Mbowe: Wanaosubiri Chadema ipasuke watasubiri sana

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, akizungumza katika kikao cha mashauriano ya chama hicho Mkoa wa Arusha.

Muktasari:

  • Amesema mgogoro unaosemwa kati yake na makamu mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu haupo. Ahimiza umoja na msamaha ndani ya chama, huku akitangaza operesheni ya majimbo 30.

Arusha. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe amekanusha kuwepo kwa mvutano kati yake na makamu mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, kama ambavyo baadhi ya watu wanadai.

Amesema ili kudhihirisha kuwa anamaanisha hilo, katika operesheni ya kukijenga chama kuanzia ngazi ya chini, maarufu kwa jina la ‘Grassroot Fortification (GF) ya majimbo 30, atakayoifanya wilayani Karatu, Juni 22, 2024 kwa kutumia chopa, ataongozana na Lissu.

Mbowe amesema hayo jana Juni 16, 2024, wakati akiongoza kikao cha mashauriano ya mkoa ya chama hicho.

“Unajua kuna watu wanasema… ooh Mbowe na Lissu wanagombana. Lissu yule ni makamu wangu, mimi ni mwenyekiti siwezi kugombana na makamu wangu kama nilivyosema siwezi kugombana na kuwa chuki za milele na yoyote ndani ya chama hiki.

“Kuwaambia hii namaanisha, ziara ya Karatu tutaifanya na Lissu, wanaongojea chama hiki kipasuke watangojea sana, labda wasubiri Master Mbowe mwenyewe afe, nikifa labda. Ila hiki chama hakifi anayefikiri kinakufa anapoteza muda wake,” amesema.


Atangaza msamaha

Katika hatua nyingine, Mbowe amesema kabla ya operesheni hiyo kuanza, amepanga kukutana na viongozi wote, kwani katika muda mdogo uliobaki kabla ya uchaguzi, silaha ya kwanza ni nguvu yao na umoja wao, kwani wakienda vitani wametawanyika hawataweza kushinda.

Amesema kuna wenzao walikimbilia Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati aliouita wa ‘Mwendazake’ na kuwa inawezekana kuna waliokimbia kwa sababu ya usaliti, ila wengine inawezekana walilazimika kukimbilia CCM kurejesha ama kulinda maisha yao.

 “Mwingine alichagua kukimbilia CCM, kama Lema alivyokimbilia Canada, mimi nilikimblia Dubai lakini dakika za mwisho, kuokoa maisha katikati ya hatari si ujinga.

“Kwa hiyo kama tunahitaji kwenda mbele tutafute wapambanaji wetu walioko ndani ya vita na walio nje ya vita tuwaejeshe tujenge jeshi letu twende mbele.

Pia Mbowe amesema hakuna anayeweza kufanya siasa na uongozi wa kuunganisha watu kama hana roho ya upatanishi, na mtu hawezi kuwa na roho ya kutosamehe wenzake akiwa kwenye siasa.

“Hivi viburi vya watu kujifanya mna roho, chuki zenu yaani mna chuki ndani ya Chadema kuliko ndani ya CCM mnapata wapi? Mimi leo naomba mniruhusu na nitumie mamlaka yangu kusema tutangaziane msamaha katika Kanda ya Kaskazini,” amesema Mbowe.


Akemea ugomvi mitandaoni

Akimtolea mfano Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, Mbowe amesema kumekuwa na makundi ndani ya chama hicho inayohasimiana na kurushiana maneno kwenye mitandao ya jamii. 

“Kuna watu hapa hawasalimiani. Lema mpaka anakimbia anaogopa kugombea Kanda, mmh shughuli ya mitandaoni hiyo. Katandikwa mtandaoni Mwenyekiti wa Kanda mwenye mamlaka ya kanda yake, kiongozi wenu,” amesema.

“Wapo viongozi ambao ni wa kawaida kabisa wa majimbo wa wilaya, kanda na wa kawaida wanaweza  wakamtukana  wakamdhalilisha na familia yake. Hii haiwezi ikakubalika awe na makosa asiwe na makosa, unapokuwa na kiongozi ambaye hamumheshimu hawezi akawaongoza katika safari yenu.  

“Naye Lema Mwenyekiti wa Kanda anapaswa kujua ana vijana wake huku chini wakikosa adabu lazima awaunge awakusanye ni wake. Mimi nawakusanya wote pamoja na matusi yote ninayopigwa,” ameongeza Mbowe.

Amesema wanahitaji amani irejee Arusha na hataki akifika mkoani aambiwe yeye ni wa kundi fulani, kwani yeye hana kundi na watu wote wa Chadema ni wake.

“Siwezi kugombana na Lema au kiongozi yoyote wa chama hiki, ninyi ni familia yangu, tuna malengo ya pamoja. Nitaongea na Lema, kwanza ni mdogo wangu kama alivyosema tuna njia moja, nikigombana na Lema kwenye chama mama yake mzazi ananipigia simu.

“Nikigeuka baba yake ananipigia simu mmeamkaje huko mwanangu, haniambii habari ya Lema ananiambia mwanangu mmeamkaje, unafikiri hiyo maanake ni nini?

“Maana yake ameshakutana kwenye mtandao huo labda Mbowe na Lema hawaelewani,” amesema Mbowe.