Rungwe kupata umeme wa joto ardhi 2024

Muktasari:

  • Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea ziwa hilo, Meneja Mkuu wa TGDC, Mathew Mwangomba, amesema tafiti za awali zinaonyesha kuwa Ziwa Ngozi lina uwezo wa kuzalisha megawati 70.

Rungwe. Kampuni ya Undelezaji Jotoardhi nchini (TGDC), inakusudia kuanza uzalishaji wa umeme megawati tano, kama sehemu ya kukabiliana na changamoto ya upungufu wa nishati hiyo.

Uzalishaji huo unaotokana na jotoardhi, unakusudiwa kuanza mwakani  katika  Ziwa Ngozi lililopo wilayani hapa.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea ziwa hilo, Meneja Mkuu wa TGDC, Mathew Mwangomba amesema tafiti za awali zinaonyesha kuwa ziwa hilo lina uwezo wa kuzalisha megawati 70.

Amesema uchorongaji wa kisima cha kwanza cha majimoto kwa ajili ya kuzalisha umeme katika eneo hilo, tayari unaendelea sambamba na kuendelea kwa tafiti na upimaji wa sampuli ili kujiridhisha na ifikapo 2024, uzalishaji unaanza.

"Serikali imetuwezesha Sh20 bilioni hivyo tutahakikisha tunafanya kazi ipasavyo bila kumuangusha Rais, kwani TGDC tuna watalaamu ambao Serikali imewagharamia kwa kuwasomesha nje ya nchi na wana ujuzi wa kutosha,” amesema Mwangomba.

Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Jafari Haniu amepongeza kampuni hiyo kwa kuwapa uelewa watumishi na wananchi kuhusu teknolojia hiyo ya uzalishaji umeme kwa kutumia jotoardhi.

Haniu amesema Serikali ya wilaya ipo tayari kutoa ushirikiano katika hatua zote za utekelezaji wa mradi huo na endapo watakuwa na changamoto yeyote wasisite kufika ofisi kwake na kuomba ushauri ili utatuzi wa haraka upatikane na mradi uendelee.

Naye, Diwani wa Kata ya Isongole, Mwalingo Sothe amesema uwepo wa mradi huo umesaidia baadhi ya vijana kujipatia ajira za muda na kuweza kuendesha maisha yao, tofauti na mwanzo walikuwa wanasubiria kazi za msimu hadi msimu zinazotokana na kilimo pekee.

Kwa upande wake msimamizi wa mradi huo, Fatumati Mzava amesema wanategemea kuchimba visima vitatu kwa ajili ya uzalishaji wa umeme ambapo kwa kuanza wameanza na kimoja katika Kata ya Isongole wilaya ya Rungwe na vingine viwili vitachimbwa Mbeya vijijini.