Mbunge aangua kilio bungeni

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Lindi, Maimuna Pathan akiangua kilio bungeni leo Aprili 12,2023 wakati akichangia mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya waziri mkuu na ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024.

Muktasari:

  • Uvamizi wa wanyama waharibifu umeendelea kusumbua kwenye maeneo mbalimbali hali iliyomfanya Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Maimuna Pathan kuangua kilio wakati akielezea madhara ya wanyama hao mkoani Lindi.

Dar es Salaam. Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Maimuna Pathan  ameangua kilio bungeni wakati akielezea jinsi tembo wanavyowasumbua na kusababisha mauji ya watu mkoani Lindi.

Ameyasema hayo leo Aprili 12,2023 wakati akichangia mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya waziri mkuu na ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024.

Amesema wananchi wa wilaya ya Liwale na Nachingwea mkoani Lindi,  wamekuwa wakiuawa na tembo kwa nyakati tofauti.

Maimuna amesema kutokana na maeneo hayo kuvamiwa na tembo kunauwezekano wa kutokea njaa kubwa kwenye maeneo hayo.

Amesema hali katika baadhi ya vijiji kwenye wilaya hizo ni mbaya na kuwa wamepelekwa askari wachache kwenye maeneo hayo ambao hawawezi kukabiliana na changamoto hiyo.

Amehoji kama katika shamba moja wakivamia tembo 50, askari wawili wataweza kufanya kazi ya kuwafukuza wanyama hao waharibifu.

“Juzi kuna kijana amefariki ameuwawa na tembo, mchana kweupe maeneo ya Kunichile. Amejitoa nyumbani aende kuangalia shamba lake kama kumebakia mahindi kidogo ama alizeti, amefika kule yeye ndiye wamemfanya chakula,”amesema.

Mbunge huyo amesema walitegemea ingetokea hali ya dharura ya kupeleka helikopta lakini licha ya kulizungumzia sana hakuna helikopta iliyopelekwa kwa ajili ya kufukuza wanyama hao.

Hata hivyo, amesema angeuawa ndovu mmoja, wangepelekwa maaskari na helikopta kwenye eneo hilo kwenda kuwaletea wananchi vurugu.

“Mimi najiuliza na wananchi wa kule wanajiuliza ndovu na binadamu ni nani muhimu? Inafikia hatua wanasema mtapigiwa kura na ndovu. Sio kwamba wanaongea hivyo kwa kutulaghai ni hasira na uchungu walionao,”amesema.

Amesema walitegemea hali ya dharura ingechukuliwa kwenye maeneo hayo kwasababu tembo wanaoingia ni wengi, wanavamia tembo zaidi ya 50 lakini askari wanaopelekwa ni wawili ambao hushindwa na kukimbia.

Amesema wabunge wamekuwa wakiripoti hali hiyo lakini hakuna hatua za dharura zinazochukuliwa.