Matumizi ya gesi kwenye bajaji suluhu kupanda kwa nauli

Muktasari:

  • “Ninatumia si chini ya Sh6,000 kila siku kutoka na kwenda kazini. Hizi ni fedha nyingi ukipiga hesabu ya mwezi na mwaka mzima,” anasema Mwalimu Agnes Paschal, anayefundisha shule ya msingi jijini Dar es Salaam.


“Ninatumia si chini ya Sh6,000 kila siku kutoka na kwenda kazini. Hizi ni fedha nyingi ukipiga hesabu ya mwezi na mwaka mzima,” anasema Mwalimu Agnes Paschal, anayefundisha shule ya msingi jijini Dar es Salaam.

Mwalimu huyo anayeishi Mji wa Mapinga, nje ya Jiji la Dar es Salaam anasema hulazimika kupanda bajaji kutoka nyumbani kwake mpaka kituo cha daladala Bunju ili apate magari yanayoenda Ubungo ambako huchukua linalopita Tandale anakofundisha.

“Ni mzunguko mrefu wa kila siku. Kutoka Bunju mpaka kwangu, napanda bajaji zinazoenda Udindivu. Barabara ni mbovu na hakuna daladala inayoenda huko, hivyo mbadala uliopo ni bajaji au bodaboda. Serikali itakapojenga barabara labda gharama za usafiri zitapungua,” anasema Agnes.

Kila mwezi, mwalimu huyu hutumia zaidi ya Sh130,000 kwenye usafiri. Yeye ni mmoja tu kati ya mamilioni ya Watanzania wanaoishi na kufanya kazi jijini Dar es Salaam wakitumia mamilioni kwenye usafiri wa umma ambao nauli yake inazidi kupanda kadiri bei ya mafuta na vipuri inavyobadilika duniani.

Gesi kwenye bajaji

Umuhimu wa kutumia nishati mbadala kwenye usafiri wa umma unatokana na ukweli kwamba gharama za mafuta hupanda mara kwa mara, huku wakati mwingine yakiadimika, huku moshi wake ukichafua mazingira.

Kutokana na uhitaji wake, katika baadhi ya maeneo bajaji hizi hubeba watu wengi kuliko uwezo wake. Badala ya kubeba abiria watatu kama inavyotakiwa, zipo zinazokuwa nao wawili wanaobanana mbele aliko dereva ukiacha wanaokaa nyuma, hivyo kuhatarisha usalama wao.

“Gharama za uendeshaji ni kubwa. Usipofanya hivi hupati kitu kabisa. Fikiria kwa bei ya mafuta iliyopo sasa hivi halafu ubebe abiria watatu kutoka hapa mpaka Kwa Mkwelemba utapata kitu kweli?” anasema Hussein Abdallah, dereva bajaji inayofanya safari zake kutoka Mo++mbasa kwenda Kwa Mkwelemba jijini hapa.

Kutokana na changamoto nyingi zilizopo kwenye usafiri wa umma, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Punjab cha Pakistan ilifanya utafiti unaoitwa ‘Exploring the potential of compressed natural gas as a sustainable fuel for rickshaw: A case of study of Dar es Salaam.’

Ripoti ya utafiti huo unaoangalia faida za kutumia gesi asilia kwenye bajaji inaonyesha iwapo bajaji 50,000 tu zitatumia gesi basi zitaleta faida nyingi za kiuchumi na kimazingira jijini Dar es Salaam, kwani usafiri huo unategemewa katika maeneo mengi ambako daladala hazifiki, hasa yanakoanzishwa makazi mapya.

Tanzania inayo hazina ya futi trilioni 57.5 za gesi asilia iliyothibitishwa ambayo kwa kiasi kikubwa hutumika kuzalisha umeme, licha ya ukweli kwamba inaweza kupunguza gharama kubwa za usafiri wa umma zinazochangiwa na foleni ndefu, hivyo kuleta hasara ya mabilioni.

Takwimu zinaonyesha Tanzania ina takriban magari milioni mbili na zaidi ya bajaji 500,000 zilizosajiliwa mpaka mwaka 2019, lakini mpaka Machi 2022 ni magari 700 tu yalikuwa na mfumo wa gesi asilia huku kukiwa na kituo kimoja cha kujazia gesi hiyo.

Asilimia 80 ya magari yaliyosajiliwa nchini yanapatikana jijini Dar es Salaam ambako taarifa za Benki ya Dunia zinaonyesha mwaka 2021 kulikuwa na zaidi ya wakazi milioni saba, wengi wakitumia usafiri wa umma.

“Tulifanya utafiti kuhusu bajaji kwa sababu ndio usafiri wa uhakika kwa watu wengi baada ya kushuka kituo cha mwisho cha daladala wakiutumia kutoka na kurudi nyumbani kabla na baada ya shughuli zao za kila siku,” inasomeka sehemu ya utafiti huo uliofanyika katika njia ya kutoka Gerezani kwenda Gongolamboto, Mbezi Mwisho na Mbagala Rangitatu.


Faida bajaji kutumia gesi

Iwapo bajaji 50 zitatumia gesi, utafiti huo unasema matumizi yake yatafika zaidi ya tani 92,662.5 kwa mwaka zenye thamani ya dola 62.083 milioni za Marekani, sawa na Sh142.79 bilioni kwa bei ya Sh1,550 kwa kilo moja. Bajaji hizo pia, utafiti unasema zitapunguza uchafuzi wa mazingira kwa asilimia 33.

