Mbunge aliyetaka pasipoti kuingia Zanzibaar azua jipya

Mbunge wa Konde (ACT-Wazalendo), Mohamed Said.

Muktasari:

  • Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika na baadaye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alikemea ubaguzi.

Dodoma. Mbunge wa Konde (ACT-Wazalendo), Mohamed Said Issa aliyetaka wananchi wa Tanzania Bara (Watanganyika) waingie Zanzibar kwa pasipoti, amezua lingine la ubaguzi akikataa taarifa tatu za kumtambua yeye ni Mtanzania.

Hayo yametokea bungeni leo Mei 15, 2024 wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka wa fedha 2024/2025, yaliyowasilishwa bungeni na waziri mwenye dhamana, Hamad Masauni.

Wabunge Anatropia Theonest (Viti Maalumu), Godwin Kunambi (Mlimba) na Conchesta Rwamlaza (Viti Maalumu) wamempa taarifa mbunge huyo wakieleza yeye ni Mtanzania, lakini amekataa kuzipokea.

Mbali na kukataa kupokea taarifa hizo tatu, mbunge huyo amewataka wabunge wamtafute awafafanulie kwa nini anataka kuwe na pasipoti kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.

“Nataka nizungumzie suala zima la ubaguzi, leo vyombo vya ulinzi na usalama viko hapa, kwa hiyo ningetamani sana kulielezea jambo hili.”

“Sisi Wazanzibari tumekuwa tukibaguliwa kwenye mitandao, kwenye vyombo vya habari, kwenye mikutano, hatujui sababu ni nini. Sasa jambo hili nilitamani nilichangie leo ili vyombo vya ulinzi na usalama vijue,” amesema.

“Hapa tumekuwa tukisikia Rais (Samia Suluhu Hassan) akibaguliwa kwa Uzanzibari wake na mwisho anaambiwa amekopeshwa kutoka kule Zanzibar.”

“Hili jambo si sahihi, mimi kama Mzanzibari kwa sababu siku yoyote naweza kuwa Rais wa nchi hii, sasa naweza kuja kubaguliwa kama anavyobaguliwa Rais, jambo hili si sahihi naomba vyombo vyetu hivi vikemee,” amesema Issa huku akikatishwa kwa taarifa kutoka kwa mbunge Anatropia.

Akitoa taarifa kwa mzungumzaji, Anatropia amesema:

“Nataka nimpe taarifa mchangiaji anayeongea vizuri sana, sisi tunaamini ni raia wamoja ni nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

“Lakini katika hali ya kusikitisha mbunge alisimama hapa bungeni akisema wanaotoka Bara wapatiwe pasipoti ya kwenda Zanzibar, sasa nataka kusema sisi ni nchi mmoja, hatuhitaji pasipoti ya kwenda Zanzibar au kuja Tanganyika,” amesema.

Mwenyekiti wa Bunge, Deo Mwanyika akamuuliza Issa kama anaipokea taarifa hiyo, naye akajibu: “Siipokei kwa sababu jambo hilo liko hadharani kila mtu amesikia, kuna kikundi cha watu akiwemo mwenyekiti (anamtaja jina) amekuwa akimbagua Rais na kikundi chake, sisemi kama (anakitaja chama), wamekuwa wakimbagua Rais, pamoja na mimi mwenyewe kwa kuweka hii hoja ya pasipoti,” akiendelea kuzungumza ikatolewa taarifa nyingine kutoka kwa Kunambi aliyesema:

“Nataka nimpe taarifa anayezungumza sasa, yeye si Mzanzibari, yeye ni Mtanzania.”

Kabla ya kuulizwa na Mwenyekiti wa Bunge, mbunge Issa akajibu: “Siipokei.”

Hata hivyo, mwenyekiti alimtuliza na kumuuliza kama anaipokea taarifa ya Kunambi.

“Siipokei, Tanzania ni Muungano, Zanzibar imeungana na Tanganyika, ikiwa ni nchi mbili huru na mimi naamini kwamba kuna Tanganyika na Zanzibar.”

Kabla hajamalizia, ikatolewa taarifa nyingine lakini nayo akasema haipokei na aachwe aendelee.

“Suala la pasipoti naomba mnipe muda niwaeleze vizuri, sina nia ya kuvunja Muungano.”

Wakati akiendelea kuzungumza ikaombwa taarifa nyingine kutoka kwa mbunge Conchesta.

“Nataka kumweleza mwenzetu kwamba sisi Watanganyika na Wazanzibari ni kitu kimoja. Na wakati mwingine watu wakikosa hoja wanatafuta hata sababu tu kusema.  Kwa hiyo, yule alikosa hoja ya kusema na Watanzania wote tunajua hayo. Aridhie kwamba yeye ni Mtanzania mwenzetu,” amesema.

Mwenyekiti Mwanyika alipomuuliza kama anaipokea taarifa hiyo alijibu:

“Siipokei, nataka nitoe mfano, Chadema ilimweka mgombea Edward Lowassa (Uchaguzi Mkuu wa 2020) na mgombea mwenza alikuwa Babu Juma Duni Haji.”

“Tuseme leo angekuwa Rais Babu Juma Duni Haji wangesema wamemkopa. Hili jambo si sahihi, ubaguzi huu hatuutaki. Na suala hili nililosema la pasipoti nifuateni niwape ufafanuzi mtaelewa tu, sikuwa na nia ya ubaguzi. Wazanzibari waingie Bara kwa pasipoti Watanzania Bara waingie Zanzibar kwa pasipoti na hakuna tatizo, ni suala tu la kulinda visiwa,” amesema.

