Mbaroni akidaiwa kumuua kaka yake aliyemzuia asibake

Mbaroni akidaiwa kumuua kaka yake aliyemzuia asibake

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia Melita Ndaletyan (34) kwa tuhuma za kumuua kaka yake Kiseri ( 38) aliyemzuia kumbaka mke wa kaka yao mkubwa.


Arusha.  Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia Melita Ndaletyan (34) kwa tuhuma za kumuua kaka yake Kiseri ( 38) aliyemzuia kumbaka mke wa kaka yao mkubwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Maseju amesema tukio hilo lilitokea jana Alhamisi Julai 8, 2021 saa 6:30 usiku katika Kitongoji cha Naamalasin kata ya Noondoto wilayani Longido Mkoa wa Arusha.

Amesema Kiseri alifariki dunia baada ya kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni na mdogo wake na kwamba wote wawili wanajihusisha na shughuli za ufugaji na walikuwa wakiishi kwenye boma moja.

Amebainisha kuwa  siku ya tukio mtuhumiwa alitaka kutenda kosa hilo kwa mke wa kaka yake ambaye hakuwepo nyumbani wakati huo.

“Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali chanzo cha tukio hilo ni tamaa ya kimapenzi ambapo mtuhumiwa huyo anadaiwa kutaka kumwingilia kimwili mke wa kaka yake na kuzuiwa na marehemu kufanya jambo hilo jambo lililosababisha ugomvi kati yao.”

"Baada ya kumzuia alichomoa kitu chenye ncha kali na kumchoma ndugu yake huyo. Bado tunamshikilia mtuhumiwa kwa kumfanyia ukatili ndugu yake na mara baada ya upelelezi kukamilika jalada litapelekwa ofisi ya mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria,"

Kwa mujibu wa Kamanda mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa familia kwa ajili ya taratibu za maziko baada ya kufanyiwa uchunguzi.


Imeandikwa na Janeth Mushi, Mwananchi