Mbowe aivaa CCM, yamjibu

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema chama tawala, CCM kinapaswa kulaumiwa kwa maumivu yote ambayo Watanzania wameyapata katika miaka 30 ya mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema chama tawala, CCM kinapaswa kulaumiwa kwa maumivu yote ambayo Watanzania wameyapata katika miaka 30 ya mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini.

Amesema katika muda huo, Tanzania imepitia vipindi tofauti, lakini kipindi cha kati ya mwaka 2015 – 2021 kilikuwa cha maumivu makali kwenye demokrasia na athari zake kila Mtanzania alizishuhudia.

Hoja hizo za Mbowe zilijibiwa na mjumbe wa Kamati kuu ya CCM, Stephen Wasira akisema CCM haiwezi kulaumiwa kwa kila jambo kwa sababu mambo mengine yanatokea kwenye vyama bila chama chenyewe kuhusika.

Mbowe alitoa lawama hizo juzi jioni, wakati akichangia mjadala kuhusu hali ya siasa ya vyama vingi na maendeleo nchini, ulioandaliwa na Kituo cha Kimataifa cha Sera Afrika (CIP) na kufanyika kupitia mtandao wa Clubhouse.

Mjadala huo ulioanza saa 11:00 jioni ulimalizika saa 3:00 usiku na kushirikisha wadau mbalimbali, wakiwemo wanasiasa wakongwe Wasira, Zitto Kabwe na Hamad Rashid Mohammed.


Kipindi kigumu zaidi

Katika mchango wake uliochukua dakika 14, Mbowe alisema kwa miaka yote 30 CCM ndiyo imekuwa madarakani na katika muda huo kipindi kigumu zaidi kilikuwa kati ya mwaka 2015-2021 chini ya Rais John Magufuli.

“CCM wabebe dhambi zote kwa makosa yote waliyoyafanya katika Taifa hili, ndiyo maana waliruhusu mwenyekiti wao na Rais wao kuli-abuse (kulikosea) taifa hili na hakuna aliyesema, wote walikaa kimya,” alisema Mbowe.

Mwenyekiti huyo wa Chadema alisisitiza kuwa chama kina wajibu wa kumdhibiti kiongozi wake pale kinapoona anakwenda kinyume na maadili au sheria, lakini “CCM wao walikaa kimya wakati uchafuzi wa demokrasia ukifanyika.”

Alitolea mfano kwa Afrika Kusini ambako chama cha ANC kimekuwa kikiwawajibisha viongozi wao kuanzia kwa Thabo Mbeki, Jacob Zuma na kuwa sasa Rais Cyril Ramaphosa yuko kwenye wakati mgumu kisiasa.

“CCM has to take a blame (inapaswa kulaumiwa) kwa namna miaka 30 ya vyama vingi imegeuka kuwa ya maumivu katika Taifa hili,” alisema Mbowe na kusisitiza wakati wa awamu ya tano CCM waligeuka kuwa watu wa kusifia kila kitu.


Haiwezi kulaumiwa

Alipopata nafasi ya kuzungumza katika mjadala huo, mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Stephen Wasira alisema CCM haiwezi kulaumiwa kwa kila jambo kwa sababu mambo mengine yanatokea kwenye vyama bila chama cyenyewe kuhusika.

Alitolea mifano migogoro kwenye vyama vya upinzani ndani ya NCCR-Mageuzi kati ya Augustine Mrema na Mabere Marando na pia ndani ya CUF akisisitiza kuwa kote huko CCM haikuhusika kwenye migogoro hiyo.

“Mimi nadhani huu ni wakati wa kujadili tunakwendaje mbele, tukianza kunyoosheana vidole hatuwezi kufika tunakotaka kwenda. Wote tunazungumzia habari ya maridhiano, sasa tutafikia hayo maridhiano kama tunalaumiana?” alihoji Wasira.

Mkongwe huyo wa siasa nchini na aliyewahi kuwa kada na mbunge wa wa upinzani, alisema wakati mwingine unaweza kuwa na kiu ya kutaka mabadiliko kumbe wewe mwenyewe ukawa ndiyo kikwazo katika kuyafikia mabadiliko hayo.

Alisisitiza kujadili namna ya kutoka Taifa lilipo ili kwenda mbele.

Licha ya mtazamo huo wa Wasira, akiwa na mtazamo unaofanana na wa Mbowe, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alisema CCM haikuutaka mchakato mzima wa kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi, lakini kwa sababu ya nguvu za nje na ushawishi wa Mwalimu Julius Nyerere uliruhusiwa.

Alisema CCM waliichukua hoja ya mfumo wa vyama vingi wakaifanya kuwa yao, wakaipeleka bungeni ambako wao ndiyo wengi, wakapitisha.

“The origin sin (dhambi ya asili) ya demokrasia yetu imekuwa ni supplied democracy (demokrasia ya kupewa). Kwamba CCM walikaa wakajadiliana wakakubali kutupatia, maana yake ni kwamba wakiitaka hiyo demokrasia wataichukua “kama ilivyokuwa mwaka 2016 – 2021.”

“Mimi nafikiri njia sahihi zaidi ni kujenga a demand for democracy (mahitaji ya demokrasia). Iwe ni demokrasia yetu, siyo ile ya kupewa ambayo mtoaji akiitaka anaichukua muda wowote,” alisema Zitto.


Utashi wa Rais

Mbali na hoja hiyo, katika mjadala huo ulioibua mambo mbalimbali, washiriki walizungumzia haja ya kuwa na Katiba mpya ambayo itazingatia masilahi ya makundi yote katika jamii na kuendana na mabadiliko mengi ambayo yametoka hivi karibuni.

Maoni hayo ya wadau yametolewa wakati kikosi kazi cha kuratibu maoni ya demokrasia kikiendelea kukusanya maoni ya wadau mbalimbali kuhusu maeneo tisa, likiwemo katiba mpya na Tume Huru ya Uchaguzi, kabla ya kuchambuliwa na kuwasilishwa serikalini kwa utekelezaji.

Akizungumzia suala la Katiba, Mbowe alisema Katiba ya sasa inatoa kinga kwa kila kiongozi wa juu, jambo ambalo linasababisha wafanye uamuzi wa kihuni kuhusu mambo ambayo hayana masilahi kwa Taifa.

Alisisitiza kwamba Watanzania hawana budi kuyakataa mambo hayo kwa nguvu zote na njia pekee ya kufanikisha hilo ni kupigania Katiba mpya kwa nguvu zote ili kujenga mazingira bora ya kisiasa nchini.

“Kuna mambo mengi ya kujadili kwenye Katiba mpya; kuna mifumo ya utawala, mgawanyo wa madaraka, usimamizi wa rasilimali zetu, tume huru ya uchaguzi. Lazima tupiganie mambo haya,” alisema Mbowe.

Hata hivyo, Mbowe alisisitiza kuwa kwa hali ya nchi ilivyo sasa, suala la kupata Katiba mpya liko mikononi mwa Rais Samia.

“Sisi na wanaharakati wengine tutaendelea kuweka presha, lakini linategemea zaidi utashi wa Rais na tunashukuru kuona Rais ana utashi huo,” alisema.

Akichangia eneo hilo, Hamad Rashid Mohammed, mwenyekiti wa ADC alisema anaamini kwamba kuna haja ya kufanya marekebisho ya Katiba mpya kwa sababu muda mrefu umepita na mambo mengi yamebadilika, hivyo Tanzania inahitaji kwenda na wakati.

Hamad ambaye pamoja na Zitto ni miongoni mwa wajumbe 25 wa kikosi kazi, alitoa mfano wa Kenya, kuwa pamoja na matatizo yao wamebadilisha Katiba na kuweka mambo mengi ya msingi ambayo yamelifanya Taifa hilo kuwa na katiba bora zaidi.

