Matumizi mabaya ya viuatilifu yanavyosababisha mimba kutoka, saratani
Muktasari:
Saratani ya ngozi, msongo wa mawazo, matatizo ya mfumo wa Neva na mimba kutoka ni miongoni mwa madhara yaliyotajwa kuchagizwa na matumizi mabaya ya viuatilifu.
Moshi. Kama hauzingati kanuni na taratibu za matumizi sahihi ya viuatilifu katika mazao, upo hatarini kukabiliwa na magonjwa lukuki, ikiwemo msongo wa mawazo, matatizo ya mfumo wa Neva na mimba kutoka.
Kwa taarifa yako, haupaswi kutumia viuatilifu hivyo bila kuwa na vifaa maalum wakati wa utumiaji. Pia unapaswa kuzingatia kiwango maalum kama inavyoelekezwa na wataalamu.
Hayo yameelezwa leo Jumatatu, Januari 15, 2024 wilayani Moshi na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Profesa Joseph Ndunguru alipohitimisha mafunzo ya siku yano ya wakaguzi wa viutalivu juu ya sheria, kanuni na taratibu za matumizi na biashara za bidhaa hizo.
Lengo la mafunzo hayo, amesema ni kuwaboresha wakaguzi wa taasisi hiyo ili wawasaidie wakulima kwa kuwa na usahihi wa viuatilifu vyenye ubora.
"Tunawapa jukumu la kwenda kuimarisha kaguzi hasa mipakani juu ya mazao, viuatilifu, pia wakulima wakapate elimu juu ya matumizi na biashara ya dawa mbalimbali za visumbufu mimea,” amesema.
Kaimu Meneja wa TPHPA Kanda ya kusini, Lilian Muyaga amesema wakulima wanaotumia viuatilifu bila kuwa na elimu ya upigaji kwenye mazao yao na vifaa vya kujikinga, wapo hatarini kukumbwa na madhara hayo ya kiafya.
"Wakulima wanatakiwa kuzingatia kiuatilifu sahihi na majira ya upigaji kutokana na maelekezo ya wataalamu na wahakikishe wanachukua tahadhari ya kujikinga kwa kuvaa vifaa maalum kama glovu na barakoa," amesema.
Awali, Mratibu wa Miradi ya Kilimo wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) nchini Tanzania, Diomedes Kalisa amesema matumizi makubwa ya viuatilifu nchini yanahatarisha usalama wa afya za watumiaji.
Ameitaka Serikali kuchukua tahadhari ya mwenendo wa kilimo kinachofanywa na wananchi, kadhalika iwahamasishe wapunguze matumizi ya kemikali.
"Matumizi ya kemikali mbali na athari za kiafya yanaathiri uchumi pia. Kwa sababu baadhi ya mazao yatakosa soko la kimataifa,” amesema.