  

Kauli ya Nyerere

Wakati akizungumzia nyufa tatu zinazolikabili Taifa mwaka 1995, hayati Julius Nyerere, Rais wa kwanza wa Tanganyika na baadaye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alikemea ubaguzi.

“Tunachotaka ni kwamba nyufa hizo zieleweke na tukubaliane kwamba kazi yetu ni kuziziba. Na tupate uongozi unaoelewa hivyo, kwamba kazi ni kuziba nyufa tulizoziona katika Taifa letu. Kazi si kuendelea kulitikisa Taifa. Litabomoka. Halitabaki. Sasa nyufa gani hizo. Ya kwanza mliniambia Muungano Mwalimu. Ufa wa kwanza ni Muungano. Wote mnajua. Mnaniambia ‘Mwalimu Muungano sasa ni imara zaidi kuliko miaka 20 iliyopita?’

Watu wamezungumza Uzanzibari. Baadhi ni viongozi wetu. Wanajivunia Uzanzibari. Nadhani wengine wanafikiria hata kujitenga. Wapo, si wengi, lakini wapo.

Kujitenga maana yake ni kuvunja nchi. Ivunjike. Tusiwe na nchi moja tuwe na nchi mbili. Ni jambo linazungumzwa. Tunataka kiongozi na viongozi watakaoelewa hivyo.

Huu, kuzungumza Uzanzibari si fahari. Si jambo la fahari. Hatima yake mtavunja nchi. Zanzibari. Mtu mwenye akili hawezi kufikiri Mzanzibari hana akili. Hawezi akautukuza Uzanzibari kwa kujiita sisi Wazanzibari na wao Watanganyika. Sisi Wazanzibari na wao Watanganyika.

Nadhani ile ina usalama ndani yake. Kwamba Uzanzibari ule na Utanganyika ule una usalama ndani yake. Hatima yake Zanzibar itajitenga.

Zanzibar ikijitenga kutokana na ulevi tu, ‘sisi Wazanzibari wao Watanganyika’, ulevi tu, ulevi hasa ulevi wa madaraka. Ikitokea hivyo kwamba ‘sisi Wazanzibari na wao Watanganyika’, wakumbuke kwamba Muungano ndiyo unaowafanya wanasema sisi Wazanzibari wao Watanganyika.

Nje ya Muungano hawawezi kusema hivyo. Nje ya Muungano hakuna Wazanzibari. Nje ya Muungano kuna wao Wapemba sisi Waunguja. Nataka mjue hivyo. Nataka mjue hivyo. Nje ya Muungano hakuna sisi Wazanzibari wao Watanganyika. Hakuna.

Mtamaliza, mtatengana na Watanganyika halafu mara mtakuta kumbe sisi si Wazanzibari. Kuna Wapemba kuna Waunguja. Mtakuta hivyo.

Wapemba watapata msukosuko kidogo aah ooh! Mtakuta kumbe kuna Wazanzibari na Wazanzibara. Hamtakaa salama. Hamwezi kukaa salama baada ya kutenda dhambi ya kubagua watu wa nchi yenu ileile moja. Mkawaita wale wao na hawa sisi.

Dhambi ile haiishii hapo. Ndivyo historia ilivyo. Ni sheria ya historia si sheria ya Mwalimu Nyerere. Huwezi kufanya ubaguzi wa namna hiyo halafu dhambi ile ikuache papo hapo, hapana. Itakuandama.

Namalizia hilo hapo. Ninalolisema kwa Wazanzibari nalisema kwa Watanganyika. Zanzibar wanaweza wakajitenga. Wanaweza wakajitenga hivi kwa ujinga, kwa ulevi, kwa ujinga hata kwa ujinga wa viongozi wao wanaweza kujitenga. Wanaweza wakajitenga hivi.

Na Watanganyika wakabaki wameduwaa tu. ‘Loh Wazanzibari hawa wamefanyaje. Wanatuacha wenzetu hawa wanatuacha jamani. Wanakwenda zao wenzetu’

Wakawaacha Watanganyika wameduwaa. Watanganyika walioachwa wameduwaa kwa kitendo cha Wazanzibari kuwakimbia watabaki wamoja. Hawataparaganyika. Narudia. Wazanzibari wanaweza wakatoka. Wakajitenga wenyewe tu. ‘Sasa wengine wana bendera sisi hatuna bendera kwa nini wengine wana wimbo wa taifa sisi hatuna, kwa nini,’ basi … si wote wanaosema hivyo, ni viongozi wanaosema hivyo. Basi, halafu wakajitenga. Wakawaacha Watanganyika wameduwaa.

Wakiwaacha Watanganyika walio katika hali hiyo, Watanganyika wanaowashangaa Wazanzibari katika kuwaacha, Watanganyika hao watakuwa salama. Watakuwa salama. Watanganyika wakiwakataa Wazanzibari, kwa tendo la dhambi ileile, ‘sisi Watanganyika, wao Wazanzibari’. Wakautukuza usisi Tanganyika. Na kwa hiyo wakawafukuza Wazanzibari. Hawabaki salama. Hapatakuwa na Tanganyika. s