Mbunge ataka bajeti itengwe kuongeza kata, mitaa, vitongoji

Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Emmanuel Mwakasaka akizungumza wakati akichangia mjadala kuhusu taarifa ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2024/2025 bungeni leo Aprili 4, 2024.

Muktasari:

  •  Mbunge Emmanuel Mwakasaka ameiomba Serikali iongeze maeneo ya kiutawala kwa kuwa idadi ya Watanzania imeongezeka hadi kufikia milioni 61, ashangazwa mitambo ya umeme kuzimwa kwa sababu ya maji mengi.

Dodoma. Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Emmanuel Mwakasaka ameitaka Serikali itenge bajeti kwa ajili ya kuongeza maeneo ya kiutawala kutokana na ongezeko la idadi ya watu Tanzania baada ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

 Mwakasaka amesema hayo bungeni leo Alhamisi Aprili 4, 2024 alipochangia mjadala kuhusu taarifa ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2024/2025.

“Tumefanya sensa, lakini nina hoja ya kuongeza maeneo ya utawala, mahali popote panapokuwa na ongezeko la watu, lazima vitu vitabadilika tu, lakini baada ya sensa ukiangalia maeneo ya utawala kwa mfano, kata zetu ni zile-zile baada ya sensa hii, mitaa ni ile-ile, vitongoji ni vile-vile,” amesema na kuongeza:

 “Suala la utoaji huduma kwa kuwa watu wameongezeka inakuwa shida, mimi ningeishauri Serikali iangalie upya namna ya kugawa maeneo kwa kutenga bajeti ambayo itarahisisha ugawaji wa maeneo.”

Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 yanaonyesha Tanzania ina idadi ya watu 61,741,120, kati ya hao 59,851,347 wapo Tanzania Bara na watu 1,889,773 wapo Zanzibar.

Kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita Tanzania ilikuwa na watu 44,928,923, hivyo  kuna ongezeko la watu 16,812,197 sawa na ongezeko la asilimia 3.2 kati ya mwaka 2012 na mwaka 2022.

Kukatika umeme

Mwakasaka pia alizungumzia kukatika kwa umeme akishauri Serikali inunue mitambo itakayofanya kazi kwenye mazingira yoyote.

Amesema bado kuna tatizo la kukatika umeme na hivi karibuni ulikatika kwa zaidi ya saa nane kwenye maeneo mengi ya nchi.

“Moja ya sababu ambayo imetolewa ni kwamba maji sasa yamezidi, sijui mvua zimezidi, sasa maji yanakwenda kwenye mitambo yanaharibu mitambo,” amesema.

Amesema alitarajia suala hilo wangekuwa wameliona na Serikali ingekuwa imechukua tahadhari kwamba maji hata yakizidi, basi mitambo isizimwe kwa sababu maji yamezidi.

“Niliona kwenye taarifa moja kwamba hata mitambo ya Bwawa la Julius Nyerere imezimwa kwa sababu hiyo, kwamba maji yalizidi yakawa yanaingia kwenye mitambo,” amesema.

Mwakasaka ameiomba Serikali kuliangalia hilo kwa sababu halijakaa sawa.

Bunge kuongeza eneo

Mwakasaka ameipongeza Serikali kwa kutwaa maeneo na hasa linalozunguka Bunge. 

“Serikali imetoa fidia ya bilioni 12 (Sh12.2 bilioni)   kwa ajili ya wale wakazi wanaozunguka maeneo ya Bunge kwa maana taasisi mbalimbali, wengine wameshaanza kuhama, lakini kuna baadhi bado wapo,” amesema.

Ameiomba Serikali kwa kuwa imeshalipa fidia ihakikishe ambao bado hawajaondoka, wanaondoka ili maeneo hayo yafanyiwe shughuli ambazo Bunge limepanga kuzifanya.

Ametoa mfano wa mabunge ya Kenya na Zambia kwamba yana eneo kubwa lenye huduma zote kwa ajili ya wabunge.

“Sisi hata wakija wageni humu tunakutana nao kantini, wakija wananchi wetu tunakutana nao kantini au nje ya Bunge, lakini hata magari ya wabunge mengi yanakaa nje na mengine mbali, kati ambacho ni hatari na hakiko salama,” amesema.

“Wenzetu kwa hizi nchi nilizozitaja na nyingine pamoja na Rwanda, maeneo ya Bunge ndiko kuna ofisi za wabunge humo-humo ambazo wanaweza kukutana na wapigakura wao,” amesema.


Kauli ya Kamati ya Bunge

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imesema mwaka 2023/2024, Sh12.215 bilioni zilitolewa kwa ajili ya kulipa fidia kwa wamiliki wote wa maeneo binafsi yanayolizunguka Bunge.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Omari Kigua amesema hayo jana akitoa maoni ya kamati kwamba ulipaji huo ulifanyika baada ya Serikali kutangaza katika gazeti la Serikali Toleo la 51 la Desemba 22, 2023.

“Utolewaji wa fedha hizo ni utekelezaji wa pendekezo la Tume ya Utumishi wa Bunge pamoja na Kamati ya Bunge ya Bajeti, ili kuongeza eneo la Bunge kutokana na mahitaji na sababu za kiusalama,” amesema.

Kigua amesema kamati hiyo inaipongeza Serikali kwa kutekeleza pendekezo la tume na kamati, na kwamba hatua hiyo inakwenda kuongeza ukubwa wa eneo la Bunge kutoka mita za mraba 42,312 hadi 165,236.

Amesema taratibu kuhusu utwaaji wa maeneo ya Umma yaliyo chini ya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), Wakala wa Ununuzi wa Serikali (GPSA), Machinjio ya Mifugo na Wakala wa Uhifadhi wa Chakula Taifa (NFRA) bado zinaendelea.