Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbunge alia tembo kuvamia Mwanga

Mbunge alia tembo kuvamia Mwanga

Muktasari:

  • Wanyama hao ambao wamedaiwa kuharibu mazao ya aina mbalimbali katika mashamba ya wananchi wametajwa kuongezeka ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Mwanga. Mbunge wa Jimbo la Mwanga mkoani Kilimanjaro, Joseph Tadayo amesema tatizo la uvamizi wa wanyama pori aina ya tembo kwa sasa  limegeuka kuwa janga katika wilaya hiyo na kwamba wanasubiri kauli ya Serikali, kujua ni nini cha kufanya ili kukabiliana na tatizo hilo.

Tadayo ameyasema hayo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM, kwa wajumbe wa mkutano mkuu, ambapo amesema, maeneo ambayo yamekumbwa na tatizo hilo, wananchi wameshindwa kuendesha shughuli za uzalishaji.

"Awali tulidhani tatizo hili la Tembo litakuwa la muda lakini sasa tunakoelekea, limegeuka kuwa janga na hatujui litaisha lini kama hatua hazitachukuliwa, tunatarajia kauli thabiti ya serikali hivi karibuni, kwamba tunafanya nini,"amesema Tadayo.

"Nitoe pole kwa maeneo yote ambayo wamekumbwa na tatizo la uvamizi wa tembo, ambapo suala la uzalishaji limekuwa gumu, lakini pia nitoe pole zaidi kwa wale ambao wamepoteza ndugu, jamaa na marafiki kutokana na janga hili la Tembo na kwa wale waliojeruhiwa, lakini nitoe pole kwa wananchi wote kwa kuwa mmekaa kwa hofu, kutokana na janga hili."

Aidha Tadayo amesema, Serikali ina mpango wa kufungua lango la kaskazini la Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, hatua ambayo wanaamini inaweza kupunguza tatizo la uvamizi wa tembo katika maeneo ya makazi ya watu.

"Miongoni mwa miradi itakayotekelezwa kwa haraka ni ufunguaji wa lango la kaskazini la Hifadhi ya Mkomazi, ambapo watalii watakuwa wanaweza kuingilia Same wakatokea Mwanga, au kuingilia Mwanga wakatokea Same."

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Nec) Mkoa wa Kilimanjaro, Seleman Mfinanga amesema kwa sasa wanachohitaji wananchi ni maendeleo na kwamba watashirikiana viongozi wa chama na Serikali, kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa.

"Ili mwaka 2025 kazi kwetu iwe rahisi ni lazima tuhakikishe tunatekeleza yale tuliyowaahidia wananchi na kushughulika na changamoto zinazowakabili,"amesema Mfinanga