Mbowe adai wazo la shule za kata lilianzia Hai alipokuwa mbunge

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe katika moja ya mikutano yake. Picha na Chadema
Muktasari:
- Viongozi wa Chadema wapo kwenye ziara maalumu ya operesheni +255 katika kanda ya Kaskazini ikijumuisha mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.
Hai. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema mpango wa ujenzi wa shule za sekondari za kata, ulianzia jimbo la Hai mwaka 2000 alipokuwa mbunge wa jimbo hilo.
Mbowe ameyasema hayo Jumamosi Julai 13, 2024 wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho, uliofanyika Nshara, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro ikiwa ni mwendelezo wa Operesheni +255.
Amesema mwaka 2005 wakati Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete anaanzisha mpango wa ujenzi wa shule za sekondari za kata, katika jimbo la Hai walikuwa wameshajenga shule 12 kwa nguvu za wananchi.
“Wakati nakuwa mbunge wa Hai mwaka 2000, miaka 24 iliyopita, mimi ndiye mtu niliyewaza kujenga shule za sekondari za kata katika nchi hii na moja ya shule za kwanza za kata ilikuwa ni shule ya Harambee,” amesema Mbowe na kuongeza:
“Wakati ule CCM haijafikiria shule za kata, tulishajenga shule 12 za kata katika jimbo la Hai kwa nguvu za wananchi na mwaka 2005 anaingia Kikwete (Jakaya Kikwete) na Lowassa ndiyo wakaiga sera ya Hai ya kujenga sekondari za kata na zikajengwa nchi nzima, wakati wazo hilo limeanzia Hai.”
Kukisafisha kijiji cha Nshara
Mbowe amesema Kijiji cha Nshara kinasifika kwa ulevi, matumizi ya bangi, dawa za kulevya na pombe haramu ya gongo katika Wilaya ya Hai na kwamba kwa sasa wanakwenda kukisafisha kwa kuwa hawawezi kufumbia macho hali hiyo.
“Kijiji hiki kina sifa kubwa ya ulevi, uvutaji wa bangi, dawa za kulevya na gongo, hili wazee wangu tukubaliane, hiki kijiji tunakisafisha, hata kaka yangu anasikia, hatuwezi kuendelea kuwa na kijiji ambacho eti ni kijiji cha mfano cha walevi Wilaya ya Hai,” amesema.
Mbowe ambaye kijiji hicho ndipo nyumbani kwake, amesema kama kuna vijana wanataka kwenda kutafuta maisha katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo mkoani Mtwara na hawana nauli, wajiorodheshe na kwamba wao watawapa nauli.
“Watoto waende Mtwara, Lindi, Mbeya, Shinyanga na Dar es salaam wakatafute maisha, siyo kupoteza maisha na bodaboda hapa, kama ni bodaboda iwe ya kupita kutafuta mtaji kidogo na kuishia.
“Vijana wa Kichaga jeuri yake mtoke mkatafute mkirudi huku mletee familia, mtunze familia, tutasafisha hiki kijiji, naomba ili kazi hii ifanyike hawa viongozi hawatoshi. Tunataka tuunde kamati hapa ya watu jasiri, wanawake kwa wanaume wanaojiamini, tuweke mkakati wa kukisafisha,” amesema.
Mbowe amesema uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani, patachimbika kati ya Chadema na CCM.
“CCM ilikuwa inahangaika na Hai lakini leo Chadema imejaa Mbeya kuliko Hai, Chadema iko Songwe, Rukwa, Serengeti, Mara, Kigoma na Kagera na ndiyo chama kikuu cha upinzani nchini, na uchaguzi wa mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani ni patashika Chadema na CCM,” amesema.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amewashauri vijana kuondoka nyumbani na kwenda mikoani kutafuta maisha akidai kazi ya bodaboda imewafunga na ujira mdogo.
“Kabla ya bodaboda vijana wa Kichaga mlikuwa mkimaliza shule mnatoka, leo kazi hizi zimewafunga na kuwafanya mmekuwa watumwa wa ujira mdogo.
“Ushauri wangu, Ibrahim hakufanikiwa mpaka alipotoka, msifungwe na kazi hizi, wachaga ni watu wajasiri wanaojua kuchukua hatua kabla ya kuona mbele, ondokeni nendeni mikoani mkatafute maisha,” amesema Lema.
Chadema kipo kwenye ziara maalumu ya operesheni +255 katika kanda ya Kaskazini kwenye mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga ambapo katika Mkoa wa Kilimanjaro tayari wamefanya mikutano maeneo mbalimbali ya wilaya za Same, Mwanga, Rombo, Moshi na Hai.