Maziwa ya nyuki tiba ya magonjwa ya binadamu

Maziwa ya nyuki tiba ya magonjwa ya binadamu

Muktasari:

  • Wahenga walisema, “baniani mbaya kiatu chake dawa.” Msemo huu unajidhihirisha kupitia nyuki namna alivyo hatari anapochokozwa na binadamu, lakini mazao yake ni dawa zinazoelezwa kutibu magonjwa mbalimbali.


Dar es Salaam. Wahenga walisema, “baniani mbaya kiatu chake dawa.” Msemo huu unajidhihirisha kupitia nyuki namna alivyo hatari anapochokozwa na binadamu, lakini mazao yake ni dawa zinazoelezwa kutibu magonjwa mbalimbali.

Mbali na mazao ya asali na nta, nyuki pia hutoa maziwa ambayo kitaalamu huitwa Royal Gel na sumu ambayo hutumika kutibu magonjwa na kuondoa muonekano wa uzee.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, daktari wa tiba kwa kutumia nyuki na mazao yake kutoka Tanzania Internation Bee Limited, Dk Musiba Paul alisema maziwa ya nyuki hutumika kutibu magonjwa yanayohusisha homoni kwa wanawake na wanaume.

“Kwa wanawake husaidia kutibu magonjwa kama homoni imbalance na kwa wanaume wenye matatizo ya kushindwa kumpa ujauzito mwanamke yanayosababishwa na mbegu kukosa mkia, uchache wa mikia na mbegu hafifu,” alisema Dk Musiba.

Pia, alisema maziwa ya nyuki kwa anayeyatumia mara kwa mara hufanya kuonekana bado kijana kutokana na kuongezeka kwa uzalishwaji wa seli za mwili.

“Hii inasababishwa na uzalishwaji wa seli kuwa mkubwa kuliko seli zinazokufa, ndio maana malkia wa nyuki anaweza kukaa hata miaka mitano huku aina nyingine wakiishi ndani ya muda wa siku 60 tu,” alisema Dk Musiba.


Sumu ya nyuki

Pia, alisema sumu ya nyuki ni zao linalotumika kutibu magonjwa mengi yanayosababishwa na bakteria, fangasi na virusi pamoja na kuondoa maumivu mwilini.

“Tafiti mbalimbali duniani zimeonyesha matibabu kupitia mazao haya ya nyuki yameleta matokeo mazuri katika kutibu saratani na kupunguza makali ya virusi vya ukimwi, tafiti bado zinaendelea,” alisema Dk Musiba na kuongeza:

“Matibabu haya hufanywa na mtaalamu kwa kukung’atisha nyuki kutokana na ugonjwa husika na kuna taratibu za kitabibu hufuatwa,” alisema Dk Musiba.

Taratibu za kupata matibabu hayo ni pamoja na kutibu ugonjwa unaofahamika, kumtibia mgonjwa mwenye cheti cha daktari pamoja na kujiridhisha uzito wa mgonjwa, presha, kiwango cha sukari na kiasi cha mzio anachoweza kupata baada ya kuumwa na nyuki.

“Matibabu haya hutumika kutibu watu waliopooza, maumivu ya mgongo, wenye matatizo ya nguvu za kiume, kuwahi kufika kileleni,” alisema Dk Musiba.


Mazao mengine ya nyuki

Dk Musiba alisema kuna mazao mengine ya nyuki yanayotumika kutibu magonjwa mbalimbali kama gundi ya nyuki inayotibu magonjwa ya njia ya mkojo (UTI), mfumo wa uzazi (PID), vidonda vya tumbo na mengineyo mengi.

Dk Musiba alisema mazao ya nyuki hutumika kutengeneza sabuni, mafuta ya kujipaka mwilini, singo (scrub) na asali.

“Hadi sasa ni mwezi mmoja tangu matibabu hayo yaanze kwa wagonjwa zaidi ya 100, wengi wao wamepata nafuu na wengine kupona kabisa,” alisema Dk Musiba.

Mmoja wa wananchi waliopatiwa matibabu ya miguu kutoka Tanzania Internation Bee Limited, Mama Maria alisema alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya miguu kwa miaka 15 na baada ya kupata matibabu amepona kabisa.

“Nilianza tiba katika kituo hiki na sasa naendelea vizuri kabisa, nafanya shughuli zangu kama kawaida,” alisema.


Mazao haya yanapatikanaje

Mkufunzi katika masomo ya ufugaji nyuki na mazao yake kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Kidabaga alisema sumu ya nyuki ni zao linalotengenezwa na nyuki kujilinda dhidi ya maadui kama viumbe wasumbufu kwao.

“Sumu hii ina kemikali ambazo husababisha binadamu anapoumwa na nyuki kuvimba au kupata maumivu makali, lakini binadamu anaweza kuitumia kujitibu, ikiwamo maumivu mwilini, kupooza mwili, kuimarisha kinga na kuongeza uzalishwaji wa seli zinazopambana na magonjwa mwilini,” alisema Kidabaga.

Alisema kuna namna kadhaa za kuvuna sumu hiyo, ikiwamo kuwakamata nyuki na kuwasaga kisha kuchambua sumu, kumkamua nyuki na kuondoa sumu na namna nyingine ni kutumia vifaa maalumu. “Baada ya hapo huchukuliwa na kuandaliwa kitaalamu, pia huhifadhiwa katika ubaridi, baada ya hapo inaweza kutumika kutibu kwa kutumia njia mbalimbali,” alisema Kidabaga.

Pia, alisema sumu inayotumika hutokana na nyuki vibarua ambao ni majike wasiotaga mayai.

Kuhusu maziwa ya nyuki, Kidabaga alisema ni yale yanayotumika kulishia watoto wa nyuki wenye umri wa chini ya siku tatu na kwa yule anayeandaliwa kuwa malikia hutumia maziwa haya kama chakula hadi mwisho wa maisha yake.

“Ni kimiminika kisicho na rangi, chenye harufu na ladha ya ukali kidogo ndicho husababisha nyuki kuwa dume, malkia au kibarua,” alisema.