Matumaini mapya mtoto aliyekuwa na uvimbe shingoni
Jopo la madaktari bingwa chini ya uratibu wa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Jumuiya ya Afya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA HC) pamoja na shirika la KIDS OR wakiwa katika chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Mount Meru jijini Arusha Julai 24, 2026.
Muktasari:
- Kambi ya madaktari bingwa jijini Arusha imefanikiwa kumuondoa uvimbe mtoto wa miaka minne, ikitoa matumaini mapya kwa familia na mgonjwa.
Dar es Salaam. Mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minne, Fahad Kijiwe ameondolewa uvimbe mkubwa uliokuwa nyuma ya shingo yake kupitia upasuaji uliofanywa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, ukiwa sehemu ya kambi ya madaktari bingwa wa upasuaji inayoendelea hospitalini hapo.
Upasuaji huo umefanyika jana Jumamosi, Julai 24, 2026 na jopo la madaktari bingwa chini ya uratibu wa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Jumuiya ya Afya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA HC) pamoja na shirika la KIDS OR, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.
Akizungumza baada ya upasuaji huo, Daktari Bingwa wa Upasuaji na Saratani, ambaye pia ni Profesa Mshiriki wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Larry Akoko amesema uvimbe huo ulikuwa unaongezeka sambamba na ukuaji wa mtoto na kuanza kuathiri mkao wake.
Amesema kutokana na ukubwa wa uvimbe huo, mtoto alikuwa akitembea akiwa ameinamisha shingo, hali ambayo ingeweza kusababisha madhara makubwa zaidi iwapo asingepatiwa matibabu kwa wakati.
"Bila kufanya upasuaji, uvimbe huo ungeendelea kukua na kusababisha matatizo ya shingo, maumivu ya mgongo na kuathiri ukuaji wa mtoto. Kwa kushirikiana na madaktari wenzangu tumefanikiwa kuuondoa na matarajio yetu ni kwamba hautajitokeza tena," amesema Dk Akoko.
Amesema mafanikio ya upasuaji huo yanaonyesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha huduma za kibingwa katika hospitali za rufaa za mikoa ili wananchi wenye magonjwa yanayohitaji matibabu maalumu, wapate huduma karibu na maeneo wanayoishi bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kwenda hospitali za rufaa za taifa.
Pia, ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuendesha kambi za madaktari bingwa zinazowafikia wananchi moja kwa moja.
Kwa upande wao, wazazi wa mtoto huyo wamesema wameishi kwa hofu kwa muda mrefu wakishuhudia uvimbe huo ukiongezeka kadri mtoto alivyokuwa akikua, huku wakikosa uhakika wa lini angepata huduma ya kibingwa.
Baba wa mtoto huyo, Kijiwe Athuman ameiambia Mwananchi kuwa waligundua ukubwa wa tatizo baada ya mtoto kufanyiwa kipimo cha CT Scan, ambacho kilisaidia madaktari kubaini chanzo cha uvimbe na kuamua kufanya upasuaji.
"Tunawashukuru sana madaktari na Serikali kwa kutuletea huduma hii karibu. Hatukuwa na uwezo wa kufuata matibabu ya aina hii mbali na nyumbani. Leo tunaondoka na matumaini makubwa kuhusu afya ya mtoto wetu," amesema.
Naye mama wa mtoto huyo, Mwanakombo Said amesema familia yao imepata faraja baada ya mtoto kufanyiwa upasuaji huo bila gharama.
"Ninaishukuru Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha mwanangu amepata matibabu ya bure. Tunaamini sasa atapona na kurejea katika maisha yake ya kawaida," amesema.
Wazazi hao wamesema wana matumaini kuwa baada ya kupona kikamilifu, mtoto wao ataendelea na ukuaji wake wa kawaida pamoja na masomo bila changamoto iliyokuwa ikisababishwa na uvimbe huo.
Kambi ya madaktari bingwa inaendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, kwa lengo la kutoa huduma za upasuaji na matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa wenye magonjwa mbalimbali, sambamba na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya nchini kupitia ushirikiano kati ya Wizara ya Afya, ECSA HC na KIDS OR.