Mbowe, Lissu waliamsha Arusha, waeleza misimamo kuelekea uchaguzi
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Bara), Tundu Lissu wameanza mikutano ya pamoja mkoani Manyara, wakiwaandaa kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Mikutano hiyo ni sehemu ya Operesheni +255KatibaMpya kwa Kanda ya Kaskazini, itakayofanyika kwa siku 22, ikilenga kuirejesha ngome ya chama hicho kwenye mikoa ya Kanda ya Kaskazini. Jana walianza na mikutano mitano mkoani Arusha.
Kabla ya operesheni hiyo, Lissu alikuwa na mikutano ya hadhara mkoani Singida kwa wiki tatu, huku Mbowe akifanya mikutano ya ndani katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Wakati kila kiongozi akienda kivyake, yalizuka maneno kwamba kuna mpasuko na kila mmoja ana kambi yake, suala ambalo Mbowe amelikanusha mara kadhaa na jana, akisema “tumemwaibisha shetani”.
Historia kuendelezwa
Akihutubia mkutano uliofanyika katika Kata ya Mang’ola, Karatu jana, Lissu aliwataka wananchi wa Mang’ola kukumbuka historia ya eneo hilo la kukataa Tanu katika uchaguzi wa mwaka 1960, baada ya chama hicho kuwawekea mgombea wasiyemtaka.
“Kwenye uchaguzi huo TANU walileta mtu anayeitwa Chifu Henry Dodo. Ninyi watu wa Karatu na Jimbo la Mbulu lilivyokuwa likiitwa wakati huo, mlikuwa na mtu wenu anaitwa Chifu Herman Sarwatt, wakamwambia (Julius) Nyerere sisi tunamtaka mtu wetu.
“Kwa hiyo katika uchaguzi huo, jimbo pekee ambalo walichagua mtu wao ni jimbo la Mbulu. Leo ni jimbo la Karatu na Mbulu Mjini.
“Leo hii kwenye Katiba yetu (ya nchi), CCM wamekataa kurudisha mgombea huru, kwa sababu mwaka 1960 babu na bibi zenu walisema kama Tanu hawakukutaka tutakupa kura. Chifu Herman Sarwatt alisimama kama mgombea huru,” alisema.
Alisema tangu mwaka 1995 hadi 2020 wananchi hao walichagua Chadema na kuweka historia ya jimbo hilo kuongozwa na chama cha upinzani kwa muda mrefu zaidi nchini.
‘Hatukubali kuenguliwa’
Akizungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa, Lissu alisema safari hii hawatakubali kuona wagombea wao wakienguliwa kama ilivyokuwa mwaka 2019.
“Jukumu letu la kwanza ni kumalizana na CCM vijijini Oktoba mwaka huu. Tuna miezi minne tu ya kujipanga na kumalizana nao, kwenye nafasi ya mwenyekiti wa kijiji, mwenyekiti wa kitongoji na wajumbe wa halmashauri za vijiji,” alisema.
Aliwaonya watendaji wa vijiji na kata watakaowahujumu uchaguzi kwa kuengua wagombea wa chama hicho kuwa hawatawavumilia.
“Tunataka tushindwe kwenye kura tu, tusishindwe mezani, tusishindwe kwa kuengua wagombea wetu,” alisema.
Aliwataka pia wananchi kujipanga na Uchaguzi Mkuu wa mwakani, akisema “tukimaliza kwenye kata turudishe halmashauri yetu Chadema inapotakiwa kuwa.
“Hili jimbo la Herman Sarwatt na Dk Willibrod Slaa, haliwezi kuongozwa na CCM,” alisema.
Huku akikosoa sera za uwekezaji za Serikali, Lissu aliwataka wananchi kumchagua mgombea urais atakayeteuliwa na Chadema.
Aliendelea kukosoa ubinafsishaji wa bandari za Tanzania, misitu na rasilimali nyinginezo, akisema unakandamiza wananchi wa maeneo husika na kuwanufaisha watu wa mataifa mengine.
“Ninyi watu wa Mang’ola vitunguu vyenu ili viende Uarabuni vinarushwa na ndege kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta nchini Kenya.
“CCM wenzake wameshindwa kuweka utaratibu wa Mangola na Karatu kupeleka vitunguu kupitia KIA (Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro). Ni wakati wa kumalizana nao,” alisema.
Kwa upande wake Mbowe alisema licha ya ardhi ya eneo hilo kuwa na rutuba inayozalisha mazao mengi, vikiwamo vitunguu, wananchi wake wameendelea kuwa masikini.
