Matumizi hatari ya simu

Dar es Salaam. Simu za mkononi ni nyenzo muhimu katika kurahisisha mawasiliano, lakini matumizi yasiyo sahihi ya simu hizo yanaweza kuleta athari kwa mtumiaji.

Kwa mujibu wa watalamu kupitia utafiti, mionzi aina ya `ultra violate’ iliyopo kwenye simu inaweza kumletea athari mtumiaji endapo ataitumia au kuitunza kwa njia isiyokuwa sahihi.

Akizungumza na Mwananchi, Dk Annely Godable alisema nguvu ya mionzi inayotokea wakati simu inapokelewa ni kubwa hivyo si sahihi kuipokea ikiwa sikioni.

Dk Godable ambaye ni miongoni mwa wanasayansi wa Afrika Mashariki waliofanya utafiti kuhusu matumizi ya simu kupitia taasisi ya `Wema Ministry Association’, anaonya kuhusu athari za mionzi mwilini pale simu inapokuwa sikioni, kulala nayo kitandani, kuitumia ikiwa kwenye chaji, kuiweka kifuani, kuweka kwenye mfuko wa nguo, kuishikilia simu kwa kutumia bega wakati ukiendelea kuzungumza.

Matumizi mengine yasiyo sahihi ni kugeuza simu na kusikilizia upande wa spika, kuiweka sikioni muda wote kama wafanyavyo waendesha bodaboda kwa kuibana kwenye helmeti, kusikiliza muziki wa kwenye simu kwa muda mrefu kwa kutumia vifaa vya kusikilizia (hearphones) na kutumia simu jirani na vifaa vya umeme au moto.

‘‘Ikitokea simu inatumika isivyo sahihi mionzi hiyo itaingia kwenye mwili na mtumiaji na upo uwezekano wa kumsababishia kupata saratani ya ubongo, tezi dume, kuharibu uzalishaji wa mbegu za kiume, kuathiri kiumbe kilichopo tumboni kwa mjamzito, kupunguza nguvu za kiume na kumuondolea mwanamke hamu ya tendo la ndoa,’’ alisema.

Kana kwamba hiyo haitoshi simu isipotumika kwa usahihi humpunguzia mtu uwezo wa kufanya kazi, kusababisha ajali ikiwa dereva ataitumia wakati anaendesha chombo cha moto na kusababisha mlipuko endapo itatumika ikiwa kwenye chaji au mtu anapolala nayo kitandani.


Matumizi sahihi ya simu

Akizungumza jinsi gani ya kukaa na simu, Dk Godable anasema:

“Simu inatakiwa iwe pembeni ikiita uipokee, zile sekunde za kuitoa mkononi kwenda sikioni uzivute kidogo ili kuruhusu ile nguvu ya mionzi kupita.

“Sio simu muda wote ipo sikioni, hata ikiita inapokelewa ikiwa huko, hii ni hatari kwa afya, nguvu ya mara ya kwanza unapopokea ni hatari,” anasisitiza.

Daktari huyo anawazungumzia waendesha bodaboda kwa kusema:

“Wanaweza wasifahamu lakini ndio wanaofanya sana hivi. Muda wote simu ameibana sikioni ikiita anaipokea hapo hapo, ile nguvu ya mionzi moja kwa moja inaingia mwilini na inaweza kuleta athari za kiafya ikiwamo kupata saratani ya ubongo.”

Hata hivyo, anasema madhara hayaonekani ndani ya muda mfupi, inaweza kuchukua hata miaka saba lakini taratibu wanajiumiza, kwa mujibu wa mtaalaamu huyo.

Akichangia mjadala huo, z Abdala Kondo ambaye ni dereva wa bodaboda alisema hakuwahi kufahamu kwamba kuna madhara anayoweza kuyapata kwa kutembea na simu ikiwa sikioni.

“Kwa kweli sifahamu, binafsi nilikuwa naona ni urahisi nikiwa barabarani kutoa simu mfukoni inaweza kunisababishia ajali, hivyo ninapoiweka sikioni kwanza nina uhakika wa kuisikia ikiita na haiwezi kupotea kwa kuwa inajibana kwenye helmeti,” alisema Kondo.


Kulala na simu

Dk Godable vilevile, anafananua kuhusu tabia ya kulala na simu kitandani, akisema unapolala nayo unaivuta mionzi iliyopo ndani ya simu kwa kuwa na yenyewe inapumua.

“Kuna tatizo la Watanzania wengi kulala na simu, haya si matumizi sahihi ya kifaa hicho. Mwenyewe unaweza kuona unaiweka katika usalama zaidi kumbe unajiua, ukilala nayo ujue unairuhusu ile mionzi iingie mwilini,” alieleza Dk Godable.

Kuhusu kugeuza simu na kusikilizia upande wa spika, daktari huyo anaonya: “Usigeuze simu na kuweka spika upande wa sikio. Kama simu yako ina shida ya spika ni vyema ukatengeneza lakini sio kutumia kwa mtindo huo,” alitahadharisha Dk Godable.

Watu mbalimbali walizunguma na Mwananchi hawakusita kueleza namna wasivyojua matumizi sahihi ya simu.

Mary Gerald, mkazi wa Kijitonyama jijini Dar es Salaam, alisema hakuwa akifahamu kuwa kugeuza simu kunaweza kuwa na madhara yoyote kiafya.

“Kama kweli kuna madhara basi yatatukuta wengi, maana hivi visimu vidogo mara nyingi vinaharibika spika, hivyo ili uweze kuzungumza usikike au kumsikia anayeongea tunaona urahisi ni kugeuza na hilo tunafanya wengi huku mitaani,” alisema Mary.

Dk Godable pia aligusia kuhusu wanaozungumza na simu wakiwa wameibana kwenye bega huku wakiendelea na shughuli nyingine kuwa hayo si matumizi sahihi.

“Kama unazungumza na simu fanya hivyo kwa muda mfupi umalize, ukijiona una shughuli nyingine ni heri usitishe kwanza unachokifanya au utumie kifaa cha kusikiliza masikioni na si kushikilia simu kwa bega, hapo unarahisisha usambaaji wa mionzi. Kama unataka kuitumia kusikiliza muziki kwa muda mrefu, bora uweke spika na si kutumia `earphones’ kwa saa nyingi,” alisema mtaalam huyo.