Matiko atoa ushuhuda bungeni aliyoona gereza la Segerea

Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha makadiro ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Mbunge huyo wa Tarime Mjini (Chadema), amesema katika gereza hilo kuna mlundikano wa mahabusu, watu kubambikiwa kesi na wanaoletwa wakiwa wamebakwa na kulawitiwa na polisi

Dodoma. Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko, ametumia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani mwaka 2019/20 kusimulia aliyoyashuhudia katika gereza la Segerea alikokaa kwa siku 104.

Baadhi ya mambo aliyoyaeleza ni mlundikano wa mahabusu huku wengi wakiwa na kesi zinazodhaminika  na baadhi ya watuhumiwa wanawake kubakwa na kulawitiwa na askari katika vituo vya polisi vya Kawe, Stakishari na Mabatini.

Matiko na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, walikuwa mahabusu katika gereza la Segerea walikokaa kwa siku 104 baada ya kufutiwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, katika kesi ya jinai inayowakabili mahakamani hapo.

“Nilipokuwa Segerea walikuja wasichana watatu wamebakwa na kulawitiwa wakiwa vituo vya polisi, Stakishari, Kawe na Mabatini. Wengi walikuwa wameharibika, jamani sasa tukisema tuonekane wabaya,” amesema Matiko na kuongeza:

“Hivi kwa nini mnafurahia kulundika raia mahabusu, pale Segerea asilimia 80 ni mahabusu. Kuna mfanyakazi wa ndani aliletwa akituhumiwa kuiba Sh800,000 tena alikuwa mfanyakazi wa ndani wa kigogo mmoja na alifuatwa Bukoba na kurudishwa Dar es Salaam kwa ndege kwa kuiba kiasi hiki cha fedha. Huku ni kutumia vibaya fedha za wananchi.” 

Amesema akiwa katika gereza hilo waliletwa vijana wakituhumiwa kutakatisha Sh10 milioni wakitokea Mwanza. “Tena wamenyimwa dhamana na kati yao kuna mama ana mtoto wa miezi 12, hivi kiasi hiki ni utakatishaji kweli?” amehoji.

Pia, amesema askari magereza hutumia fedha zao kusafirisha mahabusu na wafungwa wakati ikijulikana kiwango chao cha mshahara ni kidogo na wana madai mengi ambayo hawajalipwa.