Mbozi yapata clean sheet, DC na DED wapongezwa

Mbozi. Shule mpya ya Msingi ya DR. Samia S. H iliyopo Lutumbi katika Mamlaka ya Mji mdogo Mlowo Wilayani Mbozi mkoani Songwe imekuwa kivutio katika mbio za Mwenge wa Uhuru 2023.

 Shule hiyo ambayo imezinduliwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhueu Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim imewavutia watu wengi waliofika katika uzinduzi huo kutokana na mandhari yake ya kuvutia.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Ester Mahawe ujenzi wa shule hiyo umegharimu Sh538.5 milioni kupitia Mradi wa Kuboresha Sekta ya Elimu (BOOST) kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Amesema kuwa lengo la mradi huo ni kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani shule mama ya Msingi Lutumbi yenye wanafunzi 2,259 ili kuongeza ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji.

"Tunakuomba utufungulie mradi wa shule hii ili wanafunzi waanze kusoma"

Akizungumza kabla ya kuzinduzi shule hiyo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Abdalla Shaib Kaim amewataka wanafunzi ambao watatumia shule hiyo wajitahidi ili matokeo yaakisi uwekezaji uliofanywa na Serikali.

Ameupongeza uongozi wa Halmashauri hiyo kwa kusimamia ujenzi wa shule hiyo ambayo amesema umekidhi viwango na ubora.


 Mbozi yapata 'clean sheet'

Akizungumzia miradi ya maendeleo iliyokaguliwa na Mwemge, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaibu Kaim amesema kuwa wameridhishwa na miradi yote huku akisema kuwa wilaya hiyo imetoka na ‘clean sheet’.

“Tumepitia miradi yote. Nipende tu kusema kuwa Mbozi mmetisha, Mkuu wa Wilaya umetuheshimisha sana. Tumetembelea na kukagua miradi yote nane Mbozi mmetoka na ‘clean sheet’ safi kabisa” amesema Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge kitaifa.

Amesema kuwa utekelezaji wa miradi kwa viwango ni njia mojawapo ya kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan hali ambayo itasaidia kupata miradi mingine.

Mwenge wa Uhuru ukiwa wilayani Mbozi umetembelea miradi nane yenye thamani ya Sh8.2 bilioni huku ukikimbizwa Kilometa 130 katika wilaya hiyo.

Wilaya ya Mbozi imekuwa ya tatu kukimbiza Mwenge wa Uhuru katika mkoa wa Songwe ambapo ilianza Wilaya ya Momba Septemba 2 ikifuatiwa na Wilaya ya Songwe.

Akizungumza wakati wa kupokea Mwenge huo Septemba 2 mwaka huu katika eneo la Kamsamba, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk Francis Michael alisema kuwa Mwenge huo utatembelea miradi 47 katika mkoa huo yenye thamani ya Sh15.5 bilioni na utakimbizwa kilometa 722 katika mkoa huo kabla ya kukabidhiwa katika Mkoa wa Mbeya Septemba 7 mwaka huu.