Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matinyi: Ripoti kutathmini uchumi vyombo vya habari mbioni

Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi.

Muktasari:

  • Serikali imesema Kamati ya kutathmini hali ya uchumi wa vyombo vya habari, imekamilisha rasimu ya ripoti ya kwanza jana na hivi karibuni itawasilishwa kwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Dodoma. Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Mohbare Matinyi amesema tayari kamati ya kutathmini hali ya uchumi wa vyombo vya habari, imekamilisha rasimu ya ripoti ya kwanza jana Ijumaa Desemba 15, 2023 na hivi karibuni itawasilishwa kwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.

Machi, 2023 Waziri Nape aliunda Kamati kwa ajili ya kutathmini hali ya uchumi wa vyombo na waandishi wa habari nchini.

Kamati hiyo yenye wajumbe 10 awali ilipewa miezi mitatu kuja na ripoti, lakini baadaye iliongezewa muda na kutakiwa kutumia miezi sita.

Akizungumza kwenye mahafali ya Chuo cha Utangazaji na Uandishi wa habari Dodoma (Domeco) leo Jumamosi Desemba 16, 2023 Matinyi amesema baada kukabidhi ripoti hiyo kwa waziri, itawasilishwa serikalini ili kuona uwezekano wa kuiokoa sekta ya habari isitetereke.

“Waziri wa Habari aliunda Kamati ya tathmini ya hali ya uchumi wa vyombo vya habari na wanahabari ili ifanye utafiti wa kitaalamu na kutoa mapendekezo kwa Serikali, ambayo yanaweza kutatua matatizo haya (ya kiuchumi).

“Kamati hiyo imemaliza rasimu ya ripoti ya kwanza jana na katika siku zijazo itawasilisha ripoti hiyo kwa waziri ambaye ataifikisha serikalini ili tuone uwezekano wa kuokoa jahazi kwenye sekta ya habari,” amesema Matinyi.

Aidha Matinyi amesema kukua kwa teknolojia na matumizi yasiyo sahihi ya mitandao na mipaka yake kumechangia kupunguza matangazo, hivyo kupunguza mapato ya vyombo vya habari nchini.

Aidha, kutokana na hali hiyo, Matinyi amesema kumesababisha vyombo vya habari kuwa na hali ngumu kiuchumi, kupungua kwa idadi yake hasa kwenye vyombo vinavyohitaji mitaji mikubwa kama magazeti.

Matinyi amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo ni muhimu vyombo vya habari kuongeza ubora na ubunifu ili kuleta ushindani kwenye kazi zao.

Akisoma risala Makamu Mkuu wa chuo, Hamisi Hussein amesema wanafunzi wanakabiliwa na changamoto ya kukosa nafasi za kujitolea au kufanya mazoezi kwa vitendo katika vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Hussein amesema changamoto hiyo inapunguza ubora wa kujifunza kwani taaluma hiyo inahitaji mafunzo ya vitendo zaidi kuliko darasani.

Aidha ameiomba Serikali kuwapa mikopo wanafunzi wa vyuo vya kati, binafsi ili kumudu gharama za masomo  kwani wengi huishia njiani kutokana na changamoto za ukosefu wa ada.

Katika mahafali hayo ya sita wanafunzi 70 wa ngazi ya astashahada na 70 wa ngazi ya stashahada ya utangazaji na uandishi wa habari wametunukiwa vyeti vya kuhitimu.

Mmoja wa wanafaunzi waliohitimu stashahada chuoni hapo, Victoria Aloyce ameziomba taasisi za Serikali kuwa na utaratibu wa kuchukua wanafunzi kufanya mazoezi kwa vitendo kwenye vitengo vyao vya habari.