Kukatika umeme mwisho Machi 2024

Muktasari:

  • Tanesco imesema kuna upungufu wa Megawati 400 kwenye gridi ya Taifa kwa sasa huku kukiwa na ongezeko la megawati 12 ya matumizi kulinganisha na mwaka jana.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme (Tanesco), Gisima Nyamohanga amesema changamoto ya umeme inayoendelea nchini itaanza kupungua wiki mbili zijazo, huku akibainisha kuwa hadi kufikia Machi mwakani changamoto iliyopo sasa itakuwa imekwisha.

Jana Rais Samia Suluhu Hassan akiwaapisha wateule wapya, Ikulu jijini Dar es Salaam, alitaka changamoto ya umeme iliyopo nchini iishe katika kipindi cha miezi sita ijayo, alipokuwa akiwaapisha viongozi aliowateua akiwamo Nyamohanga.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Septemba 27, Nyamohanga aliyechukua nafasi ya Maharage Chande, amesema mpaka sasa kuna upungufu wa megawati 400.

Amesema kipindi hiki changamoto imesababishwa na matengenezo yanayoendelea katika baadhi ya visima vya gesi asilia.

"Pia ndani ya Shirika tunaendelea kufanyia matengenezo baadhi mitambo ya Ubungo namba moja na namba mbili na ule wa gesi wa Kinyerezi.

"Hivyo vyote vimepelekea upungufu wa megawati 400 na kusababisha tatizo la upatikanaji umeme kwenye maeneo tofauti," amesema.

Mbali na mikakati ya Shirika, amesema wamepokea maagizo ya Rais Samia kupitia wizara ya Nishati kuhusu tatizo la umeme na kuweka mikakati mahsusi ya kukabiliana nayo.

"Kwanza ni kukamilisha matengenezo niliyoyataja, pia kuharakisha ukarabati wa visima vinavyozalisha umeme wa gesi asilia na katika hili tunashirikiana na wadau wetu wa TPDC.

Amesema kiwango cha upungufu kitaanza kutatuliwa polepole, wiki mbili zijazo tatizo litaanza kupungua.

"Mpango ni kuongeza megawati 100 kila mwezi, na hadi kufikia Machi, changamoto iliyopo sasa itakuwa imekwisha.

"Kuna changamoto ya upungufu katika vituo vyetu vya kuzalisha umeme ambazo zimechangiwa kwa kiasi kikubwa za kuongeza kwa shughuli za kiuchumi zinazotumia umeme.

"Mwaka huu kuna ongezeko la megawati 12 la matumizi kulinganisha na mwaka jana, lakini pia atizo la upungufu umetokana na ukame unaosababishwa mabadiliko ya tabia nchi ambayo yameathiri viwango vya maji katika mabwawa," amesema.

Amesema, wanaendelea kukamilisha pia mradi wa Bwawa la Nyerere ambao utakamilika mwishoni mwaJuni, Mwakani na kuzalisha megawati 2115.

"Mradi huu ukikamilika utamaliza kabisa changamoto ya umeme, utazalisha megawati zaidi ya hizi 1900 tunazozalisha kwa sasa kwenye vyanzo vyetu vyote,"