Matukio ya ukatili wa kingono yatishia Mlimba

Sunday May 02 2021
ukatili pc
By Mwandishi Wetu

Morogoro. Matukio ya ukatili wa kingono yamezidi kuongezeka wilayani Kilombero mkoani Morogoro hususani katika Halmashauri ya Mlimba ambako kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu jumla ya watoto 57 wamefanyiwa unyanyasi tofauti ukiwemo kulawitiwa, kubakwa na kupewa mimba wakiwa na umri mdogo.

Taarifa hiyo ilitolewa jana na Afisa  Ustawi wa Jamii wa halmashauri hiyo ya Mlimba, Latifa Kalikawe katika hafla ya utoaji zawadi kwa wanafunzi wa kike waliofanya vizuri kimasomo pamoja kuendesha klabu za kupinga ukatili kwa watoto na namna ya kujitambua zilizoanzishwa na Shirika la Plan International Tanzania.

Afisa huyo alisema kuwa matukio hayo watoto waliobakwa walikuwa 21, waliolawitiwa watano na waliopata mimba walikuwa 31 na kuwa katika Halmashauri ya Mlimba ina hali mbaya zaidi hii ni kutokana na jiografia ya halmashauri hiyo ambayo eneo lake kubwa liko vijijini na pia halmashauri hiyo ni changa.

 "Sio tu ukatili umeongezeka isipokuwa elimu imezidi kuwafikia watoto wengi na hivyo sasa hivi wana uwezo wa kutoa taarifa mahali husika ikiwemo polisi na kwa walimu wao," alisema Kalikawe.

 Alitoa rai kwa jamii kuendelea kushirikiana na serikali katika kutokomeza matukio ya kikatili kwa watoto hasa wa kike ambao wanaonekana kufanyiwa ukatili zaidi kuliko watoto wa kiume.

Kwa upande wake,  Mwakiishi wa Shirika Plan International Tanzania, Roda Msigala alitaja sababu zinazosababisha ukatili wa kijinsia kwa watoto kuwa ni pamoja na watoto wengi kutelekezwa na familia zao kutokana na na migogoro ya kifamilia, elimu duni kwa baadhi ya familia na mila na desturi hivyo shirika hilo limeamua kuunda klabu za watoto katika baadhi ya shule za msingi na sekondari ili kuwajengea wezo watoto wa kujiamini.

Advertisement

Aidha kutokana na watoto wa kike kuonekana kuwa ndio waathirika wakubwa wa matukio hayo ya kikatili kuliko watoto wa kiume, shirika limeendelea kuwajengea uwezo zaidi wa uelewa kwenye makuzi yao ili waweze kukabiliana na vishawishi pamoja na changamoto zitakazoweza kuwapeleka kwenye kufanyiwa matukio ya ukatili.

Alisema katika wilaya ya kilombero shirika linaendesha miradi minne ambayo yote inahusu watoto na mradi mmoja unajihusisha na utoaji wa elimu ya kujitambua kwa watoto wa kike ambapo shirika pia limewapa watoto wa kike jumla ya taulo za kike boksi 725 na zawadi mbalimbali zikiwemo vifaa vya michezo ambavyo vyote vina thamani ya Sh10 milioni pamoja na kuunda klabu wa kupinga ukatili na za kutoa elimu ya kujitambua kwa shule saba za msingi na sekondari wilayani humo.

Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi walilishukuru shirika hilo kwa kuisaidia serikali katika mapambano dhidi ya ukatili kwa watoto hasa wa kike.

Mmoja wa wanafunzi hao, Mariam Saidi alisema watoto wa kike wamekuwa wakikabiliwa na vishawishi vingi wanapokwenda shule ama kurudi nyumbani hivyo aliiomba serikali kuongeza kasi ya ujenzi wa shule za bweni ili kuepuka vishawishi hivyo.

Advertisement