Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mawimbi yapasua mitumbwi 212, mingine 38 yaharibiwa Ziwa Victoria

Baadhi ya mitumbwi iliyoharibiwa na mawimbi pamoja na upepo ndani ya ziwa Victoria katika mwalo wa Busekela wilayani Musoma

Muktasari:

  • Jumla ya mitumbwi 212 imepasuliwa pasuliwa huku 38 ikiharibika kabisa baada ya kuibuka kwa upepo mkali uliosababisha mawimbi kuwa makubwa na makali ndani ya Ziwa Victoria katika mialo ya Busekela na Buira wilayani Musoma.

Musoma. Jumla ya mitumbwi 212 imepasuka baada ya kujibamiza kutokana na mawimbi, huku 38 ikiharibika kabisa baada ya kuibuka kwa upepo mkali ndani ya Ziwa Victoria katika mialo ya Busekela na Buira wilayani Musoma.

Tukio hilo limetokea Machi 20, 2023 saa 11 jioni wakati wavuvi wakijiandaa kuingia ziwani kwa ajili ya kufanya shughuli zao kama ilivyo kawaida.

Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi, Diwani wa Kata ya Bukumi yalipotokea maafa hayo, Munubi Musa amesema kuwa mbali na mitumbwi hiyo. Pia nyavu zinazotumiwa na wavuvi hao pia zimeharibiwa.

"Hadi sasa bado hatujajua thamani halisi ya mitumbwi iliyopasuka na ile iliyoharibika kabisa ambayo haiwezi kutengenezwa na kutumika tena. Pia nyavu zipo ambazo zimeharibika kabisa na haziwezi kutumika lakini pia zipo ambazo zimechanika chanika," amesema.

Amesema kuwa tayari wametoa taarifa uongozi wa wilaya kwa ajili ya hatua zaidi na kufafanua kuwa wakati wa tukio mitimbwi hiyo ilikuwa imetia nanga kwenye maji mafupi ziwani hapo.

"Mawimbi yalikuwa yanapiga mitumbwi hadi inakata kamba au inang'oa nanga kabisa kisha inasombwa kuja nchi kavu wakati huo inajibamiza na kupasuka pasuka. Kwa hiyo ipo mingine ilihimili, ikiharibika kiasi na mingine ndiyo imeharibika kabisa haiwezi kutengenezeka tena," amesema.

Diwani huyo ameiomba Serikali kufika katika eneo ili kuona namna ya kuwasaidia wavuvi hao ambao amesema kuwa baadhi yao walichukua mikopo kwenye taasisi za kifedha kwaajili ya kuendeleza biashara zao.

"Hapa kuna watu wana mikopo na hawajui wafanye nini sasa ni vema serikali ikaja ikaona inawasaidiaje tayari jana tulipeleka taarifa wilayani kuhusu tukio hili sasa tunasubiri bado hatujajua hatua zipi zitachukuliwa," amesema.

Amesema matukio kama hayo yamekuwa yakitokea kila mwaka lakini tukio la kipindi hiki limeleta madhara makubwa kwani mara nyingi mitumbwi inayoharibika ni kati ya miwili hadi mitano.

"Tunamshukuru Mungu wakati tukio linatokea wavuvi walikuwa hawajapanda ziwani nadhani yangetokea maafa makubwa zaidi kwani upepo ulikuwa mkali sana na mawimbi makubwa hatujawahi kuona," amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Halfan Haule amesema hajapata taarifa juu ya tukio hilo huku akiahidi kufuatilia na kutoa taarifa baadaye.

"Niko nje ya Musoma ngoja niwasiliane na walioko huko kisha nitakupa taarifa," amesema.