kutokana na upepo mkali.

“Wataalamu wetu wanashindwa kufika kwa haraka kwenye maeneo yaliyoathiriwa kutokana na miundombinu ya barabara na madaraja kuharibika,” inaeleza taarifa hiyo na kubainisha hali hiyo imesababisha upatikanaji wa umeme kwenye maeneo mengi kuwa duni.

Hata hivyo, shirika hilo limesema linaendelea kufanya marekebisho ya miundombinu ya usambazaji wa umeme katika maeneo yaliyopata hitilafu kutokana na mvua hizo ili kuhakikisha huduma inarejea kwenye hali yake ya kawaida kwa haraka.