Mbowe: Siasa zimeathiri familia yangu kwa kiwango kikubwa

Mbowe: Siasa zimeathiri familia yangu kwa kiwango kikubwa

Muktasari:

  • Jana tuliona jinsi gani Mbowe alivyokutana na mkewe, Dk Lilian Mtei katika mazingira nje ya siasa na kisha wakaoana mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Dar es Salaam. Jana tuliona jinsi gani Mbowe alivyokutana na mkewe, Dk Lilian Mtei katika mazingira nje ya siasa na kisha wakaoana mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Hata hiyo, Mbowe katika kipindi cha mahojiano kinachoandaliwa na kuendeshwa na Tundu Lissu na Nadj Khamis, kinachoitwa ‘Speaking Out With Tundu Lissu, anasisitiza kuwa pamoja na yeye kuchukua mkondo wa kisiasa, mkewe huyo hakujihusisha na shughuli za siasa.

“Mimi nimekuwa Chadema kama mwasisi na pia kama kijana niliyekuwa nasaidia chama kusimama. Mke wangu si mwanasiasa, ni mwanasayansi zaidi. Hata Mzee Mtei (baba yake) tulikuwa tunakubaliana mambo ya kisiasa tu,” alisema akifafanua jinsi ambavyo uhusiano wake na mkewe Dk Lilian haukutokana na masuala ya siasa.

Akeieleza jinsi alivyokuwa mwenyekiti wa tatu wa chama hicho baada ya Edwin Mtei na Bob Makani, Mbowe alisema yeye hajawahi kuomba kuwa mwenyekiti.

“Mwaka 2004 nilipokuwa mwenyekiti wa tatu baada ya Mzee Bob Makani, walinipendekeza wajumbe wa kamati kuu, wazee mbalimbali wa chama wakisema, hiki chama sasa apewe Mbowe,” ameeleza.

Anasema walimpendekeza kutokana na historia yake na jinsi alivyojitoa kwa chama hicho. Hata hivyo, anasema kabla ya kuwakubalia aliwapa masharti matatu.

“Sharti la kwanza niliwaambia tufanye mabadiliko makubwa katika chama chetu, sharti la pili lazima Dk Willibrod Slaa (ambaye sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Sweden) awe katibu mkuu wa chama,” alisema.

Amesema alitoa sharti hilo kwa kuwa wakati huo katibu mkuu alikuwa anachaguliwa na mkutano mkuu.

“Demokrasia ni nzuri lakini najua ilivyokuwa vigumu kupata watendaji wa kisiasa kwa kupitia kura za jumla. Ndiyo maana nilitaka huo utaratibu ubadilishwe, kwa sababu mtu anaweza tu akashangiliwa kwenye majukwaa akapigiwa kura, lakini hakuna meritocracy (uwezo),” alisema.

Kabla hata hajawa mwenyekiti, anasema alianza kukijenga chama hicho kilichoonekana kusinzia.

“Tukaenda vyuo vikuu kutafuta wanachama wenye mwelekeo wa kuwa viongozi. Nilianza harakati nikiwa kiongozi wa wabunge wanne nikiwemo mimi, Dk Slaa, Philemon Ndesamburo (na Dk Walid Kabourou) na Mbunge pekee wa viti maalum wakati huo akiwa Grace Kihwelu.”


Ajivunia kuikuza Chadema

Baada ya kugombea urais mwaka 2005 na kuibuka na kura 668,756 (sawa na asilimia 8.88), Mbowe hakuingia tena bungeni hadi mwaka 2010 alipogombea tena lakini alikitumia kipindi hicho kimkakati.

“Kipindi hicho nilikwenda kusoma, nikaenda Hull University Uingereza, nikasoma shahada ya sanaa katika filosofia, siasa na uchumi.

“Wakati huo pia tukafanya mabadiliko makubwa kwenye chama. Tukabadilisha sera ya chama, tukatengeneza mabaraza ya chama, tukatengeneza katiba ya chama, tukatengeneza kanuni na miongozo ya baraza,” alisema.

Alisema wakati huo ndio alitengeneza mazingira ya kushawishi wanasiasa mbalimbali kujiunga na chama hicho.

“Nikawaambia wenzangu, siri ya kukuza chama chetu ni kufungua milango, Chadema isifikiri kwamba tunajitosheleza. Kuna mamilioni ya watu wenye uwezo kuliko sisi, ambao tunaweza kuwatengenezea nafasi wakaja kufanya siasa safi Chadema.

