Mgawanyo wa majimbo waibuka bungeni
Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga akizungumza wakati akijibu maswali ya wabunge leo Jumanne Aprili 2, 2024. Picha na Merciful Munuo
Muktasari:
Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda ameirudisha bungeni hoja ya mgawanyo wa majimbo, Spika amjibu, Serikali yatoa ufafanuzi
Dodoma. Hoja ya mgawanyo wa majimbo imeibuka kwa mara nyingine bungeni baada ya mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda kuhoji Serikali ina mkakati gani kuhakikisha majimbo yanagawanywa ili kuainisha majimbo mapya.
Mei 3, 2023, hoja kama hiyo iliibuliwa na mbunge wa Kilindi, Omari Kigua aliyeuliza ni lini Serikali itagawa Jimbo la Kilindi kutokana na jiografia yake.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga amesema kwa kuzingatia taratibu na vigezo, muda utakapofika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itatoa tangazo rasmi kwa wadau ili wawasilishe maoni na maombi yao.
Amesema majimbo mengi yameomba kugawanywa, lakini mambo yanayotazamwa ni pamoja na ukubwa wa ukumbi wa Bunge, idadi ya wabunge wa viti maalumu, jiografia za maeneo yaliyoomba kugawanywa.
Hoja hiyo ya kugawanywa kwa majimbo imeibuka kwa mara nyingine leo Jumanne Aprili 2, 2024 wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni.
Kakunda amesema kuna majimbo makubwa kama Sikonge na kuwa wameshapitisha katika vikao vyote vya wilaya na mkoa.
“Serikali ina mkakati upi wa kuhakikisha kuwa majimbo yanagawiwa ili kuanisha majimbo mapya,”amehoji Kakunda.
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema wakati wakizungumzia majimbo makubwa pia kuna majimbo madogo.
“Lakini hii hoja ya mgawanyo wa majimbo sio ya Tamisemi (Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), kama Serikali ina majibu basi ijibu lakini kama hawana basi liulizwe kama swali la msingi ili tuje tupate majibu yatakayotupeleka sehemu nzuri,”amesema Dk Tulia.
Katika swali la msingi, mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara amehoji ni lini Serikali itatangaza maeneo mapya ya kiutawala.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Tamisemi, Dk Festo Dugange amesema uanzishaji wa maeneo mapya ya utawala huzingatia Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura 287 na (Mamlaka za Miji) Sura 288 pamoja na Mwongozo wa uanzishwaji wa Maeneo ya Utawala wa Mwaka 2014.
“Kwa sasa, Serikali imetoa kipaumbele katika kuboresha na kukamilisha miundombinu kwenye maeneo ya kiutawala yaliyopo, ili yaweze kutoa huduma kwa ufanisi zaidi na baadaye kuendelea na maeneo mengine kwa kufuata taratibu na vigezo vilivyoainishwa,”amesema.
Uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utafanyika mwakani huku maandalizi yake yakiwa yameshaanza.