Mbowe: Tulikubaliana na Rais Samia kufanya siasa za kujenga nchi

Mwenyekitii wa Chadema, Freeman Mbowe

Muktasari:

  • Mwenyekitii wa Chadema, Freeman Mbowe amesema waliketi na Rais Samia Suluhu Hassan na kukubaliana kufanya siasa za kujenga Taifa ikiwa ni pamoja na kufuta kesi zote za kisiasa zilizokuwepo mahakamani.


Shinyanga. Mwenyekitii wa Chadema, Freeman Mbowe amesema waliketi na Rais Samia Suluhu Hassan na kukubaliana kufanya siasa za kujenga Taifa ikiwa ni pamoja na kufuta kesi zote za kisiasa zilizokuwepo mahakamani.

Ameeleza hayo leo Ijumaa Agosti 12, 2022 wakati akizungumza katika kongamano la baraza la vijana lililofanyika kitaifa mkoani Shinyanga akibainisha kuwa baada ya kutoka gerezani alienda Ikulu kufanya mazungumzo na Rais Samia na wakakubaliana kufuta kesi zote za kisiasa zilizopo.

Mbowe amesema kuna wanasiasa zaidi ya 400 walikuwa gerezani mwaka 2020 baada ya uchaguzi mkuu na wengi walikuwa  vijana wa Chadema na wapo waliofungwa maisha hivyo walikubaliana kufutwa kesi na wengine kusamehewa.

"Hawa watu waliokuwa wamefungwa walibambikiwa kesi na tuliamini hivyo na ndio maana tuliomba mazungumzo yafanyike ili watu wawe huru.”

"Kwa yote yaliyotokea sina hasira, sina kisasi, sina kinyongo nitabaki kuwapigania watanzania wenzangu siku zote, nilikaa kimya kwa sababu kila jambo lina wakati wake kuna baadhi ya watu wamesema mara hili mara lile…, lakini nina taasisi nisopozungumza mimi taasisi itazungumza,” amesema Mbowe.

Mbowe amewasihi viongozi wengine wa kisiasa kuendelea na siasa za ushindani kwa ustaarabu na upendo.

Katika maelezo yake Mbowe amesema Katiba Mpya na tume huru lazima izingatiwe, “na Tanzania inatakiwa iige nchi nyingine kama Kenya wanafanya uchaguzi wa uhuru, matokeo yanatangazwa kwa uwazi. Watanzania tunatakiwa kuiga mfano huu tuna mengi ya kuiga.”