Mbatia akosa uvumilivu, Mutungi ataka watulie

Thursday June 23 2022
mbatiapiic
By Tuzo Mapunda

Dar es Salaam. Mkuu wa Idara ya Uenezi na Uhusiano wa umma wa Chama cha NCCR Mageuzi, Edward Simbeye ameziomba mamlaka za Serikali kuchukua hatua za dharura kumaliza mgogoro unaoendelea ndani ya chama hicho, la sivyo unaweza kuleta madhara zaidi.

Alisema hadi sasa hawana imani na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa namna inavyoshughulikia suala hilo, kwani wamekuwa hawajitokezi kwenye vikao wanavyokubaliana kufikia maamuzi na hata wakiandikiwa barua hawaoneshi ushirikiano.

Hata hivyo, Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, Jaji Francis Mutungi alipozungumza na Mwananchi, aliwataka viongozi hao watulie.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam mara baada ya kutoka kwenye kikao kilichoitishwa na Ofisi ya Msajili, Simbeye alisema hakikuwa na tija kwa sababu upande wa pili wanaosigana ukiongozwa na Katibu Mkuu wao, hawakuhudhuria na hakuna taarifa yoyote iliyotolewa.

“Tumeitikia wito leo Juni 21, 2022 tulikuwa na kikao na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, tumefika tangu saa tatu asubuhi hadi saa nane mchana wenzetu wa upande wa pili hawajafika kwenye shauri hili.

“Cha kusikitisha zaidi Jaji Francis Mutungi hajafika kwenye shauri hili na Sisty Nyahoza hayupo ofisini, ambaye ametupokea ni Naibu Msaidizi Hamed Hamed, tumekaa kuna mambo ambayo tumejadiliana hatuwezi kuyazungumza hapa mbele ya vyombo vya habari,” alisema.

Advertisement

Alisema kulingana na mambo yanavyoendelea wanashindwa kuvumilia na wanaamini Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini inahusika kwa asilimia kubwa kufadhili mgogoro huo aliodai kuwa athari zake ni kubwa kwa baadaye endapo hatua za kutatuliwa hazitachukuliwa haraka.

“Kwa sababu jambo limeenda kwenye udini, Utanganyika na Uzanzibari tumeandika barua kuzifikisha Ofisi ya Msajili na leo wiki ya pili hatujapata majibu na kwenye kikao tulichofanya leo hakuna majibu ya msingi ambayo tunapaswa kuyapeleka kwa Watanzania,” alisema.

Alisema wamelivumilia suala hilo kwa muda mrefu na walikuwa wanazuia vijana wao wasifanye jambo lolote, lakini kwa namna mambo yanavyokwenda uvumilivu utawashinda.

“Ni rai yetu kuitaka Ofisi ya Msajili kufanya uwajibikaji wa haraka kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kiserikali waoneshe uongozi kwenye suala hili, nchi inakwenda shimoni,” alisema.

Hata hivyo, Mwananchi lilimtafuta Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza azungumze kuhusu kutokuhudhuria kwenye kikao hicho, alijibu kwa ufupi akidai kwamba yeye hana uwezo wa kusema.

Advertisement