Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbowe, Mnyika, Mdee, Bulaya waibua shangwe kanisani

Freeman Mbowe amesimama wakati akitambulishwa na Mkuu wa KKKT, Dk Fredrick Shoo katika usharika wa Nshara, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, Katibu wa Chadema John Mnyika, Halima Mdee na Ester Bulaya ni miongoni mwa watu walioibua shangwe wakati wa utambulisho wa uwepo wao katika kanisa la kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini usharika wa Nshara, Wilayani Hai.

Hai. Shangwe na vigeregere vilitawala zaidi katika Kanisa la kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini usharika wa Nshara, wilayani Hai wakati Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, Katibu wa Chadema John Mnyika, Halima Mdee na Ester Bulaya walipotambulishwa.

Wanasiasa hao leo Jumapili, Desemba 31, 2023 wameshiriki Ibada maalumu kwa ajili ya harambee ya kukamilisha ujenzi wa awamu ya kwanza ya Kanisa la Betheli usharika wa Nshara Machame ambayo iliongozwa na Mkuu wa Kanisa hilo, Fredrick Shoo, ambapo zinahitaji zaidi ya Sh 1.5 bilioni kukamilisha ujenzi huo.

Askofu Shoo alikuwa akiwatambulisha watu mbalimbali waliofika kwenye ibada hiyo na alipowatambulisha wanasiasa hao, waumini waliokuwapo kanisani humo walilipuka kwa shangwe ikiwa ni ishara ya kuthamini uwepo wao kwenye tukio hilo.

Itakumbukwa Novemba 27, 2020, Mdee,Bulaya na wabunge wengine 17 wa viti maalumu walivuliwa uanachama na Kamati Kuu ya Chadema iliyoketi chini ya uenyekiti wa Mbowe na Katibu Mkuu Mnyika.

Wabunge hao wanadaiwa kwenda kuapishwa bungeni ilhali Chadema hawakupeleka majina yao Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa ajili ya nafasi hizo na chama hicho hakikubaliana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Hata hivyo wanasiasa hao hawakukubaliana na uamuzi wa kuvuliwa uanachama na walikata rufaa Baraza Kuu la Chadema ambalo pia lilibariki kufukuzwa kwao hali iliyowafanya wakimbilia mahakamani kupinga.

Uhusiano wa Mdee na wenzake kwa Chadema umekuwa na msuguano ambao ulizidi zaidi baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kubatilisha uamuzi wa Baraza Kuu la kuwafukuza uanachama wanasiasa hao.

Ushiriki wao katika harambee

Licha ya wanasiasa hao kuwa kwenye msuguano wa kisiasa, leo Mdee na Bulaya wameshiriki kwenye ibada hiyo pamoja na Mbowe ambaye ni mmoja wa waumini wa ushirika huo wa Nshara.

Kabla ya kuanza kwa ibada, Mbowe alikuwa amesimama mlangoni akiwapokea wageni mbalimbali wakiwemo Mdee na Bulaya waliokuja kuungana naye katika harambee hiyo ya ujenzi wa kanisa hilo.

Hata hivyo swali kubwa linaloendelea kuumiza vichwa vya wafuatiliaji wa masuala ya siasa ni nini hatima ya wanasiasa hao ndanni ya Chadema hasa baada ya hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Ibada hiyo pia imehudhuriwa na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia,  Profesa Adolf Mkenda, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Amir Mkalipa, Mbunge wa Hai,  Saashisha Mafuwe pamoja na viongozi wengine wa vyama vya siasa na serikali pamoja na wafanyabiashara mbalimbali nchini.

Katika ibada hiyo, familia ya Mbowe itatoa shukrani katika kanisa hilo.