Mbowe akatisha mkutano wake Geita kisa mvua

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akihutubia mkutano mjini Geita 

Muktasari:

  • Mamia ya wananchi wa Geita wameshiriki maandamano hayo ya kilomita 13 kutoka Mtaa wa Nyantorotoro, kata ya Nyankumbu hadi eneo la Msufini lililopo kata ya Kalangalala mjini Geita ulipofanyika mkutano wa hadhara.

Geita. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kuwa hatima ya maisha ya Watanzania ipo kwenye mikono, mioyo na akili zao.

Amesema kila kona ya nchi kuna malalamiko bila kujali aina ya shughuli wanazofanya na kusema, utafiti uliofanywa na chama hicho umebaini malalamiko na matatizo mengi ya wananchi yanatokana na mfumo wa utawala unaotokana na Katiba iliyopo.

Mbowe ameyasema hayo jana mkoani Geita, ambako chama hicho jana kilifanya maandamano ya amani na kumalizia na mkutano wa hadhara.

Hata hivyo, kiongozi huyo amelazimika kukatisha hotuba yake kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mkoani humo.

Chama hicho kilifanya maandamano kwa umbali wa kilomita 13 kutoka Mtaa wa Nyantorotoro, kata ya Nyankumbu hadi eneo la Msufini, lililopo kata ya Kalangalala mjini Geita, ulipofanyika mkutano wa hadhara.

Maandamano hayo yaliyohusisha mamia ya wananchi, yenye lengo la kuishinikiza Serikali kutatua kero za wananchi, ikiwamo ugumu wa maisha, Katiba mpya na Tume Huru ya Uchaguzi, yaliongozwa na Mbowe, aliyeambatana na Mwenyekiti wa Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa (Bavicha), John Pambalu.

Akizungumza kwenye mkutano huo aliouhutubia kwa dakika nane kabla ya kuukatisha kutokana na mvua kubwa iliyoanza kunyesha saa 11:30 jioni, Mbowe amewataka Watanzania kutambua hatima ya maisha yao iko mikononi mwao.

Mbowe amesema maandamano ya kilomita 13 waliyofanya ni ya nchi nzima ya kuwaandaa Watanzania kuelewa hatima ya nchi na maisha yao iko kwenye mikono, mioyo na akili zao.

“Wajibu wetu wa kwanza ni kupigania Taifa lipate Katiba mpya itakayorudisha sauti kwa Watanzania na kuwapa mamlaka ya kusimamia rasilimali zao na uhuru wa kuwachagua viongozi wawatakao, lazima tuimarishe chama chetu kwa kuwa siasa ya Tanzania leo ni CCM na Chadema.

“Tuna wajibu wa kujenga chama imara kitakachokuwa sauti ya wasio na sauti, kuwasemea wananchi wanaoumizwa, kubadilisha mifumo ya utawala na rasilimali za nchi zisimamiwe na wananchi wenyewe,” amesema Mbowe.

Awali akihutubia mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Ziwa, Silvesta Makanyaga amesema mwaka wa uchaguzi wa Serikali za mitaa hawatakubali kilichotokea mwaka 2020 kijirudie.

“Tuliambiwa viongozi tuliowateua kugombea Serikali za mitaa hawajui kusoma na kuandika, sasa Wakurugenzi tuwaambie wazi mwaka huu hatupo tayari, tutatengeneza kalamu za moto ili tuwaandikie,” amesema.

Kwa upande wa Wenje, amesema chama hicho kitaendelea kuandamana hadi ngazi ya kijiji na kitongoji kuishinikiza Serikali kuunda Katiba mpya itakayotengeneza taasisi huru, Tume Huru ya Uchaguzi na kushuka kwa gharama za bidhaa.