Mauzo ya Kahawa yapaa kwa asilimia 12

Mkurugenzi wa TCB, Primus Kimaryo

Moshi. Mauzo ya kahawa katika msimu wa 2022/2023 yameongezeka kwa asilimia 12 na kufikia Sh548.4 bilioni kutoka Sh489.5 bilioni msimu uliopita.

Ukiachana na mauzo hayo pia uzalishaji umeongezeka kutoka tani 66,605 msimu uliongezeka hadi tani 81,498

 Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Bodi ya kahawa Tanzania (TCB), Primus Kimaryo wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusiana na hali ya uzalishaji na bei ya kahawa kwa msimu wa 2022/2023.

Amesema kiwango kikubwa cha uzalishaji kilichowahi kufikiwa kwa miaka ya nyuma kilikuwa ni Tani 72,000 msimu wa mwaka 2020/2021 na kwamba malengo ni kufikia uzalishaji wa tani 300,000 ifikapo msimu wa mwaka 2025/2026.

“Tumefunga msimu kwa mafanikio makubwa, tulitarajia msimu wa 2022/2023 tungepata jumla ya Tani 70,000, lakini kutokana na hali nzuri ya hewa pamoja na juhudi za Serikali katika utoaji wa pembejeo na miche ya kahawa bure kwa wakulima,”amesema.

Aidha amesema mafanikio hayo yametokana na jitihada mbalimbali zilizofanywa ikiwemo kutoa miche bora ya kahawa ambapo mpaka sasa kwa msimu huu wameweza kutoa miche milioni 9.3 na wanatarajia miche milioni 11 itatolewa kipindi cha vuli cha Septemba.

Akizungumzia bei amesema mkulima wa Robusta amepata Sh2,000 kwa kilo moja ya kahawa ya maganda kupitia mnada, huku kwa upande wa Arabika akipata Sh3,000 na kwamba bado kuna fursa ya kuongeza bei kwa kuongeza ubora wa kahawa tunayozalisha.

“Ubora wa kahawa una fursa kubwa ya kumuongezea mkulima kipato chake, tunaendelea kutoa elimu kwa wakulima kuchakata kahawa kupitia mitambo ya kuchakata ya pamoja (CPU) kwa ubora mzuri na kufuata zile taratibu zinazopaswa kufuatwa ili kuweza kupata bei nzuri”amesema.

Mtafiti upande wa usambazaji wa teknolojia na mafunzo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kahawa nchini (TaCRI), Dk Jeremiah Magesa amesema moja ya mikakati ya kuongeza uzalishaji wa kahawa nchini ni kuongea uzalishaji wa miche bora ya kahawa hadi kufikia milioni 20 kwa mwaka.

“Pia tunahamasisha matumizi sahihi ya viuatilifu na ili mkulima aweze kudhibiti hili na kupata mavuno mazuri ni lazima afuate kanuni bora za kilimo cha kahawa,”amesema.