“Kwa hiyo nikaanza kuwinda watu, ndivyo nilivyokupata wewe (Tundu Lissu), ndivyo nilivyowapata kina Marando (Mabere), kina Profesa Safari (Abdallah),” anasema.

Aliendelea kusema katika ungozi wake amekuwa akiachia wenye uwezo kugombea urais ukiwemo mwaka 2010 ambao Dk Slaa aligombea urais.

“Mwaka 2015 tukasema tumepeke Edward Lowassa, sasa hayo yaliyotokea baadaye, tusipotezeane muda. Baadaye na wewe (Lissu) ukaja 2020 ukafanya wajibu wako kwa ajili ya chama,” alisema.


Miaka mitano ya majaribu

akijibu swali kuhusu kipindi kigumu kwake, Mbowe alisema miaka mitano ya hayati John Magufuli imekuwa migumu kwa chama hicho kuliko wakati wowote ule. Hata hivyo amesema kipindi hicho kimewawezesha kujipima.

“Watu wamejaribiwa. Tumeweza kujua nani ni wagumu na nani wepesi kuvunjika, nani tuko naye na nani hatuko naye. Ni kipindi ambacho pamoja na madhara yote tuliyopata tumepata mafunzo mengi ya kisiasa,” anasema.

Alipoulizwa kuhusu jambo unalojutia, Mbowe aligusia jinsi viongozi na makada waliowapata miaka ya nyuma wanavyoshawishiwa kuhamia CCM.

“Suala kama la wabunge kuondoka kwenye chama halinifurahisi, halafu wakiondoka wanatoa umbea. Hivi vitu vinavunja moyo, lakini vikitokea vinaonyesha kuwa tunalazimika kujitafakari zaidi kwenda mbele zaidi. Laiti vijana wetu wengi wasingekuwa hivyo tungekuwa mbali zaidi,” anasema.


Kuhusu maspika Bunge

Alipoulizwa kuhusu Bunge la Jamhuri ya Muungano na jinsia anavyowalinganisha maspika tangu mfumo wa vyama vingi nchini, Mbowe alianza kwa kumtaja Pius Msekwa aliyekuwa Spika wa Bunge la nane.

“Mzee Msekwa alikuwa ni scholar (msomi) na alikuwa mwelewa na ni mwandishi mzuri wa vitabu. Utotoutoto, ujinga na upumbavu, fitna majungu, mambo ya Kiswahihi alikuwa hana,” alisema Mbowe.

Alisema licha ya nguvu ya upinzani wakati wake kuwa ndogo, lakini hakuvinyanyasa vyama hivyo.

“Nikija kwa mama Anne Makinda alikuwa very accommodative (mtu anayezingatia), mwanamke mwadilifu, anasikiliza pande zote, anaweza kupendelea chama chake lakini kwa uungwana. Kwa hiyo Bunge likawa na heshima.

“Wakati mwingine mnaweza mkasema hebu tuachane na vyama, hii ni ajenda ya kitaifa, tufanye kazi pamoja kama Watanzania,’ alisema.

Alipofika kwa Spika Job Ndugai, Mbowe alisema hataki kumzungumzia. Alipoulizwa na Lissu kwa nini alisema:

“Kwanza ni Spika aliyeonyesha bila shaka yoyote kuwa na chuki zilizopita kwangu. Mpaka kuna siku nilimpelekea ujumbe, ‘Ndugai nimekukosea nini? Kwa nini hili liko binafsi?


Gharama ya kuwa mpinzani

Akizungumzia gharama za kuwa mpinzani, alisema gharama ni kubwa tangu kwenye fedha hadi familia.

“Mimi familia yangu imeathiriwa sana na harakati hizi. Watoto wangu sionani nao, mke wangu sionani naye, tunapishana wakati mwingie uwanja wa ndege.

Familia yangu kubwa hawanioni kwa sababu niko kwenye siasa. Wengine wenye moyo mwepesi wananiuliza, baba kwa nini uwe kwenye siasa, nawaambia hapana, huu ni wito. Kuwepo kwangu kwenye siasa si utumishi, ni wito. Nasukuma siasa kwa sababu wito wangu uko pale,” alisema.

Aliongeza: Tumepata hasara ya kibiashara, tumepata hasara ya kimaisha, hata ndugu zangu hawawezi kupata kazi, ukishaitwa Mbowe unaonekana mgeni. Nimepata gharama kubwa wala siwezi kuipima kwa fedha.”