Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Naibu Waziri hataki mchezo upatikanaji umeme

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga mwenye shati nyekundu akipewa maelekezo ya utekelezaji mradi wa upitishaji umeme chini ya ardhi kutoka Ilala hadi kituo cha Kurasini jijini hapa.

Muktasari:

  • Serikali imetishia kutowapa au kutohuisha mikataba makandarasi wanaosambaza vifaa vya ukarabati wa umeme wasiotekeleza kikamilifu majukumu yao.

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea na maboresho ili kuongeza uzalishaji wa umeme nchini, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameagiza hatua za kinidhamu na kisheria zichukuliwe kwa makandarasi wanaosambaza vifaa kwa ajili ya ukarabati njia za umeme wasiotimiza majukumu yao

Agizo hilo amelitoa leo, Ijumaa Desemba 1, 2023 Dar es Salaam alipofanya ziara katika kituo cha kupoza umeme cha Ilala kwa akili ya kukagua mradi wa ujenzi wa njia ya chini ya kupitisha umeme kutoka kituoni hapo hadi Kurasini.

Mara baada ya kukagua mradi huo uliofikia asilimia 68.14 sasa, Kapinga amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kupitia idara ya usambazaji kuhakikisha makandarasi waliopewa mikataba kwa ajili ya kusambaza vifaa vya matengenezo wanatimiza wajibu huo kwa wakati.

Ametaka mkazo uwekwe ili vifaa hivyo vipatikane kwa wakati na hivyo kuwezesha matengenezo kufanyika kwa zile njia za umeme zinazosumbua.

"Vifaa vimekuwa vinasumbua, wasambazaji wengine wapo kwa muda mrefu, wanasumbua na hawachukuliwi hatua tutaanza nao kwa sababu tumewaelekeza kuwa Dar es Salaam ni mjini ni lazima umeme uwe wa uhakika,” amesema na kuongeza;

“Kama tunafanya uzembe kwa kuwapa wasambazaji wasiokuwa na uwezo au wazembe tutaanza na wanaohusika," amesema

Naibu Waziri huyo amebainisha kuwa hata kama nchi ina umeme wa kutosha lakini ikiwa maboresho ya njia za umeme hayafanyiki, changamoto ya kukatika umeme itaendelea.

Ameitaka idara hiyo kufanya kazi bila kupepesa macho na ikiwa mkandarasi aliyepewa kazi hatekelezi kwa wakati asiongezwe mkataba mwingine pindi anapomaliza ule wa awali.

Kwa mujibu wa Judith, vifaa vinavyohitajika ni nguzo, transfoma, nyaya na vyote vinatakiwa kufika sehemu ya mradi kwa wakati.

 “Kuna taarifa ya baadhi ya njia ambazo zilipaswa kukarabatiwa lakini karibu mwaka mzima sasa hazijakarabatiwa, tunaanza kuwachukulia hatua mmoja baada ya mwingine kwa sababu hakuna Mtanzania anayeweza kukaa bila umeme kwa nyakati kama hizi, hatutaweza kuvumilia kutoboreshwa kwa njia za umeme kutokana na watu wachache."

Amesema maboresho ya njia hizo ni muhimu kwa sababu umeme una mchango mkubwa katika shughuli za kiuchumi.

Akizungumzia mradi wa maboresho kutoka Ilala hadi Kurasini, Judith amedokeza kuwa unalenga kuimarisha upatikanaji umeme katika baadhi ya maeneo ya Temeke, Kurasini Mbagala na Kigamboni, baada ya maeneo hayo kuwa na tatizo la upatikanaji umeme, kutokana na ongezeko la makazi ya watu.

Jitihada hizo zinaenda sambamba na uboreshaji wa kituo cha kupoza umeme Mbagala.

Awali alipokuwa akisoma taarifa mbele ya Naibu Waziri huyo, Mhandisi wa mradi huo, Nicholaus Antony amesema mradi huo unaotarajiwa kukamilika Machi mwakani na ulianza Januari mwaka huu.

Amesema kwa sasa ujenzi umefikia asilimia 68.14 huku akieleza kuwa kukamilika kwake kutaimarisha upatikanaji umeme katika wilaya ya Temeke.

"Hii utafanya maeneo mengi ya wilaya hiyo kuwa na uwezo wa kupokea umeme kutoka Ubungo kupitia Ilala kwenda Kurasini au Kinyerezi, Kipawa hata Kurasini hii utafanya kukiwa na tatizo upande mmoja wapate umeme kupitia upande mwingine," amesema Antony.

Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya TDEA kutoka nchini China.