Kwa sasa, dunia inapambana kuhakikisha inaachana na magari yanayotumia mafuta. Mkakati uliowekwa ni kuacha kuyatengeneza ifikapo mwaka 2050. Vyombo vya usafiri wa barabarani, taarifa zinaonyesha vinatumia asilimia 40 ya mafuta yote yanayotumika duniani na kuzalisha kati ya asilimia 10 mpaka 25 ya hewa ya ukaa.

“Kati ya mibadala inayopendekezwa ni gesi asilia, kwani ina kiasi kidogo cha hewa ya ukaa, inapatikana kwa kiwango cha kutosha na gharama yake iko chini,” unasema utafiti huo uliochapishwa kwenye Jarida la Journal of Natural Gas Science and Engineering hivi karibuni.

Watafiti hao wanapendekeza mambo matatu kuzifanya bajaji zitumie gesi asilia na kuongeza manufaa ya nishati hiyo nchini. Wanasema zinunuliwe bajaji zenye mfumo wa gesi asilia, au mfumo wa gesi asilia ununuliwe tofauti na bajaji ya kawaida, au mmiliki wa bajaji ya kawaida anunue injini ya gesi.

Hayo yakifanyika, wanasema Serikali ijenge vituo vya kujaza gesi katika maeneo rafiki ili kusiwe na gharama za ziada kwa dereva anayehitaji huduma.

Watanzania wataka gesi

Gerutu Bosinge, mmoja wa watafiti na msimamizi wa karakana ya kufunga mifumo ya gesi ya DIT, anasema utafiti huo waliuanza mwaka 2020 na kuukamilisha mwaka jana na kugundua kwamba Watanzania wengi wako tayari kubadili nishati ya vyombo vyao vya moto.

“Leo (Jumanne) nimepokea wateja watano wa bajaji wanaotaka kufunga mfumo wa gesi. Tunapokea maombi mengi pia kutoka mikoani kuanzia Dodoma, Mbeya, Morogoro mpaka Arusha. Kuna mmoja wa Morogoro aliniomba tumfungie mfumo wa gesi ili gesi ikianza kupatikana mkoani imkute tayari anao,” anasema Gerutu.

Tayari karakarani ya DIT imekamilisha utaratibu wa kuanza kufunga mfumo huo kwenye bajaji na Gerutu anasema mpaka wiki ijayo huduma hiyo inayogharimu kati ya Sh500,000 mpaka Sh800,000 itaanza kupatikana, kwani vifaa muhimu vimeshawasili ila bado vipo bandarini.

Mpaka mwaka 2018, takwimu zinaonyesha kulikuwa na magari milioni 27.395 yanayotumia gesi asilia duniani na idadi inaendelea kuongezeka.

Katika miji ya Mexico City, New Delhi, Mumbai, Rio de Janeiro, Pakistan, Iran na Beijing daladala zao, bajaji na usafiri mwingine wa umma unatumia gesi asilia.


Paet wako tayari kushirikiana

Ingawa ni sehemu ndogo sana ya kiasi inachozalisha, Kampuni ya Pan African Energy (Paet) imesema ipo tayari kushirikiana na wadau kujenga miundombinu muhimu ya kujaza gesi kwenye magari.

Utayari huo umebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Paet, Andrew Hannah anayesema Tanzania ina magari mengi, lakini yanayotumia gesi ni machache kutokana na kukosekana kwa vituo vya kujazia nishati hiyo.

“Iwapo vitaongezeka, watumiaji wataongezeka pia. Tupo tayari kushirikiana na wadau wengine kujenga vituo vya kujaza gesi asilia kwenye magari,” anasema Hanna. Mkurugenzi huyo amefafanua kwamba wameanza kuzungumza na baadhi ya wamiliki wa vituo nchini kuona uwezekano wa kushirikiana kufanikisha hilo.

Hata hivyo, amekumbusha kwamba kufanikisha mradi wowote mkubwa inahitajika utayari wa Serikali utakaohusisha kuhamasisha uingizaji wa magari yanayotumia nishati hiyo ili kuongeza idadi ya wateja.

Taarifa kutoka mataifa tofauti yaliyopiga hatua zaidi katika matumizi ya gesi zinaonyesha ujenzi wa kituo kikubwa cha kujaza nishati hiyo kwenye magari unagharimu kati ya Sh400 milioni mpaka Sh500 milioni na kituo kidogo ni kati ya Sh80 milioni mpaka Sh100 milioni.

“Uzuri ni kwamba vituo hivi vikishajengwa, vinadumu kwa muda mrefu bila kuhitaji matengenezo. Kile cha Ubungo kilijengwa mwaka 2009 lakini mpaka leo kinaendelea kutoa huduma na hakijawahi kufanyiwa marekebisho makubwa,” anasema Gurutu.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo cha Biashara (CBE), Dk Dickson Pastory anasema kuna vitu muhimu vya kufanya vitakavyosaidia kuongeza matumizi ya gesi kwenye vyombo vya usafiri.

“Kwanza ni kutoa elimu kwa wananchi wengi waelewe hilo, halafu gharama za kufunga mfumo wa gesi kwenye gari au bajaji zipunguzwe. Kwa sasa kufunga huo mfumo kwenye gari ni takriban Sh2 milioni, wamiliki wengi hawamudu hiyo bei. Gharama zikipunguzwa wengi watabadili mfumo hivyo kutakuwa na wateja wengi watakaoshawishi kujenga vituo maeneo mengi zaidi,” anasema mchumi huyo mwandamizi.