Mbowe, Mbatia watua Kiraracha kumzika Mrema
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiteta jambo na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia walipokutana kwenye mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha TLP, Agustino Mrema kijijini Kiraracha Marangu, mkoani Kilimanjaro.
Muktasari:
Leo Alhamisi, Mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama cha TLP, Agustine Lyatonga Mrema (77) unazikwa nyumbani kwake, kijiji cha Kiraracha, Marangu mkoani Kilimanjaro huku viongozi mbalimbali wakifika kuhudhuria mazishi hayo.
Moshi. Mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama cha TLP, Agustine Lyatonga Mrema (77) unazikwa leo Alhamisi, Agosti 25, 2022 nyumbani kwake, kijiji cha Kiraracha, Marangu mkoani Kilimanjaro.
Mrema alifikwa na mauti saa 12.15 asubuhi ya Jumapili Agosti 21, 2022 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa matibabu kuanzia Agosti 16, 2022.
Shughuli za mazishi zimekwisha kuanza nyumbani kwake huku viongozi mbalimbali wa kisiasa na wastaafu wamekwisha kufika kuhitimisha safari ya mwanasiasa huyo mkongwe nchini.
Baadhi ya viongozi hao ni Waziri Mkuu mstaafu John Malecela, Mbunge wa zamani wa Moshi Vijijini, Thomas Ngawaiya.
Wengine ni, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene anatarajiwa kumwakilisha Rais wa wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya Mrema.
Enzi za uhao wake, Mrema aliwahi kuwa waziri wa mambo ya ndani, naibu waziri mkuu, Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM), Temeke (NCCR Mageuzi) na Vunjo kupitia TLP na hadi anafikwa na mauti alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole.