Chadema yaja kivingine uchaguzi 2025

Dar es Salaam. Licha ya kuwepo matamko mbalimbali kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hakitashiriki uchaguzi ujao ikiwa hayatafanyika mabadiliko ya Katiba, shughuli zinazoendelea chinichini zinaonyesha hali tofauti.

Hata Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ameweka wazi kuwa maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa mwakani na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 yanaendelea na amebainisha baadhi ya mambo yanayofanyika.

Mnyika amekwenda mbali akitoa wito kwa wanachama wa chama hicho wanaotaka kugombea kutangaza nia zao.

Mnyika alibainisha hayo jana, kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi kuhusu masuala mbalimbali ya kisiasa ndani na nje ya chama chake, yaliyofanyika katika ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Tabata jijini Dar es Salaam.

Baada ya kutoridhishwa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, Chadema iliweka msimamo wa kutoshiriki uchaguzi wowote hadi pale Tume huru ya uchaguzi na Katiba mpya vitakapokuwa vimepatikana.

Mei 25, 2021, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, wakati akizungumza na viongozi wa kamati ya utendaji ya mikoa ya Manyara, Kilimanjaro, Tanga na Arusha, alisema chama hicho hakitashiriki uchaguzi wowote kama hakutakuwa na tume huru ya uchaguzi na Katiba mpya.

Oktoba mwaka jana, Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zakaria Obadi alinukuliwa akisisitiza kuwa haitashiriki uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani na uchaguzi mkuu mwaka 2025.

Msimamo huo pia umekuwa ukielezwa mara kwa mara na Mnyika na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Kigaila Benson.

Hata hivyo, jana, Mnyika alisema chama hicho kilishaanza maandalizi ya uchaguzi huo kuanzia mwaka 2021. Alisema wakati wanadai marekebisho ya Katiba, vilevile wanajiandaa na uchaguzi na ndiyo maana wamefanya hizo “Operesheni +255 Katiba mpya.”

Mnyika alisisitiza kuwa wataendelea na maandalizi ya uchaguzi na wakati mwafaka, kamati kuu itatathmini kama maboresho yaliyofanyika yanakidhi haja, kisha watatoa mwelekeo kwa Taifa.

“Kwa sasa nitoe wito kwa Taifa, kama kuna mtu ana dhamira ya kugombea kijiji, kitongoji au mtaa, aende kwenye tawi lake au kata yake, atoe hiyo nia ili ashiriki ujenzi wa chama, ashiriki kwenye mapambano yaliyopo mbele yetu.

“Mwenye nia ya kugombea udiwani, ubunge na urais, ajitokeze kwenye chama kwa mujibu wa mwongozo wa chama wa wagombea. Kwa hiyo, ninachosisitiza hapa ni kwamba kudai kwetu Katiba mpya hakutufanyi tubweteke kusubiri Katiba mpya,” alisema Mnyika.

Kuhusu yeye binafsi kugombea ubunge, Mnyika alisema bado hajafanya uamuzi katika hilo, kwani anasubiri taratibu za ndani ya chama zipite, ndipo ajue hatima yake kama ataendelea kuwa Katibu Mkuu wa Chadema au la.

“Ninachokiona mimi, nikipita jimboni, Kibamba huko, nikipita Ubungo ambako nilishakuwa mbunge, wananchi wanasema rudi ugombee, sasa nasikiliza vilevile sauti za watu, naamini sauti za watu ni sauti ya Mungu,” alisema Mnyika.
 

Ziara za viongozi

Katika kusisitiza hilo, Mnyika alisema baadhi ya viongozi wa Chadema kama vile Kigaila na John Mrema, mkurugenzi wa itikadi, mawasiliano na mambo ya nje, hawaonekani kwa kuwa wanazunguka mikoani kuwatembelea wanachama.

Alisema Chadema ina watu ambao wamejitolea maisha yao kukitetea chama, akitolea mfano viongozi hao waliokubali kuacha familia zao kwa muda mrefu kwenda kukijenga chama hadi ngazi ya chini.

“Mkitaka kujua kama tumefanya kazi kubwa huko Victoria, angalia jinsi CCM wanavyohangaika kurudi Kanda ya Ziwa; Mwanza, Geita na kwingineko, wanajaribu kupeleka nguvu kuzima moto, lakini moto ule hauzimiki kwa sababu unawaka chini kwa chini,” alisema.

Alisema wamefanikiwa kukiweka chama kwenye roho za watu kama chama mbadala, kama chama kilicho tayari kuleta mabadiliko kwenye maisha ya watu na kitakachorudisha matumaini yao yaliyopotea.
 

Maridhiano na CCM

Katika hatua nyingine, Mnyika alisema mazungumzo kati ya CCM na Chadema yamekwama kwa sababu chama tawala kimekataa hoja mbili muhimu za Chadema, ambazo ni kupeleka bungeni muswada wa sheria wa kuendeleza mchakato wa Katiba mpya na muswada wa mabadiliko ya Katiba ili kuwezesha matokeo ya kura za urais kuhojiwa mahakamani.

Baada ya kukwama hapo, Mnyika alisema waliwaambia wenzao wa CCM kwamba wakifanya hili na hili, wako tayari mazungumzo hayo yaendelee wakati wowote. Hata hivyo, alisema tangu wakati huo, CCM haijawatafuta tena.

“Toka wakati huo, wao hawajatutafuta tena kutoa mrejesho kama tunaendelea na mazungumzo au hatuendelei na mazungumzo,” alisema.
Alisema CCM wakitaka kurudi waendelee na mazungumzo, Chadema milango yao iko wazi lakini lazima watekeleze yale ambayo Chadema inadhani ni muhimu kwa ajili ya mustakabali mwema wa demokrasia nchini.

Akizungumzia miswada iliyopelekwa bungeni kubadili sheria za uchaguzi na Tume ya Uchaguzi, Mnyika alisema haitoi suluhisho kwa changamoto za kiuchaguzi.
Kwa mfano, alisema muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi bado unapendekeza wakurugenzi waendelee kusimamia uchaguzi na Rais bado ana nguvu ya kuteua mwenyekiti wa tume hiyo.

Kutokana na hilo, Mnyika alitoa wito: “Umma ujadili hili jambo na Serikali ipate shinikizo la umma kuhusu miswada ya sheria za uchaguzi kwa njia mbalimbali ili kabla kamati ya Bunge haijaanza, Serikali isikie sauti za wananchi.”
 

Ujumbe kwa Rais

Alipoulizwa iwapo akipata nafasi ya kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan atamwambia nini, Mnyika alisema “aisimamie falsafa yake ya 4R kikamilifu kwa kuwa watendaji wake hawafanyi kama vile malengo yake yalivyo kwenye falsafa hiyo.

“Kwa sasa zile 4R, R ya reform (mabadiliko) imevurugwa, wamepeleka miswada mibovu, aiondoe na atoe mwelekeo sahihi wa reform kwenye nchi. Suala la reconciliation (maridhiano), wamemvuruga, mazungumzo kati ya CCM na Chadema yamekwamishwa, kwa hiyo ajenda yake imekwama, aisimamie.

“Na kama hakuna reform na reconciliation, maana yake kutakuwa hakuna rebuilding (kujenga upya). Arudishe nchi katika mkondo sahihi wa zile 4R alizokuwa anazisema, yeye ndiye anaweza kulifanya hilo,” alisema Mnyika.