Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbu wa mijini tishio jipya homa ya dengue

Muktasari:

  • Wanasayansi wamesema kuna tishio jipya la homa ya dengue, kutokana na kuongezeka kwa uzalianaji wa mbu aina ya ‘Aedes’ kutokana na mabadiliko ya tabianchi, katika maeneo mbalimbali, hasa ya mijini.

Dar es Salaam. Magonjwa yanayoambukizwa na mbu katika maeneo mbalimbali, hasa ya maeneo ya mijini, yametajwa kuongezeka katika ukanda wa Afrika.

Hali hiyo imewafanya wanasayansi kutoa wito wa dharura kwa watafiti kuja na majibu ya kutosha, ili kukabiliana na tishio hilo linalosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Magonjwa hayo ni dengue, Zika, chikungunya na homa ya manjano yanayoambukizwa na mbu anayejulikana kwa jina la ‘Aedes’.

Kutokana na tishio hilo, jumla ya Sh4.1 bilioni zimetolewa na Umoja wa Ulaya kwa taasisi 25 nchini, ili zianze kufanya tafiti kuhusu mbu huyo na kuwajengea uwezo wataalamu kuhusu mbinu za kumkabili.

Wamesema wakati idadi ya wagonjwa wa malaria ikipungua, watu wanaougua homa ya dengue wanazidi kuongezeka na tayari zaidi ya asilimia 17 ya nchi za Afrika zimeathiriwa na ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Afrika ni miongoni mwa kanda nne zinazoongoza kwa kuathiriwa na dengue, ikiwa na wagonjwa 171,991 na vifo 753 mwaka 2023.

Shirika hilo limesema pia watu bilioni 3.9 waishio mijini katika nchi 129, wapo hatarini kuugua homa ya dengue.

Hayo yamesemwa Agosti 26, 2024 na Dk Raman Velayudhan, mkuu wa kitengo cha afya ya umma ya mifugo, udhibiti wa vekta na mazingira katika Mpango wa kimataifa wa magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika wa WHO, wakati wa ufunguzi wa kongamano la kimataifa kuhusu maendeleo ya ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa yanayoenezwa na Aedes.

Amesema ni vyema kufanyia kazi njia bora za kukabiliana na magonjwa hayo, ili kuepuka madhara ya kiafya na gharama zinazotokana na wimbi la pili la magonjwa hayo.

"Huu ni mkutano mkubwa kwa wanasayansi wa Kiafrika unaolenga kuzingatia zaidi juhudi za kupambana na magonjwa ya mijini ikiwemo dengue, ambao utaongezeka kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

“Kwa kweli tunatakiwa kufanya kazi zaidi na kuhakikisha tunapunguza vifo vya watu wa mijini kwa ugonjwa wa dengue, tofauti na malaria,” amesema Dk Velayudhan.

“Kwa kawaida homa ya dengue ina awamu tatu katika maisha ya binadamu. Awamu ya pili ni hatari zaidi ukilinganisha na ya kwanza na ya tatu, kwa sababu inaathiri idadi kubwa ya watu wenye matatizo zaidi ya kiafya, tusisubiri itokee,” amesema Dk Velayudhan.

Amesema juhudi za kuipunguza dengue hadi kufikia sifuri zinahitajika kwa kuhusisha jamii, ili kujilinda na kuhakikisha watoto wa shule wanatumia na kupaka dawa ya kuua mbu kabla ya kwenda shuleni.

Akitoa mada kuhusu hali ya kimataifa ya homa ya dengue na mpango wa kimataifa wa ‘arbovirus’, Dk Velayudhan amesema inaonyesha kuanzia Januari hadi Julai mwaka huu, kulikuwa na nchi 109 zilizothibitika kuwa na maambukizi ya dengue.

Amesema tathmini hiyo inaendelea na huenda maambukizi yakatokea katika nchi nyingine ambazo bado hazijanaswa na mifumo rasmi ya ufuatiliaji.

“Jumla ya wagonjwa 148,871 na vifo 105 viliripotiwa na WHO kutoka nchi 20 hadi kufikia Julai 2024. Idadi kubwa zimerekodiwa nchini Malaysia, ikiwa na waathirika 83, 131,” amesema Dk Velayudhan.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI), Dk Honorati Masanja amesema tayari wameandaa kikao kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hilo na kuwa changamoto hiyo si Tanzania pekee, bali hata sehemu nyingine za dunia ambako mbu hao hawafuatiliwi, ili kuendeleza uelewa wa kisayansi.

Katika siku tatu zijazo, tutashiriki ujuzi, kuchunguza zana na teknolojia za kisasa na kuunda ushirikiano mpya ili kuimarisha jitihada zetu dhidi ya magonjwa yatokanayo na Aedes," amesema Dk Masanja.

Mkurugenzi wa Utafiti katika Taasisi ya Utafiti wa Umma ya Ufaransa (IRD), Profesa Vincent Corbel amesema mkutano huo utakuza zana mpya na za ubunifu zitakazosaidia kuboresha ufuatiliaji wa kudhibiti mbu na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi na nchi.