Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbinu kumlinda mtoto dhidi ya matumizi hasi ya teknolojia hizi hapa

Muktasari:

  • Katika miaka ya hivi karibuni, ukuaji wa teknolojia na upatikanaji wa simu janja umeongeza fursa za watoto kupata taarifa, kujifunza na kuwasiliana, lakini pia umeibua changamoto mpya zikiwamo unyanyasaji wa mtandaoni, uraibu wa mitandao ya kijamii, maudhui yasiyofaa kwa watoto na utapeli wa kidijitali.

Dar es Salaam. Wakati nchi za Afrika leo zikiadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, wadau wa malezi, elimu na teknolojia wameonya kuhusu kuongezeka kwa matumizi hasi ya teknolojia miongoni mwa watoto, wakitaka hatua za haraka kuchukuliwa ili kuwalinda dhidi ya hatari zinazotokana na matumizi yasiyo salama ya mitandao na vifaa vya kidijitali.

Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa kila mwaka Juni 16 ikiwa ni kumbukumbu ya watoto wa Soweto nchini Afrika Kusini waliouawa mwaka 1976 walipokuwa wakidai haki yao ya kupata elimu bora.

Katika miaka ya hivi karibuni, ukuaji wa teknolojia na upatikanaji wa simu janja umeongeza fursa za watoto kupata taarifa, kujifunza na kuwasiliana, lakini pia umeibua changamoto mpya zikiwamo unyanyasaji wa mtandaoni, uraibu wa mitandao ya kijamii, maudhui yasiyofaa kwa watoto na utapeli wa kidijitali.

Changamoto hizo zimewaibua baadhi ya wadau wa haki za watoto wakihimiza kila mtu katika jamii kutekeleza majukumu yake kuwalinda watoto dhidi ya matumizi yasiyofaa ya teknolojia.

Wadau hao wanasisitiza kuwa ulinzi wa mtoto katika zama za teknolojia unahitaji ushirikiano wa wazazi, shule, serikali, kampuni za teknolojia na jamii kwa ujumla.

Akizungumza na Mwananchi Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga amesema teknolojia imekuwa nyenzo muhimu katika kujifunza, kufanya tafiti na kupata taarifa mbalimbali.

Henga amesema pamoja na manufaa hayo katika matumizi ya teknolojia baadhi ya watoto wamekutana na maudhui yasiyofaa.

Amesema changamoto hiyo siyo kwa nchi za Afrika pekee bali ni dunia nzima na ndio sababu baadhi ya nchi ikiwemo Uingereza tayari zimeshaanza kuchukua hatua ya kudhibiti matumizi hayo kwa watoto.

“Simu na teknolojia ni muhimu katika elimu na maendeleo ya mtoto, lakini matumizi yake yanapaswa kuwa chini ya uangalizi wa wazazi na walezi. Sio kila taarifa au tovuti inayopatikana mtandaoni inafaa kwa mtoto”amesema Henga.

Pia amesisitiza kuwa kuna haja ya Serikali kuimarisha sheria na mifumo ya ulinzi wa watoto katika mazingira ya kidijitali.

  Nancy Faustine kutoka Shirika la Her Initiative, amesema moja kati ya sababu inayochangia matumizi yasiyofaa ya teknolojia kwa watoto ni baadhi ya wazazi au walezi kuwapatia watoto wao vifaa hivyo bila ya kuwapa elimu ya matumizi sahihi.

Mtaalamu wa malezi ya watoto, Irene Massawe amesema matumizi ya teknolojia bila usimamizi wa wazazi yanaweza kuwa chanzo cha mmomonyoko wa maadili na kuathiri afya ya akili ya mtoto.

“Teknolojia si adui wa mtoto, lakini matumizi yake yasiyodhibitiwa yanaweza kumuweka mtoto katika mazingira hatarishi. Wazazi wanapaswa kufahamu kile watoto wao wanachotazama na muda wanaoutumia mtandaoni,” anasema.

Naye mtaalamu wa teknolojia, Mohammed Said anasema ili kuweza kuwadhibiti watoto dhidi ya matumizi yasiyofaa ya teknolojia, wazazi, walezi wanatakiwa kujifunza na kuifahamu vyema.

Said amesema watakapojifunza na kuifahamu vyema teknolojia na namna inavyofanya kazi itakuwa rahisi kwao kutumia mifumo ya kudhibiti matumizi hasi kwa watoto.

Amesisitiza wazazi na walezi kutumia mifumo ya kudhibiti matumizi ya intaneti kwa watoto pamoja na kuweka kanuni za matumizi ya vifaa vya kidijitali nyumbani.

“Si kila taarifa inayopatikana mtandaoni inafaa kwa mtoto. Teknolojia za kudhibiti maudhui zipo, lakini muhimu zaidi ni mazungumzo ya wazi kati ya wazazi na watoto kuhusu matumizi salama ya teknolojia,” amesema.

Mwalimu Emmanuel Kamenge amesema taasisi za elimu zina jukumu la kuwajengea watoto uwezo wa kutumia teknolojia kwa usalama.

“Tunapaswa kuwafundisha watoto wajue namna ya kutambua taarifa za uongo, kujilinda dhidi ya watu wenye nia mbaya mtandaoni na kutumia teknolojia kwa maendeleo yao,” amesema.