Mbowe: Hatuna chuki na sakata la bandari

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe. Picha na mtandao
Muktasari:
- Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe azungumzia tena sakata la bandari, akisisitiza chama hicho, hakina chuki wala hila, lakini hakubaliani na uamuzi wa Serikali kuingia katika makubaliano hayo huku akiwashangaa wanaofanya mzaha na utani kuhusu suala hilo.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema chama hicho hakina chuki wala hila katika msimamo wao wa kutokubaliana na hatua ya Serikali kuingia makubaliano na Serikali ya Dubai kuhusu uwekezaji wa bandari.
Oktoba 25, 2022, Serikali hizo mbili ziliingia makubaliano katika ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari uendeshaji wa miundombinu ya kimkakati ya bandari za bahari na maziwa makuu, maeneo maalumu ya kiuchumi, maegesho ya utunzaji mizigo na maeneo ya kanda za kibiashara.
Mbowe ambaye ni mbunge wa zamani wa Hai mkoani Kilimanjaro ametoa msimamo huo jana Jumamosi Juni 24, 2023 wakati akizungumza na wanadaispora wa Uingereza, nchini humo. Katika mkutano huo Mbowe aligusuia masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
“Hatupingi jambo kwa sababu tuna chuki, hila au wivu bali tunataka Taifa letu liwe mahali salama bora zaidi kwa kuishi. Chadema tulishauri kabla ya kupitishwa Serikali ya Tanzania na Zanzibar kuketi ili kuondoa sintofahamu na kasoro zilizopo, sambammba na kuwapa muda wananchi kuujadili,”amesema Mbowe.
Mbowe ambaye ni kiongozi wa zamani wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni (KUB), amesema sakata hilo linagusa maslahi ya Watanzania wote bara na visiwani, akisisitiza suala hilo sio dogo na halitaishia katika mipaka ya Tanzania.
“Katika wakati mgumu tumia wenye busara, kujenga utengamano na wakati wa changamoto za Taifa unapotumia watu wa utani utani kuzungumza mambo ya muhimu katika Taifa sio sawa kwa sababu ni jambo kubwa linalogusa maisha ya Watanganyika na Wazanzibari,”amesema Mbowe.
Licha ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha azimio kuhusu pendekezo la kuridhia kwa mkataba huo, Serikali imesema haitapuuza maoni na ushauri wa wananchi kuhusu mkataba wa ushirikiano wa uwekezaji.
"Serikali haitapuuza maoni na ushauri wa wananchi kuhusu mkataba huu, wananchi endeleeni kuiamini Serikali na Bunge," Waziri Mkuu amesema Juni 20, 2023 alipohutubia katika sherehe za maadhimisho ya miaka 40 ya moja ya shule jijini Arusha.
Hii ni mara ya pili kwa Mbowe kuzungumzia sakata la bandari, mara kwanza ilikuwa Juni 7, 2023 ambapo alikosoa hatua ya Serikali kuingia makubaliano hayo, akiitaka Serikali kufikiria upya suala hilo.