Mbarawa ataka madereva treni wapate muda wa mapumziko kuepusha ajali
Muktasari:
- Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ametaka safari za madereva treni ziangaliwe upya kwani zimekuwa chanzo cha ajali.
Dodoma. Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ametaka safari za madereva treni ziangaliwe upya kwani zimekuwa chanzo cha ajali.
Profesa Mbarawa ametoa agizo hilo leo Oktoba 27 jijini Dodoma wakati akifungua semina ya siku mbili ya usalama wa reli kwa wadau wa sekta ndogo ya usafiri kwa njia ya reli.
Waliokutana katika semina hiyo ya siku mbili, ni viongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Shirika la Reli Tanzania na Zambia (Tazara) na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa nchi Kavu (Latra).
Waziri amesema kumekuwa na ajali ambazo chanzo chake ni uchovu wa madereva wa treni ama wakati mwingine wanasinzia na kushindwa kumudu vyombo hivyo.
Amesema kama si kusinzia basi huenda watumishi hao wanapangiwa umbali mrefu wa kuendesha treni.
"Wakati mwingine watu wanakuwa wamechoka kupita kiasi na hii ni Kwa treni hii tuliyonayo, je ikifikia wakati wa kutumia treni ya mwendo kasi hamuoni kosa dogo linaweza kusababisha majanga makubwa," amesema Profesa Mbarawa.
Kwa upande mwingine Profesa Mbarawa ameuagiza uongozi wa Latra kutembelea maeneo na kutoa maoni juu ya nini kifanyike badala ya kutoa maelekezo wakiwa wamejifungia maofisa.
Amesema kitendo cha kutoa maagizo na hukumu bila kutembelea maeneo yao na kutoa ushauri kwa sasa hakipaswi kuendelea bali wahusika watoe na kujionea mazingira ya usafirishaji.