“Katika Tanzania nzima vitunguu bora vinatoka Mang’ola, historia ya vituu vya Mang’ola vinajulikana Afrika nzima. Lakini ukipita juu, unaona umasikini wa Mang’ola.
“Watu wa Eyasi mmepakana na Ngorongoro, mmepakana na Manyara, mbuga za wanyama, mmepakana na mbuga ya Tarangire. Ni watu ambao Mungu amewaweka katikati ya neema,” alisema.
Aliendelea kutaja utajiri wa rasilimali, akisema Wilaya Karatu ndio lango la kuingia Mamlaka ya Ngorongoro na Hifadhi ya Ngorongoro, ambako watalii wanalipa gharama kubwa kuingia.
“Wananchi wa Karatu hawana sauti na maliasili zinazowazunguka, mnaishia kuwa manamba wa kulima vitunguu, lakini havibadilishi maisha yenu.
“Mji wa Karatu umekuwa na gharama kubwa kwa sababu ya utalii. Lakini wananchi mnanufaika nini na utalii? Hivi kweli Serikali imeshindwa kujenga barabara kutoka Meatu (Simiyu) kuja Karatu kupitia Eyasi? Tunahitaji kuiondoa CCM madarakani ili kupata maendeleo,” alisema.
Alisema chama hicho kikifanikiwa kuingia madarakani, kitapunguza madaraka ya Rais na kuyapeleka ngazi za wilaya ili kuwanufaisha wananchi.
“Wananchi hawa watengeneze sheria za kulinda soko lao la vitunguu. Inakuwaje mkazalishe vitunguu, vikauzwe Saudi Arabia, vikauzwe Dubai, vikauzwe Somalia na Kenya, mnashindwa kuwa na kitu kinachoitwa Pack House (nyumba ya kufungashia mazao)?
“Vitunguu vyetu vinauzwa ghafi vinakwenda kufungashwa kwenye mifuko Kenya, vinaandikwa made in Kenya, wanauza dunia nzima, Karatu mnaangalia, Mang’ola mnaangalia, CCM inaangalia?” alisema.
Mbowe alisema Chadema itasimamia sera za kiuchumi ili kubadilisha rasilimali kuwa utajiri kwa wananchi.
“Bila kuimarisha uchumi wa Tanzania tutaendelea kuwa ombaomba. Kila siku wanachojua ni kwenda nje ya nchi kuongeza deni la Taifa. Tuna madeni mpaka puani,” alisema.
Tumemwaibisha shetani
Akihutubia Karatu mjini, Mbowe aliwakosoa watu wanaosema chama hicho kimepasuka na kwamba viongozi wake wamegawanyika.
“Tuna kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwamba Chadema tunaendelea kumwaibisha shetani. Nasema tunaendelea kumwaibisha shetani kwa sababu kuna kile chama cha mbogamboga, walisema Chadema inapasuka, Mbowe na Lissu hawazungumzi.
“Hii Chadema ni ya muhimu kuliko mtu yeyote, kwa sababu chama hiki sio cha Mbowe wala cha Lissu, chama hiki ni cha Watanzania wote. Sisi viongozi tuliopewa jukumu la kukilinda na ninawahakikishia Karatu, chama hiki tutakilinda kwa gharama zozote, ikiwemo maisha yetu,” alisema Mbowe.
Alisema chama hicho kimefika hapo kwa gharama za roho za watu, damu ya watu, mali za watu na ulemavu wa watu.
“Tutakuwa wajinga wa mwisho tusipojua wajibu wetu wa kukilinda chama hiki kama mboni za macho yetu. Sisi tunawahakikishia kwamba chama chenu ni salama,” alisema.
Mbowe alitumia mikutano hiyo kuwataka wananchi wilayani Karatu kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kote nchini, ili wawe na silaha ya kupiga kura.
Awali akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema alisema umaskini haujasababishwa na Mungu, bali utaondolewa kwa akili, maarifa na kazi.
Alisema Karatu ambayo imezungukwa na mbuga za wanyama ikiwemo Ngorongoro, Manyara na Tarangire ilipaswa kuwa na uwanja wa ndege ambao ungechangia kuongezeka kwa watalii na kuondoa umaskini.
“Karatu wapo vijana wengi wanaoendesha bodaboda, sehemu kama hii iliyozungukwa na mbuga za wanyama hawakupaswa kuishi maisha haya,” alisema.
Lema, aliyewahi kuwa mbunge wa Arusha Mjini, aliwataka wananchi hao kujiandaa na uchaguzi wa serkali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Imeandikwa na Elias Msuya, Fortune Francis na Janeth Mushi.