Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mauaji ya mtoto hifadhini yawaibua Tanapa

Ngatipa Parmao (17) anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na askari wa wanyamapori katika Hifadhi ya Mkomazi wilayani Mwanga.

Muktasari:

Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) limeeleza hatua inazochukua kutokana na mauaji ya Ntaipa Parmao (17) anayedaiwa kupigwa risasi na askari wa wanyamapori ndani ya Hifadhi ya Mkomazi wilayani Mwanga.

Dar es Salaam. Wakati wazazi wa Ngatipa Parmao (17) anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na askari wa wanyamapori katika Hifadhi ya Mkomazi wilayani Mwanga, wakiomba haki itendeke kwa waliohusika na unyama huo, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) limetangaza kuanza uchunguzi wa kina.

Ngatipa, ambaye alidaiwa kupigwa risasi katika hifadhi hiyo kutokana na madai ya kuingiza ng’ombe, mazishi yake yamefanyika Jumatatu ya Julai 11, 2022 katika Kijiji cha Pangaroo wilayani Mwanga.

Hata hivyo, mzazi wa mtoto huyo, amekana kuwa ng’ombe zake 54 ziliingia hifadhini kwa kuwa zilikuwa pembezoni umbali wa kilomita mbili kabla ya kufikia mpaka wa hifadhi hiyo.

Pia, amesema kuwa alilipa faini ya Sh1.3 milioni ndipo akakabidhiwa mifugo hiyo ambayo ilikuwa ikishikiliwa hifadhini hapo.

Mwili wa Ngatipa Parmao (17) mkazi wa kijiji cha Pangaroo anayedaiwa kuuawa na askari wanyamapori ukiingizwa kaburini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatano, Julai 13, 2022 na Idara ya Uhusiano ya Tanapa, imesema kuwa uchunguzi huo unafanyika ikiwa ni sehemu ya kutafuta ufumbuzi na kurejesha mahusiano mema na wananchi.

Pia, Tanapa limesema kuwa litaendelea kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi waishio pembezoni mwa hifadhi mbalimbali nchini.

“Tunatoa pole kwa familia ya Lukumay na tunaahidi kuendelea kutoa elimu kupitia mradi wa ujirani mwema kuhusiana na sheria za Hifadhi za Taifa na taratibu za kufuatwa kwa wanaokiuka ikiwa ni pamoja na kufanya shughuli za kijamii ndani ya hifadhi,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.


Hali ilivyodaiwa kuwa

Ngatipa anadaiwa kupigwa risasi Julai 6, 2022 na askari wa Hifadhi ya Mkomazi wakati anachunga ng’ombe pembezoni mwa hifadhi hiyo.

Mara baada ya kupigwa risasi, Ngatipa alipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Same kwa matibabu ya awali kisha akahamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) ambako alifariki dunia Julai 8, 2022.

Mwili wake ulifanyiwa uchunguzi wa sababu ya kifo (postmortem) na kubainika kuwa na matundu mawili yanayodaiwa kuwa ya risasi katika sehemu ya mkono upande wa kulia na tumboni.

Mazishi yake yamehudhuriwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali akiwemo mkuu wa wilaya hiyo, Abdallah Mwaipaya.

Mwaipaya aliiomba familia hiyo kuwa watulivu wakati Jeshi la Polisi linaendelea kuchunguza tukio hilo na kuwa hadi sasa linawashikilia askari watatu kwa tuhuma hizo.

“Niwape pole familia kwa hili lililotokea na sisi Serikali tumekuwa nanyi tangu tukio hili limetokea, nashukuru kwa uvumilivu wenu ambao umeonyesha na sisi tuko pamoja nanyi,” alisema.


Kauli ya baba wa Ngatipa

Muda mfupi kabla ya mazishi, baba mzazi wa Ngatipa, Marius Parmao amemwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati tukio hilo akisema mwanaye aliuawa kwa makusudi.

Pia wazazi hao wamedai kuna dalili za kufanyika kwa mchezo mchafu wa kuharibu ushahidi baada ya vipimo vya awali kabla ya upasuaji kuonyesha kulikuwa na risasi ndani ya mwili, lakini baadaye ikaelezwa haijakutwa.

Alidai kuwa baada ya kijana wake kupigwa risasi alipekwa hospitali ya Same ambako ilibainika kulikuwa na risasi ndani ya mwili.

“Tulikuwa na OCD (mkuu wa polisi wa wilaya) na aliagiza daktari amfanyie mgonjwa vipimo vya uchunguzi, daktari alifanya hivyo na kutuhakikishia kuna risasi. Akatwambia ili upasuaji ufanyike tunapaswa kulipa Sh140,000 na tukafanya hivyo ili mtoto wangu aokolewe maisha,” alisema Parmao kwa lugha ya Kimaasai ikitafsiriwa na Lameck Kipuyo kwa Kiswahili.

Mzee huyo akizungumza taratibu alisema: “baada ya kuhakikisha gharama zote zimelipwa OCD aliondoka na mtuhumiwa kwenda naye kituoni Mwanga, lakini cha kushangaza baada ya upasuaji kufanyika tukaambiwa risasi haionekani, nilipoambiwa hivyo niliumia sana.”

“Kutokana na hali ya mtoto kuendelea kuwa mbaya tuliomba tumpeleke KCMC kwa matibabu zaidi, lakini kesho yake mtoto wetu alipoteza maisha,” alisema Mzee huyo mwenye wake watatu na watoto 18.

Alidai kuwa kilichofanywa na uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Same si sawa maana hizi ni mbinu za kutuzungusha ili mtoto wetu asipate haki, kutokana na hii naiomba Serikali isimamie haki maana vipimo vilifanyika na tukahakikishiwa risasi ipo ndani.”

Alipotafutwa Mganga mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro (RMO) Jairy Khanga kuhusu tuhuma za hospitali ya wilaya ya Same, alisema amepokea taarifa hiyo na anafuatilia kuchunguza ukweli wake.

Parmao alidai Hospitali ya KCMC walipomfanyia postmoterm walibaini kuna matundu mawili ambayo moja lilikuwa upande wa kulia na lingine sehemu ya tumboni.

Hata hivyo, alidai kuwa kinachoumiza zaidi mwanaye hakukutwa na ng’ombe hifadhini, walikuwa nje ya hifadhi kwani kutoka eneo walilopokuwa mpaka hifadhini ni kilomita mbili.

“Baada ya ng’ombe 54 aliokuwa nazo mwanangu kukamatwa nilitakiwa nilipe Sh1.3 milioni na nilifanya hivyo wakati mtoto wangu akiwa hospitali, ndipo nikarejeshewa mifugo yangu,” alisema.