“Tunahitaji kuwa na Katiba itakayotupeleka mbele, mambo yamebadilika, dunia imebadilika, tunahitaji kwenda sambamba na mabadiliko ya ulimwengu,” alisema mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa kiongozi wa upinzani bungeni.

Kata hivyo katika majumuisho, Mbowe alisema “mchakato wa katiba upo mikononi mwa Rais Samia ambaye ndiye mwamuzi wa mwisho wa kuhakikisha mchakato huu unafikia mwisho na sisi tunamwombea afanye hivyo.”

Aidha, Mbowe alisema suala si la vyama vya siasa au wanasiasa pekee, bali ni la wananchi wote wanaopaswa kushiriki kikamilifu “ili tuwe na Katiba ya miaka 30, 60 au 100 ijayo.”


Maridhiano

Wadau hao wa demokrasia walijadili kuhusu maridhiano ya kitaifa, huku wakijielekeza kwenye dhana ya Rais Samia ya 4R katika uongozi wake, ikijumuisha suala la maridhiano kama njia ya kujenga umoja wa kitaifa na kuimarisha demokrasia.

Tayari Rais Samia amekutana na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa nchini ambapo Julai 15 mwaka huu alikutana na viongozi wa ADC, ACT Wazalendo na CUF kisiwani Pemba, Zanzibar.

Akigusia suala hilo, Wasira alisema hali ya kisiasa nchini imekuwa na milima na mabonde, kwa maana wakati fulani Taifa lilifanya vizuri zaidi lakini wakati mwingine hatukufanya vizuri.

“Rais amezungumzia 4R, na moja ya hizo R ni maridhiano. Sasa tunaridhiana kwenye nini, maana yake lazima tukae pamoja tuzungumze namna bora ya kujenga demokrasia yetu,” alisema Wasira.

“Nadhani nia ya Rais ni nzuri na sisi tunamuunga mkono. Tena nadhani sisi wote katika mfumo wa vyama vingi tuungane wote kumuunga mkono Rais wetu,” aliongeza Wasira.

Kwa upande wake, Mbowe alisema wanapokwenda kwenye majadiliano, wanataka mabadiliko katika nchi ili mwisho wa siku wawe na maridhiano ambayo yatalisaidia Taifa.

“Nampongeza Rais Samia kwa kusogeza sikio la kusikiliza, sasa naomba sikio la kusikiliza liende na vitendo. Tunatakiwa tujadiliane, tujue nani anataka nini, tutafute balance (mlinganyo) sehemu fulani pale,” alisema Mbowe, aliyewahi kuwa mbunge wa Hai na kiongozi wa upinzani bungeni.

Alisema “haya majadiliano yanapaswa kuwa na ukomo, hayawezi kuendelea tu, lazima yafikie mwisho ili shughuli nyingine ziweze kuendelea.”

Hoja hiyo iliungwa mkono na Hamad Rashid aliyesema, “naungana na Mbowe kwamba majadiliano haya lazima yawe na time frame.”

Kwa upande wake, Zitto alisema Tanzania imefika kwenye mazingira ya kisiasa ambayo ni kama ndiyo imeanza safari ya demokrasia kama ilivyokuwa mwaka 1992. Alipendekeza kuwa na demokrasia ya majadiliano.

“Mimi napendekeza kuwa na ‘a negotiated democracy’ (demokrasia ya makubaliano) na ndiyo kazi hii inayofanyika sasa hivi. Nawasihi sana wanademokrasia tunatakiwa kujifunza kwenye changamoto na mafanikio tuliyopita.”


Demokrasia na jinsia

Akizungumzia suala la jinsia na demokrasia, mhadhiri wa sheria katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Victoria Lihiru alisema Tanzania imepiga hatua kwa sababu idadi ya wanawake wanaoshiriki katika vyombo vya uamuzi imeongezeka.

Alisema kwa sasa idadi ya wabunge wanawake ni asilimia 36 ya wabunge wote, huku Tanzania ikiwa na Rais mwanamke na kwa mara ya pili Bunge limepata Spika mwanamke, mawaziri tisa na wakuu wa mikoa wanne.

