Mbunge alia mitaa zaidi ya 10 jimbo la mjini kukosa umeme

Muktasari:

  • Mbunge wa Kondoa Mjini, Ali Makoa amesema baadhi ya mitaa katika jimbi hilo haina umeme wala nguzo, huku akisema mtaa mmoja uliwekwa umeme wa Rea, lakini takriban miaka miwili sasa haujawashwa.

Dodoma. Mbunge wa Kondoa Mjini (CCM), Ali Makoa amelieleza Bunge la Tanzania kwamba mitaa zaidi ya 10 katika jimbo lake  haina umeme, wala nguzo za umeme.

 Amesema jitihada za kutoa mafunzo ya ujuzi kwa vijana haziwezi kufanikiwa kama majimbo ya mjini kama lake, mitaa mingi haina umeme wala nguzo.

Makoa amesema hayo leo Alhamisi Aprili 4, 2024 wakati akichangia mjadala kuhusu taarifa ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2024/2025.

“Serikali iongeze nguvu kuhakikisha miundombinu inajengwa. Ninatoa mfano mmoja, mimi niko jimbo la mjini Kondoa lenye kata nane na mitaa 36, vijana wa mjini wanatarajia wapate wawekewe miundombinu mizuri kwa ajili ya kuyajenga maisha yao,” amesema.

Makoa amesema bado utekelezaji wa miradi ya umeme ipo chini, hasa kwa wao walioko kwenye majimbo ya mijini.

“Umeme ni ajira kwa vijana na umeme unarahisisha vijana kujitegemea katika shughuli zao mbalimbali, sasa ukikuta mitaa ya mjini hamna umeme, halafu tunataka vijana waweze kujiajiri, maana yake mjini hatuna mashamba, mjini tunatarajia tupate umeme.

“Miundombinu ikiboreshwa ndio vijana wanaweza wakajiajiri na hata huo ufundi tunaokwenda kuwapa, hizi miradi za kuwaongezea ujuzi vijana kama miundombinu haijakaa vizuri kwenye majimbo yetu, basi moja kwa moja hatutafikia malengo,” amesema.

Makoa amesema watoto wanapelekwa kujifunza ufundi, lakini wakirudi mitaani wanakutana na miundombinu hafifu ya umeme ambayo wanashindwa kujiendeleza.

“Tukiongelea vijana wa jimbo la Kondoa Mjini, kuna mitaa zaidi ya 10 hata nguzo ya umeme hakuna, sasa utawapeleka vijana hawa kwenda kujifunza kuchomelea au kujifunza saluni na vitu vingine   wanawezaje kuutumia ujuzi wao wakati umeme hakuna.

“Mitaa haina nguzo za umeme, mitaa haina umeme kwa maana hiyo hata ukipeleka ujuzi kwa vijana wa kule hawawezi kutekeleza majukumu yao kwa sababu hawana miundombinu ya umeme,” amesema.

Akiendelea kuchangia, mbunge huyo amesema:“Lakini cha ajabu unakuta kuna jimbo lina vijiji 84 na vijiji vyote vina umeme, lakini mitaa 36 hakuna umeme.”

“Sasa vijana wa mjini hawana mashamba, wanatarajia wachomelee, wanatarajia wafungue saluni, wanatarajia kuuza maduka na vinywaji vya baridi, hakuna umeme watafanyaje.

“Iko mitaa ambayo ilipata bahati za mradi wa umeme wa REA ni muda umeenda sana kwenye Kata ya Suluke, umeme ule mkandarasi hajawasha umeme ni mwaka karibu wa pili huu. Miundombinu imekamilika, lakini umeme haujawaka.

“Lakini katika hili kuna mtaa ambao umerukwa na nguzo za umeme zipo zimekaa pale hazina kazi na nimeulizia nikaambiwa kwamba zitaondolewa pale zitapelekwa kwenye jimbo lingine vijijini,” amesema.

Makoa ameonyesha kushangazwa kwa nguzo kupelekwa kwenye mtaa, lakini baadaye zinataka kuondolewa kupelekwa vjijini.

“Kuna haja ya kuliona hili vizuri, ukienda kukuza vijiji ukaacha miji, miji ikabaki haina umeme bado hatujatendea haki hii miji,” amesema.