Mazishi mwanafunzi anayedaiwa kufa kwa kipigo yashindikana, Polisi wataja sababu

Muktasari:

  • Maziko ya mwanafunzi Jonathan Makanyaga (6) yaliyokuwa yafanyike leo Machi 16, 2024 katika Kijiji cha Kimanganuni Chini, Kata ya Uru Kusini, Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro yameshindwa kufanyika licha ya taratibu zote za maziko kufanyika.

Moshi. Maziko ya mwanafunzi Jonathan Makanyaga (6) yaliyokuwa yafanyike leo Machi 16, 2024 katika Kijiji cha Kimanganuni Chini, Kata ya Uru Kusini,  Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro yameshindwa kufanyika licha ya taratibu zote za maziko kufanyika, ikiwemo kuchimbwa kwa kaburi, kutokana na kilichodaiwa kuwa mwili umezuiliwa kutokana na taratibu za kiuchunguzi kuendelea.

 Wakati hayo yakijiri leo, taarifa iliyotolewa jana Machi 15 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa  ilieleza kuwa, tayari mwili wa mwanafunzi huyo wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Mrupanga, umefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Hata hivyo, licha ya maandalizi kufanyika ikiwemo kuchimbwa kaburi na watu kukusanyika hadi leo jioni, maziko hayo hayakufanyika.

Akizungumzia sababu za kutozikwa mwili wa mwanafunzi huyo, Kamanda Maigwa amesema ni kutokana na mashaka yaliyoibuliwa na familia ya mwanafunzi huyo kuhusu kifo chake na taarifa kurushwa mitandaoni zikionyesha mama huyo akilalamika kuhusu sababu za kifo cha mwanaye.

"Hatukuhitaji kuingia kwenye malumbano, tumelazimika kuagiza mtaalamu (pathologist) kutoka Dar es Salaam waje wafanye uchunguzi kwa pamoja walinganishe, hicho kinachobishaniwa ili kuondoa mkanganyiko na tunafanya hivyo kujiridhisha ili kuondoa mashaka pande zote mbili," amesema.

"Ni kweli tulishaukabidhi mwili, lakini ulikuwa haujaondolewa KCMC, waliandika maelezo yote na tukakabidhi mwili lakini kulipoibuka malalamiko mitandaoni, ndipo tukaingilia kati kuiomba familia ili kuondoa mashaka, wavumilie tumlete huyo mtaalamu ili kuondoa hayo malalamiko,"

Mwanafunzi huyo, alifariki dunia Machi 10 mwaka huu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC  alikokuwa amelazwa kwa matibabu.

Mtoto, Jonathan Makanyaga anayedaiwa kufariki baada ya kuchapwa shuleni.

Inadaiwa kuw, Februari 28, mwaka huu akiwa na wenzake wawili walitandikwa viboko na mwalimu tarajali wa mafunzo ya ualimu (BTP),aliyekuwa akifundisha shuleni hapo kwa kuchelewa kushika namba asubuhi, hali iliyomsababishia majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake na kupelekea kutoka damu puani na mdomoni.

Inaelezwa kuwa, wenzake wawili aliokuwa nao wakati wanachapwa walijikinga na fimbo hizo kwa kutumia mabegi waliyokuwa wamebeba mgongoni na kwamba Jonathan (marehemu) alishindwa kujizuia na kuumizwa sehemu ya uti wa mgongo, mbavuni na sehemu ya mapajani na kisha kuangushwa chini.

Mpaka sasa, walimu tarajali wa mafunzo ya ualimu watano wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa mahojiano kwa kudaiwa kuhusika na kifo cha mwanafunzi huyo.

Aidha Kamanda Maigwa alieleza kuwa, uchunguzi wa tukio hilo umekamilika na tayari shauri limepelekwa ofisi ya Mashtaka(DPP) kwa ajili ya kulitolea maamuzi ya kisheria.

"Bado tunaendelea kuwashikilia walimu tarajali watano wa mafunzo ya ualimu kwa mohojiano baada ya kuripotiwa kwa tukio hili,” amesema.


 Hali ilivyokuwa msibani

Mamia ya waombolezaji waliofika kwenye mazishi ya mwanafunzi huyo, yaliyotarajiwa kufanyika leo machi 16,  walijikuta njiapanda baada ya mwili wa mwanafunzi huyo kushindwa kufikishwa nyumbani kwa taratibu za maziko.

Waombolezaji hao ambao walikuwa wamekaa kwenye makundi msibani hapo, walifika nyumbani hapo kuanzia asubuhi kwa ajili ya kushiriki maziko hayo ambayo hayakufanyika.

Hata hivyo, ilipofika saa 10:53 Mshereheshaji wa shughuli hiyo, Kalisti Mushi aliwataka waombolezaji kutulia kusikiliza tangazo kutoka kwenye familia kuhusu maziko hayo.

Mmoja wa wanafamilia aliyetambulishwa kwa jina moja la Urio, alisema familia kwa sasa hawana taarifa na kwamba wanasubiri taarifa kutoka mkoani (polisi).

Baada ya kauli hiyo mshereheshaji alisema kwa "kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Urio, kwa sasa tunaondoa mazingira ya mazishi, tunabaki na maombolezo. Hayo mengine ya kifamilia yatabaki wao kama wao, lakini waombolezaji wengine ambao tulipata nafasi ya kuja kumuhifadhi kijana wetu tutaenda nyumbani, tutapewa tarehe nyingine na siku nyingine ya maziko."

Alisema "Tuwaombe radhi kwa kilichotokea na nikuombe umshukuru Mungu kwa nafasi hii uliyopewa ya kushiriki na familia, lakini nikutakieni kila la heri kwenye majukumu na mfike salama na msituache kama familia.

“Tupiganieni kwa sababu bado hatujazika na bado tuna gharama zilishatumika, nyingine hazikulipwa na tutaenda kuzilipa baadaye katika tarehe husika ya kumzika kijana wetu, niombe tuendelee kushikiana na familia na michango mbalimbali hadi siku ya maziko ya kijana wetu."

Aidha alisema baada ya majibu kutoka polisi, familia itakaa na kutoa taarifa ya siku ya maziko hayo.