“Tumepiga hatua kwa kutanua wigo wa wanawake kushiriki katika demokrasia. Tumeweza kupata sera na sheria zenye mrengo wa jinsia kama kwenye umiliki wa ardhi. Hatujafika pale ambapo jumuiya ya kimataifa inataka tufike lakini tumepiga hatua,” alisema Lihiru.

Hata hivyo, alisema katika miaka 30 ya vyama vingi, Tanzania inatakiwa kuwa na vyama vinavyozingatia masuala ya kijinsia katika uendeshaji wa vyama vyao, hasa katika nafasi za juu za uongozi.

“Katika uchaguzi wa mwaka 2020, asilimia 90 wagombea walikuwa ni wanaume na wanawake walikuwa ni asilimia 10 tu. Vilevile, tangu Bunge lianzishwe, wabunge wanawake kwenye majimbo hawajawahi kufika asilimia 10 ya wabunge wote,” alisema mwanazuoni huyo.

Alisisitiza kuna njia kadhaa za kushiriki demokrasia, baadhi ya njia hizo ni pamoja na vyama vya siasa kuwashirikisha wanawake katika nafasi za uongozi wa chama na kugombea nafasi kama vile ubunge na udiwani.

Julai 17 mwaka huu, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Neema Lugangira aliwasilisha maoni yake mbele ya kikosi kazi cha kukusanya maoni ya demokrasia na kupendekeza kuboreshwa sheria mbili ili kuleta usawa na kijinsia, ikiwemo kuteua angalau asilimia 20 ya wagombea wanawake kwa chaguzi zote zinazofanyika.

Alisema licha ya Katiba ya nchi kuweka takwa hilo la Sheria ya Vyama vya Siasa Sura 258, lakini utekelezaji wake haufanyiki kutokana na udhaifu uliopo wa kukosekana kwa chombo kilichopewa nguvu ya kisheria kufuatilia.

“Hivi sasa kupitia Katiba, Sheria ya Serikali za Mitaa kuna kiwango cha asilimia cha uteuzi kilichowekwa kisheria; mfano kwa upande wa ubunge si chini ya asilimia 30 ya wabunge lazima wawe wanawake. Hivyo takwimu zinaonyesha bado tupo nyuma kwenye ushiriki wao katika siasa,” alisema.

Katika maelezo yake, Neema alisema hata taarifa za uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa 2019 na ubunge 2020 zinaonyesha kati ya wenyeviti wa vijiji 11,915 ni asilimia 2.1 tu ni wanawake, kati ya wenyeviti wa mitaa 4,171 ni asilimia 12.6 tu ni wanawake na kati ya wenyeviti wa vitongoji 62,612 ni asilimia 6.7 tu ambao ni wanawake wakati kwa wabunge, katika ya majimbo 238 asilimia 9.1 tu ndiyo wanawake.

Aidha alisema vyama vya siasa vitakiwe kisheria kutumia sehemu ya ruzuku na mapato kupitia wahisani kuwajengea uwezo wanawake na makundi mengine kushiriki katika siasa na eneo hili liwe moja ya maeneo ambayo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anaweza kukagua.


Utayari wa Watanzania

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mohammed Bakari alisema bado Watanzania hawajawa tayari kudai demokrasia yao kama ilivyo katika nchi nyingine ambazo wananchi wake wanadai kwa nguvu.

Alisema miundombinu ya demokrasia nchini bado iko chini, Taifa linaongozwa na Katiba ya chama kimoja na mfumo wa tume ya uchaguzi ambayo si huru, jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa kwa muda mrefu.

“Kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuimarisha huu mfumo wa demokrasia, kwa sababu ya mifumo ya kisheria, hakuna tofauti kubwa kati ya chama tawala na Serikali,” alisema Profesa Bakari.

Alisisitiza kwamba: “Moja ya taasisi nyeti ya kupima maendeleo ya demokrasia ni Bunge, ukitazama Bunge letu la sasa unaweza kuona huenda hata Bunge la wakati wa chama kimoja lilipiga hatua.”