Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maziko ya Mkono kujulikana wiki ijayo

Aliyewahi kuwa Mbunge wa Butiama mkoani Mara, Nimrod Mkono enzi za uhai wake. Picha na mtandao

Muktasari:

  • Ratiba ya kuwasili nchini mwili wa aliyewahi kuwa Mbunge wa Butiama mkoani Mara, Nimrod Mkono na maziko yake yanayotarajiwa kufanyika nyumbani kwake Butiana itajulikana wiki ijayo.

Mwanza. Ratiba ya kuwasili nchini mwili wa aliyewahi kuwa Mbunge wa Butiama mkoani Mara, Nimrod Mkono na maziko yake yanayotarajiwa kufanyika nyumbani kwake Butiama, itajulikana wiki ijayo.

 Mkono aliyekuwa akitibiwa nchini Marekani tangu mwaka 2018, alifikwa na mauti Aprili 18, mwaka huu ambapo mdogo wake, Zadock Mkono ameujulisha umma kuwa; mwili wa mwanasheria na mwanasiasa huyo, utarejeshwa nchini kwa maziko yanayotarajiwa kufanyika nyumbani kwake Kijiji cha Kigoro Wilaya ya Butiama mkoani Mara.

Chifu wa Wazanaki, Joseph Wanzagi ameiambia Mwananchi Digital kuwa maandalizi kufanikisha maziko ya mbunge huyo wa zamani, yanaendelea nyumbani kwake Butiama huku vikao kadhaa vikiendelea maeneo mbalimbali ikiwemo jijini Dar es Salaam.

“Niko nyumbani Butiama, hivyo sina taarifa za vikao vinavyoendelea jijini Dar es Salaam; wasiliana na Mzee Joseph Butiku anayeongoza kamati maalum iliyoundwa au Katibu wake, Wilson Mahera. Hata mzee Stephen Wasira pia ni mjumbe wa kamati hiyo anaweza kukusaidia kujua kinachoendelea,” amesema Chifu Wanzagi

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Mahera ambaye pia ni mzaliwa wa Wilaya ya Butiama kama alivyo marehemu Mkono alisema; ‘’Hadi sasa taarifa rasmi za lini mwili utawasili nchini hazijafahamika kwa sababu bado taratibu zinaendelea kukamilishwa kule Marekani,”

Alisema hadi kufikia wiki ijayo, taarifa ya siku rasmi ambapo mwili wa Mkono kuwasili nchini zitafahamika na umma utajulishwa.

“Lakini muhimu ni kwamba ‘definitely’ mwili utaletwa kwaajili ya maziko yanayo tarajiwa kufanyika nyumbani Butiama,’’ amesema Mahera

Marehemu Mkono aliyezaliwa Agosti 18, 1948, eneo la Busegwe Mkoani Mara, alikuwa mwanasheria na mwasiasa maarufu wakati wa uhai wake.

Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu, Zadock Mkono, mwanasiasa huyo alikuwa  akisumbuliwa na ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu (Alzheimer) na amekuwa akitibiwa nchini Marekani kwa kipindi cha miaka minne iliyopita.

Kijiji chake wamlilia

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kigori ambako ndiko yalipo makazi ya marehemu Mkono, Selemani Muhaya amesema kifo cha mbunge huyo wa zamani ni pigo kwa kijiji hicho, Wilaya ya Butiama, Mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla kutokana mchango wake kwa jamii.

"Kwetu wanakijiji cha Kigori, Kata ya Busegwe na Wilaya ya Butiama kwa ujumla Mkono hakuwa tu kiongozi wetu wa kisiasa, bali alikuwa nguzo muhimu ya kuegemea katika shughuli za maendeleo. Alifanya zaidi ya tulichokitarajia kutoka kwake," alisema Muhaya

Alitaja kumbukumbu nzuri zilizoachwa na marehemu Mkono kuwa ni utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za afya, maji, elimu na miundombinu ya barabara kwa kutumia fedha zake binafsi, umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi.

"Watu wengi, kuanzia Wilaya ya Butiama na maeneo kadhaa nchini wanamzungumzia Mkono kwa kutaja miradi ya maendeleo; lakini sisi tulikuwa tunamwangalia kwa jicho tofauti. Kwetu alikuwa mhimili siyo tu wa maendeleo yetu, bali pia umoja na mshikamano wetu hapa kijijini," alisema Muhaya

Amesema kwa miaka 15 ya ubunge wa Mkono, Kijiji cha Kigori hakijawahi kuwa na mgogoro ulioshindikana kumalizwa kwa njia ya majadiliano na maelewano ya kindugu.

Alisema kutokana na nafasi ya marehemu katika maendeleo ya kijiji hicho wakati wa uhai wake, tayari uongozi wa kijiji umeitisha vikao kuunda kamati na kufungua daftari maalum la rambirambi katika ofisi ya Mtendaji wa kijiji huku wakisubiri taarifa rasmi ya lini mwili utawasili nchini.

‘’Nimeongea na Leah Mkono ambaye ni mtoto wa marehemu Mkono jana na amenihakikishia kwamba familia inakamilisha taratibu za kupata vibali vya kusafirisha mwili kutoa nchini Marekani. Sisi tuko hapa nyumbani kwake tukiendelea na taratibu za maandalizi ya maziko ikiwemo kufanya usafi wa mazingira,’’ amesema Muhaya

Miradi ya kukumbukwa

Kwa upande mwingine, Chifu Wanzagi amesema kifo cha Mkono siyo tu ni pigo kwa Wilaya ya Butiama, bali pia Taifa kwa ujumla kutokana na jinsi alivyokuwa akijitolea kwa hali na mali kusaidia jamii, hasa utekelezaji za miradi ya maendeleo.

"Kwa wana Butiama, Mkono alikuwa Mkono! Hakuwa na mbadala. Ametufanyia mengi ninayoamini yataishi kuwa kumbukumbu yake daima," alisema Chifu Wanzagi

Baadhi ya miradi ya maendeleo atakayokumbukwa nayo mwanasiasa huyo ni ujenzi wa Shule za Sekondari za Chifu Ihunyo, Chifu Wanzagi na Chifu Oswald Mang'ombe.

Miradi mingine ni ujenzi wa Hospitali ya Murangi na uchimbaji wa visima vya maji maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Butiama, kikiwema kisima kwa ajili ya familia ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.