Mbaroni kwa tuhuma za kumchoma moto mtoto wake

Tuesday September 14 2021
mtotopic
By Joseph Lyimo

Babati. Mkazi wa Mtaa wa Negamsii mjini Babati, Mkoa wa Manyara, Janeth Vicent anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumchoma moto mtoto wake wa kike baada ya kumuomba fedha mpitanjia.

Akizungumza mjini Babati leo Jumanne Septemba 14, 2021 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi (ACP), Merrison Mwakyoma amesema tukio hilo limetokea Septemba 12 saa 3 asubuhi.

Kamanda Mwakyoma amesema mtuhumiwa huyo Janeth alimchoma moto mtoto wake Neema Vincent (3) kwa kutumia kitu chenye ncha kali.

Amesema mtuhumiwa huyo alimchoma moto mtoto huyo wa miaka mitatu sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya kumuomba pesa mpitanjia.

Amesema mama mzazi huyo alimfanyia mtoto wake ukatili huo kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali sehemu za usoni shingoni na kumsababishia majeraha mbalimbali.

"Baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo waliamua kutoa taarifa katika kituo cha polisi, waliofika eneo la tukio na kumkamata mtuhumiwa huyo," amesema Kamanda Mwakyoma.

Advertisement

Amesema hivi sasa mtoto huyo amelazwa kwenye hospitali ya Mrara inayomilikiwa na halmashauri ya mji wa Babati.

Ametoa onyo kwa wazazi kutowaumiza watoto wao kwani tukio la mtoto kuomba fedha kwa mpita njia lingepaswa kukemewa mapema ila mtoto wa miaka mitatu ni mdogo.

"Mzazi mwenyewe alipaswa kumfundisha mtoto wake maadiili mema kwa kutumia busara badala ya kumfanyia ukatili kwani ni kosa kisheria," amesema Kamanda Mwakyoma.


Advertisement